Serikali yawaita wapiga kura siku ya uchaguzi, ikiwahakikishia usalama

Muktasari:
- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameulizwa maswali ya papo kwa hapo bungeni jijini Dodoma na miongoni mwa maswali limehusu usalama siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imeahidi siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 2025 hali ya usalama itakuwa nzuri na kila mtu atakayekwenda kupiga kura atakuwa salama katika eneo la kupigia kura, hadi kurudi nyumbani kwake.
Ahadi hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Aprili 24, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani.
Katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Khenan ameuliza ni namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wengi wanajitokeza kupiga kura kutokana na idadi ya wapiga kura kupungua kila mwaka.
Khenani ametolea mfano wa kupungua kwa wapiga kura kila uchaguzi akisema mwaka 2010 walijitokeza kwa asilimia 42.7, uchaguzi wa mwaka 2015 wakashiriki asilimia 65.3 na uchaguzi wa mwaka 2020 walipiga kura asilimia 57.7 akahoji nini mkakati wa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha hali hiyo haijitokezi?
Waziri Mkuu amesema kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo Serikali itashirikiana na wadau wengine ili kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, ikiwemo kuangalia ratiba na matukio ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
“Tume wanayo ratiba ya matukio yote kuanzia sasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, sisi Serikali tutahakikisha tunashirikiana katika kutoa elimu ya mpigakura hadi utakapofika uchaguzi ili wapiga kura wajitokeze kutumia haki yao,” amesema Majaliwa.
Amesema jukumu la kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ni la wadau wote ingawa lipo chini ya INEC, hivyo akaomba wanaohusika wote washiriki.
Tatizo la ukatili
Aidha, Majaliwa amekiri uwepo wa ukatili kwa makundi ya wanawake, wazee, watoto na wenye ulemavu lakini akasema Serikali ipo macho na itaendelea kuyalinda makundi hayo.
Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Fiyao aliyeuliza Serikali ina mkakati gani wa kuwalinda na kuwapa elimu wananchi ili kuondokana na ukatili ambao umeonekana kukithiri kwa jamii.
Waziri Mkuu amesema, upo mkakati wa kuwalinda Watanzania dhidi ya ukatili na yapo madawati maalumu ambayo yanashughulikia mambo hayo na kuratibu.
“Lakini tusisahau kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu ambayo inashughulika moja kwa moja na matatizo haya ikiwemo kutoa elimu,” amesema.
Hata hiyo, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuwa wepesi wa kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili, ili Serikali ichukue hatua kwa haraka na kushughulika na wahusika wanaotenda makosa hayo.
Waziri Mkuu pia amezungumzia huruma wanayopaswa kuwa nayo Watanzania kwa kuwasaidia watoto wanaoishi mitaani bila kuwa na wazazi.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa viti Maalumu, Ester Maleko ambaye ameuliza ni upi mkakati wa Serikali kuwasaidia watoto wa mitaani na kukomesha tabia ya watu kutelekeza watoto.
Majaliwa ametoa sababu za kuwapo kwa wimbi la watoto wa mitaani kuwa ni vifo vya wazazi, kutengana kwa wanandoa na wakati mwingine watu kutupa watoto wanaowazaa.
Ameiomba jamii kuendelea kuwabaini watoto wanaozagaa mitaani ili wawasaidie kupata huduma stahiki ikiwemo elimu, kwani hawawezi kujua mbeleni watakuwa akina nani watoto hao.