Jinsi ya kuwaepusha watoto na selimundu

Muktasari:
- Uchunguzi uliofanywa kwa watoto wachanga 5,000 waliozaliwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando, umebaini 1,300 kati yao wana ugonjwa wa selimundu sawa na asilimia 26, tatizo linalotajwa kukithiri katika maeneo ya ukanda wa kitropiki, yakiwamo maeneo ya kanda ya ziwa.
Mwanza/Dar. Uchunguzi uliofanywa kwa watoto wachanga 5,000 waliozaliwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando, umebaini 1,300 kati yao wana ugonjwa wa selimundu sawa na asilimia 26, tatizo linalotajwa kukithiri katika maeneo ya ukanda wa kitropiki, yakiwamo maeneo ya kanda ya ziwa.
Uchunguzi pia umebaini watoto 150 kati 1,300 wailiokutwa na selimundu, wamerithi ugonjwa huo kutoka kwa wazazi wote wawili.
Kihistoria inaelezwa kuwa wagonjwa wengi wa selimundu wanaishi katika ukanda wa kitropiki, Kanda ya Ziwa ikiwemo kulikoshamiri wagonjwa wengi wa malaria ambayo inatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa hitilafu kwenye vinasaba vinavyosababisha selimundu.
Ugonjwa huu ambao ni wa kurithi unasababishwa na hitilafu katika vinasaba vya damu na kusababisha damu kuwa nyepesi, jambo linalosababisha mgonjwa kuishiwa damu mara kwa mara, kupata nimonia, homa ya manjano na maumivu makali kwa mgonjwa.
Uchunguzi huo uliofanyika kwa mwaka mmoja umebaini kuna idadi kubwa ya watoto wenye ugonjwa wa selimundu, huku tabia ya wenza kufunga ndoa bila kufanya kipimo cha ugonjwa huo ikitajwa kuchangia.
Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa kitengo cha selimundu katika hospitali ya Bugando, Dk Emmanuela Ambrose alisema uchunguzi uliofanyika kuanzia Juni, 2021 hadi Juni 15, 2022 kwa watoto wachanga 5,000 waliozaliwa hospitalini hapo, umebaini watoto 1,300 wana ugonjwa wa selimundu.
Dk Ambrose alisema kabla ya kuanza kufanya uchunguzi wa selimundu kwa kila mtoto anayezaliwa hospitalini hapo, kliniki ya selimundu katika hospitali hiyo, ilikuwa inahudumia wastani wa wagonjwa wa selimundu 1,000 kwa mwaka.
“Uamuzi wa kufanya kipimo cha selimundu kwa kila kichanga kinachozaliwa hospitalini hapa ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi la kutaka uchunguzi wa tatizo hilo ili kubaini hali halisi ya ugonjwa kwenye mikoa ya ukanda huu,” alisema Dk Ambrose.
Alisema walibaini vichanga 150 kati 1,300 vilivyokutwa na selimundu vimerithi ugonjwa huo kutoka kwa wazazi wote.
Alisema ili kukomesha ongezeko la watu wenye ugonjwa wa selimundu, wazazi wanashauriwa kufanya kipimo cha ugonjwa huo kwa watoto, huku akisisitiza wenza kufanya kipimo hicho kabla ya kuchukua uamuzi wa kubeba ujauzito.
“Kuna mbinu za kisayansi za kuepuka ugonjwa huo kutoka kwa mzazi kwenda kwa mtoto, ndiyo maana tunasisitiza wanandoa kufanya kipimo cha selimundu kabla ya kufanya uamuzi wa kupata mtoto,” alisema Dk Ambrose.
“Kihistoria kanda hii ina wagonjwa wengi wa selimundu wanaoishi katika ukanda wa kitropiki ambayo ni pamoja na kanda ya Ziwa. Ukanda huu una wagonjwa wengi wa malaria ambayo ndiyo inatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kusababisha hitilafu kwenye vinasaba,” aliongeza daktari bingwa huyo wa ugonjwa wa selimundu.
Dk Ambrose alisema ili kuhakikisha wagonjwa wa selimundu wanapata huduma ya matibabu kwa haraka na uhakika, Hospitali ya Bugando imesambaza madaktari bingwa kwenye kila kitengo ili kurahisisha ubainishaji wa wagonjwa wanaofika kutibiwa hospitalini hapo.
“Kila kitengo kuna mtaalamu wa selimundu na tunafanya kazi kama timu, ikitokea mgonjwa amekuja kutibiwa tatizo lingine Bugando lakini akabainika kuwa na selimundu tunawasiliana naye na kumwanzishia tiba.”
Pia alisema hospitali hiyo ina utaratibu wa kutoa huduma ya upimaji wa selimundu bila malipo mara kwa mara kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, ili kuongeza uelewa na kupata takwimu itakayosaidia kutambua ukubwa wa tatizo hilo.
Imani potofu
Dk Ambrose alisema idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki ya selimundu katika hospitali hiyo kabla ya kugundulika kusumbuliwa na ugonjwa huo, walihusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina.
“Wagonjwa wengi wanaohudhuria kliniki hapa Bugando kabla hatujawapa elimu juu ya tatizo hili walikuwa wanasema wanaamini wamelogwa, jambo ambalo siyo kweli,” alisema.
Alisema ili kuondoa imani hiyo, Hospitali ya Bugando inaendesha kliniki inayotembea katika maeneo na taasisi za umma Kanda ya Ziwa kutoa elimu juu ya chanzo, dalili na athari za ugonjwa huo.
“Kwa upande wa Tanzania, mikoa ya Kanda ya Ziwa inaongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu. Siyo tu wanaotibiwa Bugando bali hata wanaoenda kutibiwa Muhimbili,” alisema Dk Ambrose.
Mkurugenzi wa Tiba katika hospitali hiyo, Dk Bahati Wajanga aliiomba jamii kutumia siku ya selimundu duniani kufanya uchunguzi wa afya kwa watoto wao ili kubaini changamoto za kiafya zinazowakabili na kuanza matibabu mapema.
“Ni jukumu la kila mtu katika jamii kuhakikisha ulinzi wa mtoto unaimarishwa ili kuwaepusha dhidi ya hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili. Ukatili unaoongoza ni kubakwa, kulawitiwa, shambulio la aibu, kipigo na utumikishwaji wa watoto,” alisema Dk Wajanga.
Hali ilivyo
Wakati namba ya Watanzania wenye vinasaba vya ugonjwa wa selimundu na watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo ikikua, zipo njia zilizotajwa kuzuia tatizo hilo.
Tanzania inapotajwa kushika nafasi ya nne kidunia kwa kuwa na wagonjwa wengi, watoto 11,000 wenye selimundu huzaliwa kila mwaka huku wenye vinasaba vya ugonjwa huo wakiongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2016 mpaka asilimia 20 kwa mwaka 2021.
Arafa Salim Said amefanikiwa kuishi kwa miaka 35 tangu alipogundulika kwa mara ya kwanza kuwa na ugonjwa huo akiwa na umri wa miezi minane, alisema zipo changamoto nyingi zinazowakumba wagonjwa wa selimundu katika maisha.
Alisema kuishi na ugonjwa huo kunaathiri mambo mengi sana kuanzia kwenye elimu, uhusiano na ajira, kuishi kwa maumivu ya mwili na unyanyapaa.
“Lakini pia kuna upande wa uhusiano ambako kwa kuwa bado hakuna uelewa wa kutosha, inakuwa vigumu sana kumkubali mtu anayeishi na ugonjwa huo, kwani ukiachilia mbali dhana ya kifo, pia wengi huamini kuwa mgonjwa wa selimundu ni mtu asiyefaa kwenye jamii,’’ alibainisha Arafa, ambaye ni mwasisi wa jumuiya ya Mashujaa wa Sickle cell Tanzania.
Matibabu
Ugonjwa huu wa kurithi hutokea baada ya mwili wa binadamu kuwa na upungufu katika umbile la seli hai nyekundu za damu ambazo muda wake wa kuishi unapofikia ukomo, zinapokuwa katika mzunguko wa damu husababisha damu kushindwa kufika katika baadhi ya viungo mwilini kama vile mapafu, figo na ini.
Hiyo hutokana na seli kuziba mishipa ya damu na matokeo yake ni kusababisha viungo hivyo kushindwa kupata hewa ya kutosha, sukari, virutubisho na hatimaye kuumia kwa viungo hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema tayari nchi imeanzisha matibabu ya kisasa ambapo mtoto anayezaliwa na ugonjwa wa selimundu akigundulika mapema hutibiwa na kupona kabisa.
Profesa Makubi alisema tayari nchi imeanza kupandikiza uboho (bone marrow) kwenye mifupa kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo ambapo tayari Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanza kutoa huduma tangu mwaka 2021.
“Mafanikio haya yametokana na tafiti zilizofanywa ili kutibu ugonjwa huu, ikiwamo ya kupandikiza uboho na vinasaba. Hii ni mikakati ya kuhakikisha tunawatibu wagonjwa wa selimundu na watoto wakiwa bado wachanga.
“Tutafunga mifumo ya kubaini ugonjwa huu ili kila mtoto anapozaliwa ajulikane mapema na kupokea matibabu. Kwa sasa mashine hizi zipo katika hospitali kubwa pekee, Serikali imepanga kufikia mwaka 2026 tuwe tumefikisha vipimo hivi katika hospitali za ngazi za chini ili watoto 11,000 wote tuwabaini na kuwatibu mapema,” alisema Profesa Makubi.
Alitaja njia nyingine za kupunguza idadi ya watoto wenye selimundu wanaozaliwa nchini na kupunguza wenye vinasaba iwapo wazazi wataamua kupima kabla hawajazaa mtoto, kwani idadi ya wenye vinasaba na wanaozaliwa inaongezeka.
Alisema wakati umefika sasa kwa Tanzania kuwa na kituo cha umahiri cha uchunguzi, tafiti na tiba dhidi ya ugonjwa huo.
“Ugonjwa huu unatesa watoto wengi, tutakuwa na kituo cha umahiri cha uchunguzi, tafiti zaidi na tiba dhidi ya ugonjwa huu ni mwelekeo wa Serikali katika kuukabili. Wizara itahakikisha inasimamia kwa dhati kufikia hili kwani ni muhimu.”
Mratibu wa taasisi Sparco Tanzania, Dk Agnes Jonathan alisema idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo inazidi kuongezeka lakini changamoto kubwa kwao ni upatikanaji wa damu.
Nyongeza na Herieth Makwetta