Kenyatta atoa msimamo Jubilee

Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiwa kwenye Mkutano Mkuu wa wa Chama cha Jubilee leo Jumatatu Mei 22, 2023.

Muktasari:

  • Baada ya shinikizo la kuachia ngazi ndani ya Jubilee, Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameeleza msimamo wake.

Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema uamuzi wa kuachana na uongozi wa Chama cha Jubilee, utatokana na maamuzi ya waliomchagua.

 Kenyatta ametoa kauli hiyo, wiki tatu baada ya kuwepo mashinikizo ya kukatiza uongozi wake ndani ya chama hicho, alichohudumu kwa miaka kadhaa kama kiongozi.

Hata hivyo, Katiba ya Kenya Ibara ya 6 (1) inamtaka mkuu wa nchi hiyo anayemaliza muda wake, kutoshika nafasi yoyote katika chama chochote cha siasa, miezi sita baada ya kustaafu urais.

Akihutubia Mkutano Mkuu wa Jubilee nchini Kenya leo, Mei 22, 2023, Kenyatta amesema ingawa alikuwa na fikra za kuachana na shughuli za kisiasa, wengine walimtaka kufanya hivyo kwa vitisho.

“Wengine wameamua kazi itakuwa ya vitisho na kulazimisha, siku ya leo  nimewaambia tafuteni mwingine sio Uhuru wa Kenyatta,” amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wanachama hao.

Hoja yake hiyo inatokana na kile alichoeleza kuwa, wakati anapewa uongozi wa chama na nchi, alikabidhiwa mwongozo wa utekelezaji na amefanya kwa kadri ya uwezo wake.

“Tukamaliza kwa amani na tukapatiana uongozi kwa amani wajameni, hadharani mchana, hata wakati wananitukana nilikaa kimya nikasema acha watende yale wanaona haki yao kuyafanya.

“Nikakaa kimya na yale yametokeza tu matusi, kuiba mbuzi, kuchoma mashamba, yote wakifikiria wanatisha, haya nawaambia waendelee lakini chama sio cha Uhuru kina wenyewe na wenyewe walinipatia niichunge.

“Na mpaka wataniambia wapo tayari wamechagua mwingine, nitashikiria mpaka wataniambia sasa muachie mwingine,” amesema.

Hata hivyo, mkutano huo umeamua hatma ya uongozi wa aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Jubilee, Kanini Bega na Sabina Chege, kwa kile kilichoelezwa kuwa wanashirikiana na upande wa Rais wa Kenya, William Ruto.