‘Mkipata nafasi simamieni fedha za umma’

Muktasari:
Wahitimu Vyuo vya Uhasibu nchini wametakiwa kusimamia vyema fedha za umma pindi watakapo pata nafasi ya kuajiriwa ili kupunguza madudu katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mwanza. Wahitimu Vyuo vya Uhasibu nchini wametakiwa kusimamia vyema fedha za umma pindi watakapo pata nafasi ya kuajiriwa ili kupunguza madudu katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Wito huo umetolewa kufuatia uwepo wa mfululizo wa ripoti za CAG kila zinapotoka kuonyesha madudu na dosari kwenye taasisi na maeneo mbalimbali katika fedha na miradi nchini.
Akizungumza leo Ijumaa Novemba 24, 2023 katika mahafali ya 21 ya Chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Mwanza yaliyofanyika katika uwanja wa Nyangomango wilayani Misungwi mkoani Mwanza,
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elkana Balandya amewaomba wahitimu hao kuwa washauri wazuri wanaofuata sheria na taratibu za manunuzi ya Serikali.
"Miongoni mwa changamoto zinazotukabili ni usimamizi ubora wa matumizi ya fedha za umma... ripoti za CAG zimekuwa zikieleza juu ya ubadhilifu wa fedha za umma na wakati mwingine kwenye miradi ambayo Serikali inakuwa inatekeleza inakuwa haikamiliki vizuri. Niwaombe wahitimu mnapopata nafasi mkashauri vizuri na kusimamia vyema," amesema Balandya
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara TIA, Wakili Said Chiguma mbali na kuunga mkono hoja hiyo, amewataka wahitimu kuwa wazalendo na kuhakikisha wanaenda kutatua changamoto zinazoizunguka jamii ikiwa ni pamoja na tatizo la ukosefu wa ajira.
"Mwana falsafa mmoja kutoka India amewai kusema 'elimu isiyombadilisha mhitimu haina maana' kwahiyo wahitimu naomba mkawe wazalendo wa taifa lenu, nendeni mkawe wepesi wa kutafuta fursa lakini pia mkawe mfano kwa wenzenu katika kuhakikisha mnakabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira,”
Naye Rashidi Kishimba, Mhitimu katika Shahada ya Manunuzi na Ugavi chuoni hapo ameahidi kufanya kazi kwa bidii huku akihakikisha anapunguza madudu na dosari zinazobainika kwenye ripoti ya CAG.
"Tumepokea kauli hiyo vizuri na tumetambua kuwa kumbe thamani yetu ni kubwa hivyo cha kuwa ahidi ni kufanya kazi kwa bidii pindi tukipewa nafasi na tuweze kupunguza makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye ripoti ya CAG," amesema Kishimba
Jumla ya wahitimu 947 kwa mwaka 2022/23 katika chuo hicho Kampasi ya Mwanza wanatarajia kuhitimu masomo yao katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi katika ngazi tofauti huku kati ya hao wanawake wakiwa 526 na wanaume 421.