Waandamanaji Kenya wataka muswada wa fedha wote uondolewe

Waandamanaji Kenya wakiwa nje ya majengo ya Bunge jijini Nairobi leo Juni 25, 202. Picha na NMG

Muktasari:

  • Wakati wabunge wakiendelea na vikao, maandamano yameibuka upya, yakikabiliana na polisi

Nairobi. Wakati Bunge la Kenya limepitisha marekebisho ya muswada wa fedha kwa mwaka 2024, maandamano yameibuka upya, waandamanaji wamevamia eneo la Bunge na kuchoma moto.

Maandamano hayo yaliyoanza wiki mbili zilizopita, yalilenga kupinga vifungu vya muswada huo ambao wabunge 195 walipiga kura kupitisha muswada huo, huku 106 wakipiga kura kukataa sheria iliyopendekezwa.

Baada ya maandamano hayo, muswada huo ulirudishwa wabunge wakapiga kura mara ya tatu.

Wakati wakiendelea na vikao, maandamano hayo yameibuka upya, yakikabiliana na polisi waliowatawanya waandamanaji wakipinga muswada wa fedha wa 2024.

Umati huo ulianza kukusanyika saa moja asubuhi karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Kenya na baadaye kutawanyika katika barabara mbalimbali.

Waandamanaji hao waliokuwa wakiimba kauli mbiu za pingamizi dhidi ya muswada wa fedha huku maduka kadhaa yakisalia kufungwa katika maeneo mbalimbali ya katikati ya mji huo.

Kulingana na michakato ya Bunge, leo hii ni hatua ya wabunge kupitia muswada kifungu kwa kifungu kinachopendekeza marekebisho.

Muswada huo ulipita awamu ya pili wiki iliyopita baada ya wabunge 204 kuunga mkono huku 115 wakiupinga.

 Baada ya hapo muswada huo utasogea awamu ya tatu na Bunge litaupigia kura ukiwa na marekebisho mapya.

Waandamanaji wanahoji kuwa mpango wa kukusanya kodi zinazopendekezwa katika muswada huo zitazidisha hali ngumu ya kiuchumi kwa Wakenya wa kawaida.

Jumatatu Juni 24, 2024 Serikali ilionya Wakenya wanaopanga kuandamana leo dhidi ya aina yoyote ya ghasia na uharibifu wa mali.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki, mbali na kukiri kila Mkenya ana haki ya kuandamana au kulaani, alisisitiza kwamba waandamanaji hawapaswi kukiuka haki na uhuru wa wengine.

Rais Ruto

Wakati maandamano yakiendelea, Rais William Ruto ameongoza ufunguzi wa kikao cha mapumziko kuhusu mageuzi ya taasisi za Umoja wa Afrika (AU) katika Hoteli ya Enashipai huko Naivasha.

Rais Ruto ambaye mwanzoni mwa mwaka huu aliteuliwa kuwa Bingwa wa Mageuzi ya Taasisi za Umoja wa Afrika, aliwahakikishia wawakilishi wa nchi wanachama wa AU kujitolea kwake kufanya mageuzi makubwa yatakayoongeza ufanisi wa umoja huo.

"Nina azma ya kufanya mageuzi makubwa ambayo yatafanya Umoja wa Afrika, vyombo vyake na mashirika maalumu kuwa na ufanisi zaidi. Hasa, kuna maeneo ya kazi yanayokaribiana yanayohitaji suluhisho la haraka ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa AU," amesema Rais Ruto.

Kiongozi huyo alichukua uongozi wa mabadiliko ya kimfumo ya Umoja wa Mataifa uliokuwa ukishikiliwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Jukumu hilo linahusisha kurekebisha muundo, utendaji kazi na mwelekeo wa Tume ya Umoja wa Afrika, vyombo vya AU na mashirika maalumu ili kuyafanya kuwa na ufanisi zaidi katika kusimamia mambo ya nchi wanachama.

"Tuna nafasi ya kihistoria ya kurekebisha Umoja wa Afrika na kuufanya uwe na lengo la wazi katika mwangaza wa malengo yetu ya pamoja ya maendeleo. Tunapaswa kutekeleza mageuzi haya kwa azimio na haraka inavyostahili kwa ukubwa wa changamoto zetu, uwezo wetu, na matarajio yetu," amesema Rais Ruto.

"Wafrika ni wachapakazi, wenye elimu, wenye ujuzi na vijana na wako tayari kuchangia katika kuendeleza bara letu. Hatupaswi kuwaangusha, na hatupaswi kuwaacha wakisubiri," ameongeza.

Akitambua mageuzi yaliyofanywa na mtangulizi wake, Paul Kagame, Rais Ruto ameahidi kuifanya Tume ya Umoja wa Afrika iwe na lengo la wazi na kuipa uwezo wa kushirikiana na dunia kwa niaba ya Afrika.

"Kutokana na mageuzi yaliyofanywa hadi sasa, maamuzi katika mkutano wa AU yameboreshwa kufikia uwazi na uchumi mkubwa. Vilevile, muundo na mamlaka ya ngazi za juu za tume yamepangwa upya na kuimarishwa kwa taratibu za uteuzi zilizorahisishwa.”

Rais Ruto pia ameahidi kuanzisha utaratibu madhubuti na endelevu wa ufadhili kwa bajeti ya kawaida na ya programu za AU.


Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika ya habari