Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Jiungeni na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa’

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, uwazi, uwajibikaji na utawala bora ili kuhamasisha wanachama wengi zaidi kujiunga na vyama hivyo

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahimiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa ili kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo, ikiwamo huduma za kitaalamu, elimu ya kilimo na upatikanaji wa mitaji.

Akizungumza leo Jumapili Aprili 27, 2025 katika kongamano la sekta ya ushirika lililofanyika jijini Dodoma kuelekea uzinduzi wa Benki ya Ushirika utakaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kuimarisha ufuatiliaji wa watendaji wa vyama vya ushirika.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maadili, uwazi, uwajibikaji na utawala bora ili kuhamasisha wanachama wengi zaidi kujiunga na vyama hivyo.

 “Taasisi hizi zinapaswa kuwapa wakulima taarifa sahihi na zinazotekelezeka ili kujenga imani na kusaidia kufanya uamuzi bora,” amesema Majaliwa.

Amekitaja Chuo cha Ushirika Moshi kama sehemu muhimu inayosaidia kutoa wataalamu wa usimamizi wa vyama vya ushirika kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada.

Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kuimarisha masoko ya mazao kupitia vyama vya ushirika na taasisi za kifedha na kuhamasisha kuundwa kwa ushirika katika sekta mbalimbali.

Amesema lengo la kuwaunganisha watu wanaofanya shughuli za aina moja au tofauti ni kutaka kuongeza mtaji na kukuza biashara zao.

Akizungumzia changamoto, Majaliwa amesema sekta ya ushirika bado inakumbwa na matatizo ya usimamizi dhaifu, upungufu wa uadilifu na uaminifu kwa baadhi ya watendaji.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetoa mkopo wa Dola 129.71 milioni za Marekani kwa ajili ya kuendeleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora, inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta ya kilimo.
Amesema mkopo huo utasaidia vijana takribani 11,000 wenye miradi zaidi ya 6,000 kutimiza ndoto zao katika sekta hiyo.

Bashe pia, amesema katika mwaka 2023/24, jumla ya tani milioni 2.2 za mazao ziliuzwa kupitia vyama vya ushirika na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Amesema Sh4.2 trilioni zilipatikana ikiwa ni mafanikio makubwa kwa sekta ya kilimo nchini.

Pia, waziri huyo amesema kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika si kwa nia ya kuondoa benki nyingine, bali kuongeza nguvu ya kuwahudumia wakulima kwa kuwapatia mitaji na mikopo inayohitajika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.