Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uamuzi wa Latra waibua mjadala usafiri wa Mbagala

Muktasari:

  • Uamuzi wa Latra kuzuia daladala kushusha na kupakia abiria katika njia ya mwendokasi umeibua hofu kwa wakazi wa Mbagala wanaodai utachochea matumizi ya bodaboda na bajaji, huku wadau wakilalamikia kukosekana kwa ushirikishwaji.



Dar es Salaam. Hofu ya kuongezeka kwa gharama za usafiri na matumizi ya bodaboda na bajaji imeibuka miongoni mwa wakazi wa Mbagala kutokana na uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) wa kuzuia daladala kupakia na kushusha abiria katika Barabara ya Kilwa.

Wadau wamelalamikia kutoshirikishwa kabla ya utekelezaji wa mabadiliko hayo yanayoanza Julai mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa agizo la Latra la jana, Jumatatu, Juni 15, 2026, daladala za Mbagala zitahamia katika Kituo Kikuu cha Mwendokasi na hazitaruhusiwa kupakia wala kushusha abiria katika njia ya mwendokasi.

Uamuzi huo wa Latra unakuja miezi mitatu tangu mtoa huduma wa mabasi hayo, Kampuni ya Mofat, ilalamikie kukosa faida ya uwekezaji wake, ikisisitiza kuwa uwepo wa daladala unafanya mabasi yake kutoa huduma chini ya uwezo wake.

Mofat walisema kati ya mabasi 200 yaliyopo, mabasi 50 pekee ndiyo yanayotumika, jambo linalowafanya kujiendesha kwa hasara.

Leo Jumanne, Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali, wakiwemo wananchi. Mkazi wa Mtongani, Kelvin Patrick, amesema uamuzi huo unaweza kuibua biashara kubwa zaidi ya bodaboda na bajaji kutokana na wananchi kulazimika kutafuta usafiri wa kuunganisha safari zao.

“Wakitaka kujua kuwa hilo ni tatizo, waangalie hali ilivyo sasa. Kuna mwendokasi, lakini bado daladala, bajaji na bodaboda zinafanya kazi kwa sababu zinahitajika. Ukiondoa daladala katika maeneo hayo, watu wengi wataanza kutegemea zaidi bajaji na bodaboda,” amesema Patrick.

Amesema mamlaka zinapaswa kuangalia hali halisi ya wakazi wa Mbagala badala ya kuzingatia mfumo mmoja wa usafiri pekee.

“Isiangalie kumsaidia mwekezaji pekee, iangalie namna mwananchi wa kawaida atakavyofika kazini, sokoni au kwenye shughuli zake bila kuongezewa gharama,” amesema.

Mkazi wa Kipati, Asha Mchonjo, amesema wananchi wanaofanya safari fupi ndiyo watakaobeba mzigo mkubwa wa mabadiliko hayo.

“Kwa sasa mtu anaweza kushuka karibu na eneo analokwenda au kuzungumza na kondakta kwa safari fupi na kulipa kidogo, lakini mfumo mpya unaweza kumlazimisha kutumia usafiri mwingine na kuongeza gharama ambazo hakuzipanga,” amesema Asha.

Mbali na wananchi, Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam (UWADAR) umeeleza kutoridhishwa na namna uamuzi huo ulivyofikiwa.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa UWADAR, Jafari Kismat, amesema hajaridhishwa na uamuzi unaofanywa na Serikali, akidai kuwa haushirikishi wadau muhimu kabla ya kutekelezwa.

Amesema wadau wa usafirishaji walipokea taarifa za uamuzi huo baada ya kumepitishwa bila kupewa nafasi ya kutoa maoni yao.

“Tumekuwa tukisikia taarifa baada ya uamuzi kufanyika. Sisi ni wadau muhimu katika sekta hii, lakini hatukushirikishwa. Kama kungekuwa na vikao vya kutusikiliza, huenda tungetoa mawazo ambayo yangesaidia kuboresha utekelezaji wake,” amesema Kismat.

Amesema pamoja na kutoridhishwa kwao, kwa sasa wanaendelea kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa uamuzi huo, huku wakisubiri kuona matokeo yake.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, viongozi wa UWADAR wanatarajia kukutana na kufanya mashauriano ya ndani ili kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa baada ya kutathmini athari za uamuzi huo kwa wanachama wao.

Aidha, amewasihi wananchi kuwa watulivu wakati wakisubiri mwelekeo wa suala hilo, akisisitiza kuwa ni muhimu kuheshimu uamuzi wa Serikali huku wakitafuta njia za kuwasilisha maoni yao kupitia taratibu zilizopo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC), Daudi Daudi, amesema changamoto itajitokeza iwapo wananchi hawatapewa elimu ya kutosha kuhusu sababu za mabadiliko hayo na namna yatakavyotekelezwa.

Amesema mara nyingi taasisi huandaa mipango bila kuwashirikisha wadau mbalimbali mapema, jambo linaloweza kusababisha sintofahamu na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma.

“Wangewashirikisha wananchi zaidi na kupata maoni yao mapema, huenda wangepata mawazo mengine mazuri zaidi. Sasa wanahitaji kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu ili watu waelewe dhana nzima ya mabadiliko hayo,” amesema Daudi.

Amesema mafanikio ya mpango huo yatategemea zaidi ufanisi wa utekelezaji wake kuliko sera yenyewe.

Daudi amesema ikiwa daladala zitawafikisha abiria kwa wakati kwenye vituo vya BRT na mabasi ya mwendokasi yakapatikana kwa uhakika bila ucheleweshaji, wananchi wataona faida ya mfumo huo na kuupokea vizuri.

“Uzuri wa mpango huu utapimwa na ufanisi wake. Watu wakifika kwenye vituo na kupata mabasi ya mwendokasi kwa haraka na kwa uhakika, hakutakuwa na sababu kubwa ya kulalamika,” amesema.

Pia, amesema wananchi hawataki kuona mwendokasi ukiwa na abiria wengi pekee, bali wanachotaka ni huduma bora, ya uhakika, inayodumu na yenye gharama nafuu kwa wananchi.

Amesema iwapo Latra na wadau wengine watasimamia utekelezaji wa mpango huo kwa umakini, mfumo huo unaweza kuwa hatua muhimu katika kuboresha usafiri wa umma na kuendana na maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam.