Prime
Vurugu zatokea msibani mabomu yapigwa, jeneza juu ya gari la DC
Muktasari:
- Vurugu hizo zimetokana na shinikizo la vijana kutaka wenzao 10 wanaoshikiliwa na Polisi waachiwe.
Dar es Salaam. Vurugu zimeibuka katika mazishi ya kijana aliyepoteza maisha akidaiwa kugongwa na gari la polisi wakati wanamkimbiza, wenzake wakishinikiza pikipiki yake iliyochomwa moto inunuliwe mpya.
Jambo lingine lililozua vurugu msibani hapo Kijiji cha Ngirinyi, kata ya Nasai, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro kwa mujibu wa mashuhuda, ni kitendo cha vijana 10 kushikiliwa na Polisi walipokwenda kuchukua mwili katika Hospitali ya KCMC kwa madai wanataka kufanya maandamano.
Vurugu hizo zilizotokea leo Juni 16,2026 zimekwenda mbali zaidi, hadi vijana kuamua kuuweka mwili wa marehemu juu ya gari la Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, wakishinikiza wenzao waachiwe na pikipiki iliyochomwa inunuliwe mpya na kupelekwa msibani hapo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka ambaye alikuwa eneo la tukio alijitahidi kutuliza ghasia hizo ambapo hata hivyo vijana hao waligoma kushusha jeneza lenye mwili wa kijana huyo wakishinikiza wenzao waachiwe na kufika eneo la tukio.
Alipotafutwa kuzungumza hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amekiri kutokea kwa vurugu hizo, akisema tayari kuna askari katika eneo la tukio kushughulikia hilo.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema vurugu zilianza kwa vijana kuzuia mwili wa mwenzao usizikwe.
Uamuzi huo wa vijana, amesema umetokana na kile walichokuwa wanadai mwenzao hawezi kuzikwa hadi vijana 10 walioshikiliwa na polisi waachiwe.
Amesema mapema walipokwenda kuchukua mwili katika Hospitali ya KCMC, baadhi ya vijana walikamatwa ikidaiwa kuwa wanataka kufanya maandamano.
“Hao vijana waliokamatwa ni kwa sababu ilidaiwa wanataka kuandamana. Sasa huku msibani wengine wameamua kuzuia mwili usizikwe hadi wenzao waachiwe,” amesema.
Mbali na kufungwa barabara, amesema kingine vijana hao wameuchukua mwili wa marehemu na kuuweka kwenye gari la Mkuu wa Wilaya kushinikiza madai yao.
Hatua hiyo, amesema ikasababisha vijana hao 10 waachiwe na vurugu ziliendelea zikishinikiza kununuliwa kwa pikipiki mpya ili kulipa iliyochomwa moto wakati wa vurugu za siku ya kwanza.
“Mkuu wa wilaya anaendelea kuzungumza nao akitaka waruhusu mwili uzikwe, na yeye atahakikisha pikipiki mpya inaletwa kesho,” amesema.
Ilipofika saa 12:35 jioni, amesema Polisi walifika katika eneo hilo na kuanza kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wamefunga barabara na hatimaye zikafunguka.
Alipotafutwa kuzungumza hilo, Kamanda Maigwa, amesema ni mapema mno kufafanua kinachoendelea kwa sababu ndio kwanza askari wameenda eneo la tukio kushughulikia.
"Ni kweli kuna vurugu na askari wetu wapo eneo la tukio kushughulikia. Kwa hatua ya sasa sina cha zaidi ninachoweza kusema, tusubiri tuone," amesema.
Hata hivyo, baadaye Maigwa ameiambia Mwananchi kuwa, hali imeshatulia na yeye yupo katika eneo la tukio kushughulikia.
Ilianzaje
Juni 12, 2026 kulitokea vurugu zilizosababisha abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Rombo kwenda maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine kukwama kwa zaidi ya saa tatu baada ya vurugu zilizoibuka katika eneo la Uuwo Mwika, Wilaya ya Moshi.
Sababu ya vurugu hizo, ni madai ya mmoja wa dereva bodaboda kugongwa na kufariki dunia.
Imedaiwa dereva huyo ambaye alihisiwa kuwa amebeba dawa za kulevya aina ya mirungi alikuwa akikimbizwa na gari linalodaiwa kuwa la polisi kutoka Rombo na na akagongwa na gari hilo wakati wa purukushani na kusababisha kifo hicho.
Tukio hilo lilidaiwa kuwatia hasira wananchi wa eneo hilo pamoja na madereva bodaboda kutoka mpakani mwa Wilaya ya Moshi na Rombo na hivyo walifunga barabara kuu ya Rombo-Moshi na kusababisha usumbufu kwa abiria.
Hata hivyo, polisi waliofika katika eneo hilo walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao.
Kutoka na hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, kuongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, kufika eneo hilo la tukio na kutuliza vurugu hizo na kurejesha hali ya utulivu.