Prime
Ramaphosa katika mtanziko Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala cha African National Congress (ANC) akizungumza na wananchi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- ANC inakabiliwa na changamoto kubwa kisiasa kuliko wakati mwingine wowote tangu mwaka 1994.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Mei 29, 2024 nchini Afrika Kusini, chama tawala cha African National Congress (ANC) kilikabiliwa na changamoto kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Matokeo ya uchaguzi huo yalionyesha kuporomoka kwa umaarufu wa ANC, hivyo kukosa wingi wa kura unaohitajika kuunda serikali peke yake. Hali hii imekilazimu chama hicho kutafuta njia mbadala za kuunda serikali.
Rais Cyril Ramaphosa Alhamisi iliyopita alisema chama chake cha ANC kinatarajia kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), baada ya kushindwa kupata wingi wa kura katika uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita.
Baada ya saa kadhaa za majadiliano, Ramaphosa alisema uongozi wa ANC umeamua kujaribu kuungana na kundi kubwa la vyama vya upinzani, kuanzia vile vya mrengo wa kulia hadi mrengo mkali wa kushoto.
ANC ilishinda asilimia 40 ya kura, ambao ni ushindi wa chini zaidi tangu kilipoingia madarakani mwaka 1994, na kwa mara ya kwanza katika historia yake kinahitaji kuungwa mkono na makundi mengine ili kubaki madarakani.
"Kwa hivyo tumekubaliana kwamba tutaalika vyama vya siasa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kama chaguo bora zaidi la kuendeleza nchi yetu," Ramaphosa alisema katika mkutano na waandishi wa habari juzi jioni.
Rais Ramaphosa anasema tayari wameshafanya mazungumzo na vyama kadhaa vikiwamo vya mrengo wa kushoto, Economic Freedom Fighters (EFF), chama cha Zulu Inkatha Freedom Party (IFP) na chama cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA). Haijafahamika iwapo wote wamekubali kujiunga nayo.
Kwa nini mseto au GNU
Lakini kwa nini ANC inataka GNU na si serikali ya mseto? Ni mfumo gani hasa wa serikali utakaoifaa Afrika Kusini kati ya hiyo miwili inayopendekezwa – mseto au GNU?
Kwa kuzingatia changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi zinazoikabili Afrika Kusini, ANC inalazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa au mseto ili kuimarisha utawala, kudumisha amani na utulivu na kuhakikisha maendeleo endelevu ya nchi. Ushirikiano huu ni muhimu kwa ajili ya kushughulikia matatizo yanayowakabili wananchi na kujenga Taifa lenye mshikamano na ustawi.
Kwa hiyo ANC inalazimika kuchagua moja ya njia mbili ili kuunda serikali.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ni mfumo wa utawala ambapo vyama vya siasa mbalimbali vinashirikiana kuunda serikali. Hii inaweza kufanyika kwa sababu ya haja ya kutatua matatizo makubwa ya kitaifa, au kutokana na hali ambayo hakuna chama kimoja kinachoweza kupata wingi wa kutosha kuunda serikali pekee.
GNU inalenga kuleta utulivu na mshikamano katika nchi, hasa baada ya uchaguzi wenye matokeo yasiyo ya kawaida au wakati wa mgogoro wa kitaifa.
ANC, ikiongozwa na Rais Ramaphosa, imeeleza nia yake ya kuunda GNU ili kuepuka kuunda serikali ya mseto na chama chochote cha upinzani.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, chama hicho kinapitia kipindi kigumu zaidi kisiasa, na kuunda GNU kunawapa fursa ya kushirikiana na vyama vingine katika kutatua changamoto za kitaifa bila kuwa chini ya masharti magumu ya makubaliano ya mseto na chama kimoja cha upinzani.
ANC inajua kuwa kuunda serikali ya mseto na chama kimoja cha upinzani, kunaweza kuwalazimisha kukubali masharti ambayo yanaweza kudhoofisha ajenda zao za kisiasa na kiuchumi.
Kwa hiyo, wanatumaini GNU itatoa jukwaa pana zaidi la kushirikiana na vyama mbalimbali na kuimarisha utawala bora na utulivu wa kisiasa.
Lakini ANC inakabiliwa na changamoto nyingi. Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha kupungua kwa umaarufu wa ANC kutokana na malalamiko ya umma kuhusu rushwa, ukosefu wa ajira na hali mbaya ya uchumi.
Pia ndani ya chama kuna migawanyiko miongoni mwa viongozi, hali ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa umakini kudumisha umoja na uthabiti.
Kuunda serikali ya mseto na chama kimoja cha upinzani, kunaweza kuwa na changamoto za kisiasa na kiitikadi, na kunaweza kudhoofisha uwezo wa ANC kutekeleza ajenda zake kikamilifu.
Kwa kuchagua GNU, ANC inatarajia kupata suluhisho la muda mrefu kwa changamoto hizi, huku ikitoa nafasi kwa vyama vingine vya siasa kushiriki katika uongozi wa nchi na kusaidia kutatua matatizo ya kitaifa.
ANC itakuwa na wabunge 159 pekee katika Bunge la Kitaifa lenye viti 400, tofauti na kilivyopata wabunge 230 katika uchaguzi wa mwaka 2019.
Ramaphosa alibainisha ANC ilikuwa na tofauti za kiitikadi na kisiasa na vyama vingine lakini akasema Waafrika Kusini wanatarajia wanasiasa kuzishinda tofauti hizo na kutafuta muafaka wa kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya kila mtu.
Tofauti za kisera ni kubwa hasa kati ya vyama viwili vikubwa vilivyotajwa na Ramaphosa -DA na EFF.
Awali ANC iliwasiliana na chama cha Rais wa zamani Jacob Zuma cha Umkhonto weSizwe (MK), ambacho kilipata asilimia 14.6 ya kura na viti 58, lakini hakijatoa jibu.
Zuma, ambaye zamani alikuwa kiongozi wa ANC, amekuwa na uchungu kwa muda mrefu kuhusu jinsi alivyofukuzwa na chama chake chini ya wingu la tuhuma za ufisadi mwaka 2018.
Chama cha MK, ambacho kilianzishwa mwishoni mwa mwaka jana tu, kimekataa matokeo ya uchaguzi na kusema hakitaunga mkono serikali inayoongozwa na ANC ikiwa Ramaphosa ataendelea kushikilia usukani.
Kwa nini ANC inakwepa mseto
Ziko sababu kadhaa zinazodokeza kwa nini ANC inakwepa serikali ya mseto zikiwamo za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kwanza, serikali ya mseto inahusisha kushirikiana na baadhi vyama vingine vya siasa, jambo ambalo linaweza kumaanisha ANC itabidi ipunguze nguvu zake za kisiasa na kufanya uamuzi kwa maelewano na vyama vingine. Hii inaweza kusababisha ANC kupoteza udhibiti wa baadhi ya sera muhimu na mikakati ya kitaifa ambayo imekuwa ikitekeleza kama chama tawala.
Pili, vyama tofauti vya siasa vina itikadi na sera tofauti. ANC, kwa mfano, ina msimamo tofauti wa kisiasa na DA na EFF. Migongano hii ya kiitikadi inaweza kuleta changamoto kubwa katika kutekeleza sera na mikakati ya pamoja ndani ya serikali ya mseto.
Tatu, serikali za mseto mara nyingi zinakumbwa na changamoto za utendaji kutokana na tofauti za kimasilahi kati ya vyama vinavyoshiriki. Hii inaweza kusababisha kuchelewesha uamuzi muhimu na kuzorota kwa utendaji wa serikali, jambo ambalo linaweza kuathiri vibaya utendaji wa serikali na maendeleo ya nchi.
Nne, katika serikali ya mseto, ANC itahitaji kufanya makubaliano na vyama vingine kuhusu sera na mipango ya maendeleo. Hii inaweza kuifanya kushindwa kutekeleza ajenda zake kikamilifu kama chama tawala, kwa kuwa itapaswa kuzingatia matakwa na masharti ya vyama vingine vinavyoshiriki katika serikali.
Tano, kuunda serikali ya mseto kunaweza kuzidisha migawanyiko ndani ya ANC yenyewe, hasa ikiwa baadhi ya wanachama hawatakubaliana na masharti au mikataba iliyowekwa na vyama vingine vya upinzani. Hii inaweza kudhoofisha mshikamano na umoja wa chama, na hatimaye kuathiri umaarufu wake zaidi.
Sita, vyama vingine vya siasa vitakuwa na nafasi za madaraka katika serikali ya mseto, jambo ambalo linaweza kuongeza ushindani wa madaraka, na kuzidisha mivutano ya kisiasa ndani ya serikali. Ushindani huu unaweza kufanya kazi ya serikali kuwa ngumu zaidi na kuongeza uwezekano wa migogoro ya kisiasa.
Kwa sababu hizi, ANC inaona hatari kubwa katika kuunda serikali ya mseto na inajaribu kuepuka hilo kwa kutafuta njia mbadala kama kuunda GNU ambao wanaweza kuwa na udhibiti zaidi na kudumisha mshikamano wa kitaifa bila kuwa chini ya masharti magumu ya makubaliano ya mseto.
Vyovyote iwavyo, ANC inakabiliwa na changamoto kubwa kisiasa kuliko wakati mwingine wowote tangu mwaka 1994.