Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahouthi warusha kombora la ‘Balistic’ nchini Israel, Trump aionya Iran

Muktasari:

  • Tangu kuanza kwa operesheni ya IDF eneo la Gaza Oktoba 7,2023, Ofisi ya Habari ya Serikali ya Gaza ikidai kuwa idadi ya vifo ni zaidi ya 61,700, na zaidi ya 200 walitekwa. Inaelezwa maelfu ya Wapalestina bado wapo chini ya vifusi huku takriban watu 1,139 wakiuawa nchini Israel tangu kuanza mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas Oktoba 7, 2023.

Jerusalem. Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema limefanikiwa kuzuia kombora la ‘Balistic’ lililorushwa na waasi wa Kihouthi kutoka nchini Yemen.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, shambulizi hilo lililofanyika usiku wa kuamkia leo Alhamisi Machi 20,2025, ni la mara ya kwanza katika kipindi cha miezi miwili tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitishwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas la Gaza nchini Palestina.

“Kombora hilo lilidunguliwa kabla ya kuingia kwenye anga ya nchi hiyo. King’ora cha tahadhari kililia kuonyesha hali ya hatari kwa umma,” IDF iliandika katika mtandao wa X.

Msemaji wa kijeshi wa kundi la Wahouthi, Ameen Hayyan, amesema kuwa kombora hilo lilielekezwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion nchini Israel.

Wahouthi wanadhibiti sehemu kubwa ya magharibi mwa Yemen, ikiwemo mji mkuu wake, Sanaa.

Kundi hilo limekuwa likiendesha mashambulizi yake kwenye meli za kimataifa na kurusha makombora kuelekea Israel kama hatua ya kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya IDF dhidi ya Hamas huko Gaza.

Mwishoni mwa wiki, Rais wa Marekani Donald Trump aliamuru mashambulizi ya anga na makombora ya masafa marefu dhidi ya ngome za wahouthi huko Yemen. Jumatano, alionya kuwa Marekani italifutilia mbali kundi hilo.

Kiongozi wa waasi wa Kihouthi, Abdul-Malik al-Houthi, aliahidi kuendelea na mashambulizi kwa ajili ya kulipiza kisasi cha Wapalestina wanaoishi Gaza.

“Tutafanya kila tuwezalo dhidi ya adui wa Kizayuni (Israel) na kuwaunga mkono watu wa Palestina. Tutapambana na msaada wowote wa Marekani kwa Israel ambao utahusisha kushambulia nchi yetu,” kwa mujibu wa tovuti ya habari ya The New Arab.

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel yalivunjika wiki hii baada ya pande hizo kushindwa kufikia maelewano.

Jeshi la Israel lilirejesha tena mashambulizi yake ya anga huko Gaza Jumanne na limeendelea na operesheni zake za ardhini, huku takwimu zikionyesha kuwa zaidi ya watu 400 wameuawa ndani ya siku tatu.

IDF kupitia operesheni zake za ardhini imerejesha udhibiti wa Ukanda wa Netzarim ulioko kusini mwa Jiji la Gaza nchini Palestina.

Wakati huohuo, Donald Trump ameitaka Iran kusitisha msaada wake wa kijeshi kwa Wahouthi, akiahidi kuwa kundi hilo lipo mbioni kufutwa kabisa na Marekani.

Matamshi ya Rais wa Marekani Jumatano yalikuja siku moja baada ya waasi wa Houthi kushambulia meli za kivita za Marekani katika eneo la Bahari Nyekundu na pia kurusha kombora kuelekea Israel.

Jumatano pia iliashiria siku nyingine ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za Wahouthi huko Yemen, ikiwemo mji mkuu Sanaa.

“Uharibifu mkubwa umetokea kwa waasi wa Kihouthi na mtashuhudia hali inavyozidi kuwa mbaya kwao haya si mapambano ya haki, na hayatakuwa hivyo kamwe. Watafutwa kabisa,” ameandika Trump katika mtandao wa kijamii wa Truth Social.

Mwezi huu, Marekani imefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya waasi wa Kihouthi, ambao wanajitangaza kama jeshi rasmi la Yemen.

Tangu mwaka 2023, Wahouthi wamekuwa wakishambulia meli katika eneo la Bahari Nyekundu na kurusha makombora kuelekea Israel kwa lengo la kuishinikiza serikali ya Israel kukomesha vita dhidi ya Gaza.

Utawala wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Joe Biden pia ulifanya mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi, lakini kampeni hiyo haikufanikiwa kuwazuia kuendelea na mashambulizi yao.

Katika ujumbe wake wa mtandaoni Jumatano, Trump alidai kuna ripoti zinazoonyesha kuwa Iran inapunguza msaada wake kwa Wahouthi lakini bado inatuma vifaa kwa wingi.

“Iran lazima isitishe mara moja usambazaji wa vifaa hivi. Wahouthi wajipiganie wenyewe. Vyovyote iwavyo watashindwa, lakini kwa njia hii watashindwa haraka,” ameandika Trump. Ambapo pia ameitishia Iran kuwa itaichukulia hatua kali iwapo itashindwa kuwadhibiti waasi hao wa Kihouthi.

Ingawa Wahouthi wanaojulikana rasmi kama Ansar Allah wana uhusiano wa karibu na Iran, haiko wazi ni kwa kiwango gani wanategemea msaada wa Iran ama iwapo Iran inaweza kuwaamuru waache mashambulizi yao.

“Kila risasi inayorushwa na Wahouthi itachukuliwa, kuanzia sasa, kama shambulio lililoratibiwa na silaha na uongozi wa Iran na  itawajibishwa na itaathirika vibaya na madhara hayo yatakuwa makubwa sana,” Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii Jumamosi, wakati mashambulizi ya Marekani dhidi ya Houthi yalipoanza tena.

Kwa upande wao, Wahouthi wamepuuza vitisho na mashambulizi ya Marekani, wakiahidi kuendelea na mashambulizi yao hadi Israel itakapositisha mashambulizi yake huko Gaza.

“Jeshi la Yemen linathibitisha kuwa uchokozi wa Marekani hautaizuia kwani wapo thabiti na wanapigana  kutekeleza wajibu wao kidini, maadili na kibinadamu kwa watu wa Palestina,” lilieleza kundi hilo katika taarifa yake ya Jumanne ya wiki hii.

Trump aliliongeza kundi la Kihouthi kwenye orodha ya makundi ya kigaidi ya kigeni mwanzoni mwa urais wake mwaka huu. Utawala wa Biden hapo awali nao uliwapa Wahouthi hadhi ya magaidi wa kimataifa walioteuliwa rasmi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya eneo la Gaza, mashambulizi ya wiki hii yameua takriban Wapalestina 436, wakiwemo watoto 183.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.