Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Bwana harusi’ afikishwa kortini akidaiwa kuiba gari

Mshtakiwa Vicent Massawe, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili yanayomkabili. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Vicent Masawe anadaiwa kuuza gari aliloazimwa kulitumia wakati wa harusi.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Vicent Masawe (36) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili, likiwemo la wizi wa gari aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni.

Masawe ‘bwana harusi’ inadaiwa gari hilo aliazimwa ili kulitumia wakati wa sherehe ya harusi yake.

Mshtakiwa huyo, mkazi wa Kigamboni amefikishwa mahakamani hapo leo, Jumanne Desemba 24, 2024 akikabiliwa na kesi ya jinai namba 35738 ya mwaka 2024.

Mshtakiwa amesomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Rimoy amedai mshtakiwa ameshtakiwa chini ya kifungu 258 na 273(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shtaka la kwanza, Masawe anadaiwa kuiba gari hilo akiwa wakala. Anadaiwa Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari namba T 642 EGU aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni mali ya Silvester Masawe.

Anadaiwa aliazimwa gari hilo na Silvester kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake lakini baada ya hapo, hakulirudisha kama walivyokubaliana.

Shtaka la pili anadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kosa analodaiwa kulitenda Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo anadaiwa kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia Sh3 milioni kutoka kwa Silvester akidai atamrudishia, wakati akijua kuwa ni uongo na hakuweza kurudisha fedha hizo hadi alipokamatwa.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika umeomba tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.

Mshtakiwa Vicent Massawe, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili yanayomkabili. Picha na Hadija Jumanne

Kuhusu dhamana, wakili Rimoy amedai upande mashtaka hauna pingamizi isipokuwa mahakama itoa masharti ambayo yatamfanya mshtakiwa ahudhurie mahakamani kila kesi inapotajwa.

Hakimu Nyaki alitoa masharti mawili ya dhamana kwamba, awe na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Pia, anatakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh9 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Hakimu Nyaki baada ya kutoa masharti hayo, alimuuliza mshtakiwa iwapo wadhamili wake wamefika mahakamani, baadhi ya maswali yakiwa yafuatayo:

Hakimu: Wadhamini wako wapo mahakamani hapa?

Mshtakiwa: Nimeambiwa wapo, wife (mke) yupo njiani wanakuja, hivyo naomba mahakama yako inipe muda kidogo kwa sababu Polisi hawakuniambia kama leo wananileta mahakamani.

Hakimu: Kuhusu kiasi hiki cha mali?

Mshtakiwa: Zitapatikana mheshimiwa hakimu.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, kwa sababu hilo gari lipo na nyaraka zake zipo, ninaweza kulileta mahakamani likatumika kama dhamana kwenye kesi hii?

Hakimu: Gari inayobishaniwa kwenye kesi hii ni yako? Au ni ya nani?

Mshtakiwa: Ndiyo mheshimiwa, gari inayobishaniwa ni yangu

Hakimu: Nimesema mali yoyote isiyohamishika, sasa gari si linahamishika na baadaye gari hilo linaweza kutumika kama kielelezo kwenye kesi hii.

Hakimu Nyaki amesema iwapo wadhamini watafika muda wa kazi na watatimiza masharti aliyotoa mshtakiwa atapata dhamana, asipokamilisha atarudishwa rumande.

Baada ya kueleza hayo, Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2025 kesi itakapotajwa. Mshtakiwa amepelekwa rumande.