Mapya bwana harusi aliyepotea na kupatikana Pemba

Muktasari:
- Kamanda Muliro amesema katika kumuhoji Massawe alikiri alichukua fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Ramadhani Bakari Sh15 milioni, mkazi wa Temeke.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Vincent Massawe, bwana harusi aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha likisema alikuwa amejificha kwa mganga wa kienyeji Chakechake Mgogoni kisiwani Pemba.
Vincent (35), mkazi wa Ungindoni Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa alipotea Novemba 18, 2024 baada ya kuisha harusi yake. Novemba 19, taarifa za kupota kwake zilifikishwa polisi Kigamboni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 17, 2024, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema baada ya uchunguzi wamebaini alitengeneza mazingira ya uongo kupotosha umma kuwa ametekwa.
Kamanda Muliro amesema Vincent ana madeni na ameuza mali za watu, hivyo ilikuwa sababu ya kwenda kujificha.
Amesema Desemba 15, Jeshi la Polisi lilimkamata akiwa amejificha kwa mganga wa kienyeji.
“Tulimkamata Vincent Massawe maarufu Baba Harusi, mkazi wa Kigamboni kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wizi wa kuaminiwa baada ya kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea na kutengeneza hisia kwa umma,” amesema.
Kamanda Muliro amesema Vincent alijificha kwa mganga wa kienyeji Hamis Khalid, huku akieleza uchunguzi wa mashauri yake, likiwemo la wizi na kutapeli fedha za watu, unaendelea na atafikishwa kwa mamlaka zingine za kisheria kwa hatua zaidi.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuwa watulivu pindi wanapopata taarifa kuhusu matukio ya namna hii na kuviachia vyombo vya kiuchunguzi kufanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka zingine na wananchi,” amesema.
Muliro amesema katika ufuatiliaji na mahojiano ya kina kati yake na Polisi, Vincent alikiri kutenda makosa hayo, akidai alichukua fedha kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali.
“Amekiri kuchukua Sh55 milioni na gari namba T642 EGU aina ya Toyota Ractis kwa udanganyifu kutoka kwa Sylivester Massawe, alichukua tena Sh10 milioni kutoka kwa Ramadhani, mkazi wa Magomeni,” amesema.
Kamanda Muliro amesema katika kumuhoji Massawe alikiri alichukua fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Ramadhani Bakari Sh15 milioni, mkazi wa Temeke.
“Mtuhumiwa alichukua pesa kwa udanganyifu Sh5 milioni kutoka kwa Rasma Mbugumi, alichukua pesa nyingine Sh1.5 milioni kutoka kwa Ngoma mkazi wa Kibaha, alichukua Sh4 milioni kutoka kwa Asia Mohamed, mkazi wa Madale,” amesema.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro
Mbali na udanganyifu huo, amesema alichukua Sh8 milioni kutoka kwa Fauz Suleiman Mussa, mkazi wa Tabata baada ya kumuuzia gari ambalo si mali yake aliloliazima siku ya harusi yake.
“Gari lilikuwa namba T 642 EGU Toyota Ractis mali ya Sylivester Massawe. Tunakionya na kukitahadharisha kikundi cha watu wanne ambao kazi yao ni kujenga taharuki na kuandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa mtuhumiwa huyo alipotea baada ya kuchukuliwa na gari nyeupe aina ya hardtop,” amesema.
Sylivester aliyekuwapo kituo kikuu cha polisi leo Desemba 17, amekiri alimuazima gari Vincent baada ya kumuomba kulitumia kuwabeba watu kwenda kwenye harusi na walikubaliana siku ya pili angelirejesha.
“Nilipompigia simu kesho yake ili anirejeshee gari langu alikuwa hapatikani kwenye simu nikasubiri siku iliyofuata hakuonekana. Nilichukua hatua ya kwenda kuripoti Polisi na kufanya jitihada za kutafuta gari,” amesema.
Amesema alitafuta gari lake kwa takriban wiki nzima baadaye alipigiwa simu na fundi wake aliyekuwa akilitengeneza, akamweleza ameliona.
“Baada ya kufuatilia hadi sehemu aliyonieleza nilikuta gari lipo lakini linakwanguliwa rangi, lilikuwa halijafanyiwa chochote. Mafundi tulipowauliza walidai wameuziwa tangu Novemba 18, mwaka huu,” amesema.
Desemba 15, msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akizungumzia tukio hilo alisema taarifa za kupotea Massawe zilifikishwa Kituo cha Polisi Kigamboni Novemba 19, 2024 na mke wa Vincent. Alisema upelelezi ulithibitisha alikuwa na harusi Novemba 16, 2024.
Alisema Novemba 18, Vincent alidai alikuwa anafuatiliwa na gari ambayo alikuwa anaitilia shaka na kwamba, siku hiyohiyo aliuza gari aliloazimwa, kwa Sh9 milioni akalipwa Sh8 milioni ikabaki 1 milioni.
Kamanda Misime alisema siku hiyohiyo alimtumia mke wake fedha ili alipe madeni mengine yaliyotokana na harusi ikiwemo Toyota Coaster aliyokodi kuwarejesha wageni wake Moshi.