DA yakaribisha mazungumzo na ANC kuunda Serikali mpya

Rais wa Afrika Kusini ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala cha African National Congresss (ANC), Cyril Ramaphosa (kushoto) na kulia kwake ni kiongozi wa Chama cha Democratic Alliance (DA), John Steenhuisen.
Muktasari:
- Kiongozi wa DA John Steenhuisen amesema kwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa 2024 yametoka chama chake kinaweza kuanza mazungumzo ya muungano wa kuunda Serikali mpya.
Johannesburg. Kiongozi wa Chama cha Democratic Alliance (DA), John Steenhuisen amesema kwa kuwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2024 yametoka, chama chake kinaweza kuanza mazungumzo ya muungano wa kuunda Serikali mpya.
Kauli yake inakuja baada ya chama tawala cha African National Congresss (ANC) kuhitaji muungano kutokana na kukosa sifa ya kuunda Serikali, kwa kupata kura chini ya asilimia 50 katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.
Hata hivyo, matokeo ya Uchaguzi Mkuu yalitangazwa jana Jumapili na Bunge jipya linapaswa kukutana si zaidi ya siku 14, katika tarehe iliyopangwa na jaji mkuu kulingana na Katiba ya nchi hiyo wabunge watamchagua Rais wa nchi hiyo.
Hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya Africa News Steenhuisen (48), akiwa kama kiongozi mkuu wa upinzani amesema chama chake pia kitaanzisha mazungumzo na vyama mbalimbali, isipokuwa MK na EFF.
DA imeweka mstari hapo na kusema haitafanya kazi nao kutokana na tofauti za kiitikadi.
Katika taarifa yake Shirika la Habari la AFP limesema vyama kadhaa vya upinzani, hususan chama cha mrengo wa kati cha DA na chama cha Kizulu cha Inkatha Freedom Party (IFP), vimedokeza kuwa viko tayari kujadili mkataba wa kisiasa na ANC. Wakati huo kati yao, viti 159 vya ANC na 87 vya DA huku 17 za IFP
Kwingineko, AFP imesema Chama cha MK cha Jacob Zuma hakitaunga mkono Serikali inayoongozwa na ANC ikiwa Cyril Ramaphosa ataendelea kushikilia usukani.
Zaidi ya hayo, kiongozi Mzungu wa DA, Steenhuisen amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na ANC ili kuzuia kile anachokiita ANC-MK-EFF. "Muungano wa Siku ya Maangamizi" ambao amesema ungevuruga katiba na uchumi.
Hata hivyo, Al Jazeera imesema muungano unaohusisha ANC na DA unaweza kuwa thabiti zaidi ikinukuu wachambuzi waliosema pande zote mbili ni za kihafidhina zaidi kiuchumi kuliko MK Party na EFF, ambazo zinaunga mkono sera za mrengo wa kushoto.
Hayo yote yanajiri baada ya matokeo ya mwisho ya uchaguzi ambayo ANC, imepoteza idadi ya wabunge na kimeshinda viti 159 kati ya viti 400.
ANC ilikuwa na viti 230 awali kabla ya matokeo yaliyoshuhudiwa kwa mara ya kwanza katika miaka 30 ya utawala wa chama hicho kikongwe nchini humo na barani Afrika.
Nyuma ya viti 159 vya ANC ni (DA) viti 87, katika nafasi ya tatu kuna chama cha Jacob Zuma kilichoundwa hivi karibuni cha uMkonto weSizwe (MK), ambacho kimepata viti 58.
Katika kura ANC imepata milioni 6.4 sawa na asilimia 40 huku DA ikipata kura milioni 3.5 sawa na asilimia 21.8 pia M.K imepata kura milioni 2.3 sawa na asilimia 14.6 , Economic Freedom Fighters (EFF), inayoongozwa na kiongozi wa zamani wa vijana wa ANC Julius Malema ikipata kura milioni 1.5 sawa na asilimia 9.5, kwa mujibu wa AFP.
Hata hivyio Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa jana Jumapili amesema matokeo ya uchaguzi huo ni ushindi kwa demokrasia, baada ya chama chake kupoteza idadi kubwa ya kura kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo mitatu.
Ramaphosa amesema ni wakati wa wao wote kuweka Afrika Kusini mbele huku akiusifu uchaguzi huo kuwa ni ushindi kwa demokrasia ya nchi hiyo.