Ramaphosa achaguliwa kuwa Rais Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Muktasari:
- Serikali mpya ya umoja wa kitaifa inaunganisha ANC ya Ramaphosa, Chama cha Democratic Alliance (DA) na vyama vidogo kikiwamo cha Inkhata Freedom Party
Afrika Kusini. Bunge la Afrika Kusini limemchagua tena Cyril Ramaphosa kuwa Rais wa nchi hiyo kufuatia makubaliano kati ya chama tawala cha African National Congress (ANC) na vyama vya upinzani.
Serikali mpya ya umoja wa kitaifa inaunganisha ANC ya Ramaphosa, Chama cha Democratic Alliance (DA) na vyama vidogo kikiwamo cha Inkhata Freedom Party.
Katika hotuba yake ya ushindi, Ramaphosa ameusifu muungano huo mpya na kusema wapigakura wanatarajia viongozi kuchukua hatua na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya kila mtu katika nchi yetu.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kutokea mvutano mrefu jana Juni 14, 2024, Bunge lilikaa hadi jioni kwa ajili ya kura za kuthibitisha nani atashika madaraka katika utawala mpya.
Awali, makubaliano yalifikiwa kufuatia wiki za uvumi kuhusu chama kipi ANC itashirikiana nacho baada ya kupoteza wingi wa viti bungeni kwa mara ya kwanza katika miaka 30 katika uchaguzi wa mwezi uliopita.
ANC ilipata asilimia 40 ya kura, wakati DA ilishika nafasi ya pili kwa asilimia 22. Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula ameeleza makubaliano hayo ya muungano kama "hatua ya ajabu."
Makubaliano hayo yalifanya Ramaphosa aliyemrithi Jacob Zuma kama Rais na kiongozi wa ANC kufuatia mapambano makali ya madaraka mwaka 2018 ili aweze kubaki madarakani.
Hatua inayofuata ni kwa Ramaphosa kugawa nafasi za baraza la mawaziri, zitakazojumuisha wanachama wa DA.
Makubaliano ya vyama vingi hayausishi vyama viwili vilivyojitenga na ANC na pengine vitafaidika kama hayatatoa maboresho ya kiuchumi yanayodaiwa na wapigakura.
ANC imekuwa ikipata zaidi ya asilimia 50 ya kura tangu uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia wa nchi hiyo mwaka 1994, ambao ulimfanya Nelson Mandela kuwa Rais.
Hata hivyo, uungwaji mkono kwa chama hicho umekuwa ukipungua sana kutokana na hasira juu ya viwango vya juu vya ufisadi, ukosefu wa ajira na uhalifu.
Akilihutubia Bunge la Afrika Kusini baada ya kuthibitishwa kwake, Ramaphosa alikumbusha ushindi wa kwanza wa urais wa chama chake miaka 30 iliyopita.
"Tumekuwa hapa awali, tulikuwa hapa mwaka 1994, tulipotafuta kuunganisha nchi yetu na kuleta maridhiano na tuko hapa sasa," amesema Ramaphosa.
Muungano kati ya DA na ANC haujawahi kutokea kwa kuwa vyama hivi viwili vimekuwa wapinzani kwa miongo kadhaa.
Chini ya uongozi wa Nelson Mandela, ANC iliongoza kampeni dhidi ya mfumo wa kibaguzi wa apartheid na kushinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia wa nchi hiyo.
Wakosoaji wa DA wamekilaumu kwa kujaribu kulinda masilahi ya kiuchumi ambayo Wazungu walijijengea wakati wa apartheid, tuhuma ambazo chama hicho kinazikanusha.
Akilihutubia Bunge Ijumaa jioni huko Cape Town, John Steenhuisen, kiongozi wa DA, amesema: "Leo ni siku ya kihistoria kwa nchi yetu na nadhani ni mwanzo wa sura mpya."
Bunge pia liliapisha spika kutoka ANC, huku nafasi ya naibu spika ikienda kwa DA. Miongoni mwa viongozi wa vyama waliotoa hotuba baada ya makubaliano kufikiwa Ijumaa alikuwa Julius Malema, mkuu wa Economic Freedom Fighters, chama alichokianzisha baada ya kuondoka ANC mwaka 2013.
Amesema ingawa chama chake kinakubali matokeo na sauti ya watu wa Afrika Kusini, lakini alikosoa makubaliano hayo, akisema: "Hatuafikiani na ndoa hii ya mkataba, ili kuimarisha nguvu ya ukiritimba wa Wazungu juu ya uchumi na njia za uzalishaji nchini Afrika Kusini."
Imetafsiriwa kutoka BBC.