Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Papa Leo XIV afichua siri kuchagua jina hilo, aitaja Akili Mnemba

Muktasari:

  • Papa Leo wa XIV (Robert Francis Prevost), alizaliwa Septemba 14, 1955 mjini Chicago, Illinois, Marekani. Ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu. Baba yake akiwa Louis Marius Prevost, mwenye asili ya Kifaransa na Kiitaliano, na mama yake Mildred Martínez, mwenye asili ya Kihispania. Robert ana kaka zake wawili wakubwa, Louis Martín na John Joseph.

Dar es Salaam. Papa Leo wa XIV amesema miongoni mwa matishio ya maisha ya binadamu katika karne ya sasa ni ujio wa akili mnemba (AI) huku akiahidi kuendeleza vipaumbele vya mtangulizi wake, Papa Francis.

Leo XIV ambaye alichaguliwa Mei 8, ametoa kauli hiyo jana Jumamosi alipotembelea Kanisa la Mtakatifu Maria Maggiore, lililoko kusini mwa Roma ambalo lina umuhimu mkubwa kwa Shirika lililomlea la Waagostino na pia kwa mtangulizi wake wa jina, Papa Leo XIII aliyeongoza kanisa hilo kati ya 1878-1903.

“Katika siku zetu hizi, kanisa linatoa kwa wote hazina ya mafundisho yake ya kijamii kama mwitikio kwa mapinduzi mengine ya viwanda na kwa maendeleo ya akili bandia yanayoleta changamoto mpya kwa ulinzi wa utu wa binadamu, haki na kazi,” amesema Leo XIV.

Akimkumbuka mtangulizi wake, Leo XIV amesema kuelekea mwisho wa upapa wake, Papa Francis alizidi kutoa sauti juu ya vitisho vya AI kwa ubinadamu na alitaka kuwe na mkataba wa kimataifa kuisimamia.

Katika hotuba iliyotolewa kwa Kiitaliano kwenye ukumbi wa Sinodi wa Vatican ambalo siyo Jumba la Kitume, Leo XIV amemtaja Francis mara kwa mara huku akieleza kuhuzunishwa na kifo chake.

Alilitaja tangazo la misheni la Francis la 2013, “Furaha ya Injili” kama mwongozo wa utume wake.

Alinukuu msisitizo wa Francis juu ya asili ya Kimishionari ya kanisa na hitaji la kufanya uongozi wake kuwa wa ushirikiano zaidi.

Alisisitiza hitaji la kuwasikiliza waumini wa kanisa hilo hasa katika maumbo yake halisi na jumuishi, hasa ibada za watu wa kawaida, kuonyesha upendo kwa walio duni na waliokataliwa na kufanya mazungumzo yenye tija kwa dunia ya sasa.

Akiwa njiani kurejea katika makazi yake, Papa Leo XIV, alisimama kusali kwenye kaburi la Papa Francis katika Kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu mjini Roma.


Asili ya jina Leo XIV

Katika hotuba yake rasmi ya kwanza aliyoisoma leo Jumapili Mei 11, 2025, mbele ya Baraza la Makardinali tangu achaguliwe. Papa Leo XIV amefichua chanzo na siri ya kuchagua jina hilo.

Kwa maneno yake mwenyewe, Papa Leo XIV amesema alichagua jina hilo kwa sababu linaakisi kujitolea kwake kwa Kanisa na kuheshimu utu wa binadamu na haki ya kijamii.

“Papa Leo wa XIII (mtangulizi wa jina lake), kupitia waraka wake mashuhuri “Rerum Novarum”, alizungumzia masuala ya kijamii katika muktadha wa mapinduzi ya kwanza ya viwanda.”

“Leo kanisa linatoa hazina yake ya mafundisho ya kijamii kama jibu kwa mapinduzi mengine ya viwanda na maendeleo ya akili bandia (AI),” amesema Papa Leo XIV.

Amesema kupitia jina hilo ataendeleza utamaduni, kutazama mbele ili kukabiliana na changamoto za dunia inayobadilika kwa kasi na wito wa kuwalinda walio hatarini zaidi.

Viongozi, waumini wamzungumzia

Padri Bartholomew Mrosso, wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph la Jimbo Kuu la Dar es Salaam amemuelezea Papa Leo XIV  kuwa karibu na waumini wake (Kondoo) pia ni mchungaji anayesimamia mafundisho ya kanisa.

Amesema viongozi wa kanisa sio watu wakubwa wala machifu bali ni watu ambao wanatakiwa kuwa karibu na kondoo wao, kusikia sauti na kuingia katika fikra zao ili kupata mateso yao na kuwa pamoja nao.

Ameyasema hayo leo Jumapili ya nne ya Pasaka katika misa ya tatu iliyofanyika kanisani hapo wakati wa mahubiri ya injili yaliyoelezea kuhusu mchungaji mwema.

"Jumapili ya leo tunamshukuru Mungu kanisa letu Katoliki limepata mchungaji mwema Papa Leo XIV. Ndugu zangu mnaona kanisa limepata kiongozi wa namna yake ni ambaye yupo karibu na kondoo zake,” amesema Padri Mrosso.

Amesema Papa Leo amekuwa na sifa ya Mtakatifu Benedicto ambaye alikuwa ni mchungaji na msimamizi wa mafundisho ya dini aliyehitaji watu kumfuata Yesu na mafundisho yake, huku papa Fransisko alikuwa na sifa ya uchungaji.

Padri Mrosso amesema Papa Leo alipokuwa askofu akmivaa buti za mvua na kwenda kwenye eneo chafu chafu na hilo ilikuwa ni kuendeleza mtazamo wa Papa Francis kwa kuwa karibu na watu.

"Papa Leo ana sifa au tabia za Mtakatifu Benedicto alikuwa anasimamia mafundisho ya dini, wakati Papa Francis alikuwa ni mchungaji na huyu analeta mafundisho ya kidini basi na sisi tuwe waaminifu kumfuata yeye," amesema.

Pia, ametoa wito kwa waumini wa kanisa hilo kuwa Jumapili hii ya mchungaji mwema ikawabadilishe na kuwa wachungaji wema katika familia, taasisi mbalimbali wanazofanya kazi katika Taifa la Tanzania na ulimwengu mzima.

Hata hivyo, Padri mlezi wa watawa katika Kanisa Kuu Parokia Ngokolo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga, Emmanuel Kahabi amesema anaamini Papa Leo alichagua hilo jina ili kuongoza waumini kwa masilahi ya Jamii.

“Amevutiwa na kuongoza waumini kwa masilahi ya jamii, akaamua kuendeleza kile mtangulizi wake alichokuwa akikifanya ambaye ni Papa Leo wa XIII, ili kuishi katika njia hiyohiyo akaamua kuchagua jina la Leo ambapo yeye ni Papa wa XIV kutumia jina hilo” amesema Kahabi.

Naye, Selina Andrew amesema ni furaha kwa kila muumini kuona wamepata kiongozi ambaye wanamchukulia kama Rais wa makanisa ya Katoliki na anayesimamia mwongozo na katiba za kanisa hilo.

"Kanisa ni kama Serikali ambayo inatakiwa kuwa na uongozi ili kujiongoza vyema ndiyo maana waumini walikuwa wanasubiri kwa hamu kuona moshi mweupe, ndiyo maana ulipotoka mweusi sura za waliokuwa wanafuatilia huko Vatican zilikuwa na huzuni," amesema.

Kwa upande wake, Jacob Lyimo, amesema Mungu ndiye anayeteua watu wake hakuna anayechaguliwa kwa bahati mbaya na ikitokea hivyo, kiongozi huyo hawezi kufanikiwa katika kuongoza watu wake.

"Leo tumesikiliza somo la mchungaji mwema na tunaamini kabisa mafundisho na maelezo mafupi tuliopewa na Padri yanastahili kwa Papa wetu mpya Leo XIV kuchaguliwa kwa ajili ya kuliongoza kanisa Katoliki duniani kote,"amesema Lyimo.

Amesema kilichobaki ni wao kufuata mafundisho yanayotolewa na viongozi wao ili kufanya matendo yanayopendeza machoni pa Mungu.

Papa Leo ni nani?

Papa Leo wa XIV (Robert Francis Prevost), alizaliwa Septemba 14, 1955 mjini Chicago, Illinois, Marekani. Ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu.

Baba yake anaitwa Louis Marius Prevost, mwenye asili ya Kifaransa na Kiitaliano, na mama yake anaitwa Mildred Martínez, mwenye asili ya Kihispania. Robert ana kaka zake wawili wakubwa, Louis Martín na John Joseph.