Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Israel yaibua hofu mwafaka wa amani Mashariki ya Kati

Muktasari:

  • Kuendelea kwa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon licha ya makubaliano ya awali kati ya Marekani na Iran ya kusitisha vita, kumeibua hofu ya kuvurugika kwa mchakato mpya wa amani huku G7 na Umoja wa Mataifa wakitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.

Dar es Salaam. Makubaliano mapya kati ya Marekani na Iran yaliyolenga kusitisha vita, kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz na kurejesha mazungumzo ya kisiasa, yanakabiliwa na sintofahamu mpya.

Matumaini hayo yaliyoibuka baada ya Marekani na Iran kutangaza kufikia mwafaka wa kusitisha mapigano yanaingia sintofahamu baada ya Israel kuendelea na mashambulizi yake nchini Lebanon, hali inayotajwa kuwa inaweza kuharibu juhudi za kuhitimisha mzozo huo.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya kimataifa, Marekani na Iran tayari zimesaini kwa njia ya kielektroniki hati ya makubaliano ya awali, huku sherehe rasmi ya kutiwa saini ikitarajiwa kufanyika nchini Uswisi.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kufungua awamu mpya ya mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi na hatua za kujenga amani ya kudumu katika eneo hilo.

Hata hivyo, wakati dunia ikisubiri kutiwa saini rasmi kwa makubaliano hayo, mashambulizi mapya ya anga yameripotiwa katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Lebanon, yakiwamo Nabatieh, Kfar Tebnit na Ansariyeh.

Mashambulizi hayo yamezidisha wasiwasi kwamba vita vinaweza kuendelea licha ya juhudi za kidiplomasia zinazofanyika.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameikosoa Israel kwa kuendelea kwa mapigano hayo, akisema mzozo unaoendelea nchini Lebanon unatatiza juhudi zake za kumaliza vita na Iran.

"Mapigano yanayoendelea Lebanon yanachanganya juhudi zangu za kumaliza vita na Iran," amesema Trump, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na CBS News.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema suala la Lebanon ni sehemu muhimu ya makubaliano hayo na kwamba amani ya kudumu haiwezi kupatikana ikiwa mashambulizi yataendelea.

"Mashambulizi yoyote mapya ya Israel dhidi ya Lebanon au kuendelea kwa uwepo wa majeshi ya Israel nchini humo vitachukuliwa kuwa ukiukaji wa makubaliano kati ya Marekani na Iran," amesema Araghchi wakati akizungumza na wanadiplomasia wa kigeni kupitia televisheni ya taifa ya Iran.

Iran imeendelea kusisitiza kuwa makubaliano hayo yanapaswa kuleta kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote ya mzozo, ikiwamo Lebanon.

 Hata hivyo, viongozi wa Israel wameweka wazi kuwa hawana mpango wa kuondoa majeshi yao nchini Lebanon, Syria na Ukanda wa Gaza.

"Makubaliano ya Trump hayatufungi," amesema Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, akitetea uamuzi wa nchi yake kuendelea kuwepo kijeshi kusini mwa Lebanon.


Wito wa UN na G7

Umoja wa Mataifa nao umeonyesha wasiwasi wake kuhusu hali hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amekaribisha makubaliano ya Marekani na Iran na kuyataja ni hatua muhimu ya kuelekea utulivu wa Mashariki ya Kati.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Guterres amesisitiza umuhimu wa kufunguliwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuendelea kwa juhudi za kusitisha mapigano ili kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya kibinadamu katika eneo hilo.

Nchi za G7 pia zimeunga mkono mchakato huo wa amani na kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kuendelea kwa mazungumzo ya kisiasa.

Kundi hilo limesema kuendelea kwa mashambulizi katika Mashariki ya Kati kunaweza kuhatarisha usalama wa kimataifa, usafirishaji wa nishati na uchumi wa dunia.

Hali ya sasa inaonyesha kuwa, wakati Marekani na Iran zikijaribu kufungua ukurasa mpya wa diplomasia, mustakabali wa amani hiyo unaning'inia kwenye uwezo wa pande zinazohusika kusitisha hatua za kijeshi.

 Kuendelea kwa mashambulizi nchini Lebanon kumeifanya Israel kutajwa katika mijadala ya kimataifa kama upande unaoweza kuhatarisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Hata hivyo, Israel imeeleza kuwa  operesheni hizo zinaongozwa na mahitaji ya usalama wa taifa lao.