Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marekani yaishambulia Iran, yenyewe yaapa kulipa kisasi

Muktasari:

Kwa mujibu wa kundi la Human Rights Activists lenye makao yake Washington, mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yamesababisha jumla ya vifo takriban 865 na kujeruhi wengine 3,396 Iran na Israel. 

Lilikuwa suala la muda tu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Marekani kutangaza hadharani kuwa imefanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nyuklia nchini Iran.

Marekani sasa imeingia rasmi katika mgogoro  kati ya Israel dhidi ya Iran. Hatua hiyo imetangazwa usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 22, 2025, na Rais wa taifa hilo, Donald Trump.

Katika hotuba yake kwa umma, Trump amesema ndege za Jeshi la Marekani zimelenga na kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran vilivyoko maeneo ya Fordow, Natanz na Isfahan.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Vituo muhimu vya nyuklia vya Iran vimeharibiwa kabisa na kikamilifu katika mashambulizi niliyoamuru yafanyike,” amesema Trump alipozungumza na vyombo vya habari nchini humo.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ameionya Marekani kuwa mashambulizi yake dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran yatakuwa na athari za kudumu na kwamba Iran haitakaa kimya badala yake italipiza kisasi.



Waziri huyo, Araghchi ameandika kwenye akaunti yake ya Mtandao wa X, akiwa ofisa wa kwanza wa ngazi ya juu Iran kutoa kauli kuhusu mashambulizi ya Marekani dhidi ya eneo la Isfahan, Fordo, na Natanz.
“Matukio ya asubuhi hii ni ya kuchukiza na yatakuwa na athari za kudumu,” ameandika Araghchi.

Ameongeza kuwa: “Kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa na masharti yake yanayoruhusu kujilinda kwa njia halali, Iran haina chaguo zaidi ya kufuata kanuni na sheria za umoja huo za kujilinda ili kulinda uhuru wake, maslahi na watu wake.”

Rais Trump amechukua hatua hiyo bila idhini ya Bunge huku akionya kwamba kutakuwa na mashambulizi zaidi iwapo Iran itajibu kwa kushambulia vikosi vya Marekani.

“Kutakuwa na amani au janga kwa Iran,” amesema Rais huyo.

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limethibitisha kuwa mashambulizi yalilenga vituo vyao vya Fordo, Isfahan, na Natanz, lakini lilikataa kuthibitisha iwapo kuna athari kwa raia ama shughuli zilizoathiriwa na mashambulizi hayo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Iran imesema hakuna dalili za mionzi kuvuja katika maeneo hayo na hakuna hatari kwa wakazi wa karibu na maeneo yaliyoshambuliwa na ndege hizo za Marekani.
Iran imesisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani tu huku mashirika ya ujasusi ya Marekani yakikadiria kuwa Tehran haijaanza kutengeneza bomu. 

Hata hivyo, Trump na viongozi wa Israeli wameeleza hofu kuwa Iran inaweza kutengeneza silaha ya nyuklia haraka na hivyo kuwa tishio la dharura kwa mataifa ya Mashariki na Marekani.

Uamuzi wa Marekani kujiingiza moja kwa moja katika vita hivyo unakuja baada ya wiki moja ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yaliyolenga kuharibu mifumo ya ulinzi wa anga na makombora ya Iran, pamoja na kuharibu mitambo yao ya urutubishaji wa uranium. 

“Tumekamilisha kwa mafanikio mashambulizi yetu dhidi ya vituo vitatu vya nyuklia vya Iran, ikiwemo Fordow, Natanz, na Esfahan,” Trump alianza kwa kuandika hivyo kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Ndege zetu sasa zipo nje ya anga ya Iran. Tulirusha mabomu yote kwenye kituo kikuu cha Fordow. Ndege zote zinarudi salama nyumbani.”

Katika ujumbe mwingine, Trump aliandika: “Huu ni wakati wa kihistoria kwa Marekani, israel na dunia. Iran sasa inapaswa kukubali kumaliza vita hivi, asanteni!,”

Akizungumzia uamuzi wa Marekani kuingia moja kwa moja kwenye mgogoro huo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amempongeza Rais Trump kupitia ujumbe wa video kuwa:

“Uamuzi wako jasiri wa kulenga vituo vya nyuklia vya Iran, kwa nguvu ya haki ya Marekani, utabadilisha historia. Marekani imefanya kile ambacho hakuna taifa lingine lingeweza kufanya,” amesema Netanyahu.

Baada ya mashambulizi hayo ya Marekani, Israel imetangaza kufunga anga lake kwa safari zote za kuingia na kutoka ndani ya nchi hiyo kwa kile ilichodai ni sababu za kiusalama.

Hii ina maana gani?

Akizungumzia mzozo huo ambao umeingia siku ya tisa leo, Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayattolah Khamenei alitangaza Alhamisi iliyopita kuwa jaribio lolote la Marekani kuishambulia Iran, litaufanya mzozo huo kuwa ‘vita kamili’.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameonyesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa hatari ya vita kati ya mataifa hayo jambo linaloweza kusababisha athari mbaya kwa raia, kanda nzima na dunia.

Mabomu yaliyotumika

Israel awali ilisema mashambulizi yake tayari yameharibu ulinzi wa anga wa Iran na hivyo kurahisisha uharibifu wa vituo vingi vya nyuklia.

Maofisa wa Marekani na Israeli wamesema kuwa ndege za kivita za Marekani za siri (stealth bombers) na bomu la uzito wa kilo 13,500 (pauni 30,000) ndizo pekee zinazoweza kulenga na kuharibu maeneo ya nyuklia yaliyofichwa chini ya ardhi.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa Marekani alisema kuwa mashambulizi yalitumia mabomu maalum yanayopenya ardhi (bunker-buster bombs) dhidi ya kituo cha Fordo kilichojengwa ndani ya mlima.

Aidha, ofisa mwingine wa jeshi la Marekani ambaye hakutaka majina yake yatajwe amelieleza Shirika la Habari la Associated Press kuwa manowari za Marekani nazo zinatajwa kuwa zilirusha makombora 30 ya Tomahawk.

Lakini ili kuharibu kituo cha Fordo kilicho ndani ya mlima, Israel iliomba msaada wa bomu maalumu la Marekani la GBU-57 Massive Ordnance Penetrator, ambalo hutegemea uzito na nguvu ya msukumo kulenga maeneo ya ndani kabisa kabla ya kulipuka. 

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Bomu hilo linatumika tu na ndege ya kivita ya siri ya Marekani, B-2, ambayo haipo kwenye mataifa mengine.

Hii ilikuwa mara ya kwanza silaha hiyo kutumika vitani.

Bomu hilo lina kichwa cha kawaida cha mlipuko na linaaminika kuwa na uwezo wa kupenya hadi futi 200 (mita 61) chini ya ardhi kabla ya kulipuka. Mabomu yanaweza kurushwa mfululizo, yakizama zaidi kwa kila mlipuko.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limethibitisha kuwa Iran inazalisha uranium yenye kiwango cha juu cha urutubishaji katika Fordo, na hivyo kutumia GBU-57 A/B kwenye kituo hicho kunaweza kusababisha kuvuja kwa nyenzo za nyuklia.

Mashambulizi ya awali ya Israel kwenye kituo kingine cha nyuklia cha Natanz yalileta uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo tu, si maeneo ya jirani, kwa mujibu wa IAEA.

Kwa mujibu wa kundi la Human Rights Activists lenye makao yake Washington, Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yamesababisha vifo vya watu takriban 865 na kujeruhi wengine 3,396 kwa pande zote (Iran na Israel). 

Kati ya waliouawa, waliwatambua raia 363 na wanajeshi 215.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.