Ngoma bado mbichi Jubilee ya Kenyatta

Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiwa kwenye Mkutano Mkuu wa wa Chama cha Jubilee leo Jumatatu Mei 22, 2023.

Nairobi. Mgogoro wa uongozi uliokikumba Chama cha Jubilee washika kasi licha ya Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta kuandaa mkutano maalumu wa wajumbe wa kitaifa (NDC) uliowatimua wanachama ‘waasi’ wanaodaiwa kuungwa mkono na serikali.

Wanachama hao wanaoongozwa na Mbunge Sabina Chege na mwenzake wa Bunge la Afrika Mashariki Kanini Kega, bado wamesistiza kuwa ndio wanatambuliwa rasmi kama viongozi wa chama hicho licha ya kutimuliwa na kundi lnaoongozwa na Kenyatta.

Kwa mujibu wa Sabina na Kega, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu, ameishainidhinisha uamuzi wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama lililoketi Februari 10, 2023 na ule wa Mei 10 mwaka huu ambao uliwatimua Kenyatta, Naibu Mwenyekiti David Murathe, Katibu Mkuu Jeremiah Kioni, na Kagwe Gichohi.

“Kufuatia ukaguzi wa stakabadhi zilizowasilishwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya kisiasa na katiba ya chama, ofisi hii imeridhika kwamba, chama kilifuata mchakato unaohitajika. Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya kisiasa, ofisi hii imebadilisha rekodi zake na sajili ya wanachama wa chama,” Nderitu amesema katika barua aliyomwandikia Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, Joshua Kutuny mnamo Mei 19, 2023.

Bw Kutuny ni mmoja wa waliotimuliwa na NDC iliyoitishwa na kambi ya Uhuru. Ni katika muktadha wa barua hiyo toka Msajili wa vyama, Kega alipuuza kongamano la Jumatatu lililomtimua pamoja na washirika wake akilitaja kama mkutano wa kawaida wa kisiasa akisema haukuwa halali.

Azungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kutimuliwa Jubilee, Kega alipuuza NDC aliyoitisha Kenyatta akisisitiza Rais huyo mstaafu hana mamlaka ya kufanya maamuzi ya chama, na kwamba watamchukulia Uhuru hatua za kinidhamu kwa kufuata taratibu za utatuzi wa migogor ndani ya chama chao.

Hata hivyo, inasemekana kwamba kambi ya Kenyatta, kupitia kwa Katibu Mkuu Kioni, ulikuwa umepata agizo la Mahakama la kusimamisha kwa muda uamuzi wa kuwatimua chamani Sabina na Kega.

Kwa upande mwingine, agizo lililotolewa na Mahakama ya Kutatua mizozo ya kisiasa Jumatatu Mei 22 2023 limezuia kambi ya Kega na msajili wa vyama vya kisiasa kutekeleza uamuzi wa jopo la nidhamu la chama cha Jubilee wa kutimua Kioni na wenzake.

“Agizo la muda linatolewa kusimamisha uamuzi wa jopo la nidhamu la mshtakiwa wa kwanza (chama cha Jubilee) wa kumtumia mlalamishi.”

“Agizo la muda linatolewa kuzuia mshtakiwa wa pili (msajili wa vyama vya kisiasa) kutekeleza mawasiliano ya mshtakiwa wa kwanza (chama cha Jubilee) yanayodai kutimua mlalamishi kutoka uanachama,” linasema agizo lililotolewa na mwenyekiti wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa, Desma Nungo.

Haya yanajiri huku Kenyatta akisisitiza kuwa hataachilia uongozi wa chama hicho, huku muungano wa Azimio ukitishia kujiondoa katika mazungumzo ya kamati teule ya Bunge yaliyoufanya kusitisha maandamano iwapo serikali itaendelea kuvuruga Jubilee.

“Kuna wakati ambao nilifikiria nitastaafu kutoka siasa. Nilifikiria ningekuja kwa NDC kukabidhi uongozi hadi pale baadhi ya watu walipoanza vitisho. Ninataka kuwaambia kwamba, watishe mtu mwingine lakini sio mimi,” alisema Bw Kenyatta.

Jana Jumanne, kambi ya Kenyatta ilitarajiwa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa, uamuzi wa NDC iliyoketi Jumatatu na kufanya maamuzi ya kuwatimua chamani Sabina, Kega na washirika wao.

Akizungumza akiwa Siaya jana Jumanne, kiongozi wa Azimio Raila Odinga alishambulia serikali kwa kushawishi Msajili wa Vyama vya Kisiasa kutoidhinisha kutimuliwa kwa waasi wa chama cha Jubilee na mkutano mkuu wa wajumbee (NDC) uliofanyika Jumatatu.