Raila amtuhumu Rais Ruto mauaji ya waandamanaji wa ‘Gen Z’

Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga akizungumza jambo na Rais wa nchi hiyo, William Ruto. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Machafuko yanayoendelea nchini Kenya kutokana na maandamano ya Gen Z, yamemuibua Waziri Mkuu mstaafu, Raila Odinga na kumkosoa Rais Ruto kwa namna anavyoyashughulikia.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa mgombea Urais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu 2022, Raila Odinga amemtuhumu Rais William Ruto kuhusika na mauaji ya waandamanaji wa Gen Z yaliyotokea jana Juni 25, 2024.

Aidha, Odinga kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo Jumatano Juni 26, 2024 ametaka maandamano hayo yamalizwe kwa njia ya mazungumzo na si nguvu kama inavyofanya Serikali ya Kenya.

“Leo nchi yetu inalipia gharama kubwa kwa ukaidi wa Serikali. Mambo ambayo yalipaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na unyenyekevu yameharibika na kushuhudiwa vitu ambavyo havijawahi kutokea kwa miaka 61 ya Uhuru.

“Nimesikitishwa sana na ukandamizaji mbaya dhidi ya vijana, waandamanaji wa amani wanaotumia haki yao ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza. Nimesikitishwa na mauaji, kukamatwa, kuwekwa kizuizini na ufuatiliaji unaofanywa na polisi kwa wavulana na wasichana wanaotafuta tu kusikilizwa kuhusu sera za ushuru zinazoiba maisha yao ya sasa na ya baadaye,” amesema Odinga na kupitia taarifa yake.

Waandamanaji wa Kenya, wanapinga muswada wa sheria ya fedha na hali ngumu ya maisha.

Hata hivyo, Rais Ruto jana alihutubia Taifa hilo, akisema waandamanaji wa Gen Z waliovamia jengo la Bunge walikuwa na viashiria vya kiuhalifu na hayakuwa maandamano ya amani.

“Navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi waliyoufanya leo (jana) ya kulinda amani…sio sawa wahalifu kujifanya waandamanaji wa amani, tutalimaliza jambo hilo bila kuleta madhara,” alisema Rais Ruto.

Pia, Odinga amesema Katiba ya Kenya imesiginwa, huku yeye na chama chake cha muungano wa Azimio hawawezi kuliruhusu hilo.

“Serikali imetumia nguvu zisizo za kiutu kwa watoto wa nchi yetu na inaonekana inaendelea. Hatuwezi kuruhusu hilo. Hatuwezi na hatutavumilia dakika zozote za ziada za mauaji na vurugu hizi ambazo zingeweza kuepukika na bado zinaweza kuepukika,”amesema Odinga.

Aidha, Odinga ametoa wito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuingilia kati ukiukwaji wa sheria kwa raia unaoendelea nchini humo.

Mbali na Odinga, pia aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta jana usiku alikosoa namna maandamano hayo yanavyoshughulikiwa na Serikali, huku akitaja kitendo hicho ni uvunjifu wa Katiba.

“Nasikitishwa na vifo vinavyotokana na hali ya sasa ya nchi yetu. Ni haki ya kila Mkenya kuandamana kama ilivyoamuliwa na Katiba tuliyotangaza sote mwaka wa 2010. Pia, ni wajibu wa kiongozi kuwasikiliza wanaowaongoza,” amesema Kenyatta.