Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita Mashariki ya Kati vinavyoathiri bei za vyakula, mafuta Tanzania

Muktasari:

  • Athari za vita hivyo zinajitokeza katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, hususan katika sekta za nishati, uchukuzi, viwanda, biashara na kilimo.



Dar es Salaam. Serikali imeeleza namna Tanzania ilivyoathirika na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati baina ya Iran, Israel na Marekani, huku ikiahidi kuchukua hatua za kisera kulinda uthabiti wa uchumi wake.

Mbali na hilo, imesema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 utapimwa kwa viashiria vya matokeo (KPIs) badala ya wingi wa miradi, katika hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Hayo ni sehemu ya taarifa ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2026/27, uliowekewa misingi 10 ya utekelezwaji wake, kama yalivyobainishwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkumbo alikuwa anawasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27.


Athari vita

Awaziri huyo alisema vita vya Iran vimeathiri minyororo ya usambazaji wa bidhaa na huduma duniani kwa kuongeza gharama za usafirishaji wa mizigo na muda wa usafirishaji.

Pia, baadhi ya kampuni za usafirishaji zimebadilisha njia za usafirishaji ili kuepuka maeneo yenye migogoro iliyoongeza gharama za biashara ya kimataifa.

Alisema hali hiyo imeathiri upatikanaji wa baadhi ya bidhaa muhimu zikiwemo mafuta, mbolea, malighafi za viwandani na bidhaa za chakula katika baadhi ya masoko duniani.

Kwa Tanzania, alieleza kuwa athari za vita hivyo zinajitokeza katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, hususan katika sekta za nishati, uchukuzi, viwanda, biashara na kilimo.

Moja ya maeneo ni uingizaji wa mbolea, ambayo alisema Tanzania huagiza asilimia 30 hadi 40 ya mbolea aina na Urea na DAP kutoka nchi za Ghuba, hususan Qatar.

Hivyo, alisema vita hivyo vinatarajiwa kusababisha ongezeko la gharama za uingizaji wa mbolea na kusababisha kuongezeka kwa bei katika soko la ndani, hali itakayoathiri shughuli za kilimo kwa msimu ujao wa mwaka 2026/27.

Kwa upande wa mafuta, Profesa Kitila alisema Tanzania huagiza asilimia 100 bidhaa za petroli zilizosafishwa kutoka nje ya nchi, sawa na asilimia 13 ya thamani ya bidhaa zote zinazoagizwa nchini.

Alisema sehemu kubwa ya mafuta hayo, asilimia 60 hadi 70, huagizwa kutoka nchi za Ghuba, husuani Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, na Kuwait; pamoja na  India na Singapore.

“Pamoja na athari zingine, kuongezeka kwa bei za mafuta kumeongeza gharama za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa na huduma.

“Aidha, suala hili linaweza kuiathiri sekta ya utalii inayochangia takriban dola za Marekani 4,410.6 milioni na kutoa ajira takribani milioni 1.5 kupitia ongezeko la bei ya tiketi za ndege na kuahirishwa kwa safari za ndege,” alisema.

Waziri huyo, alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na migogoro ya kidunia.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha usimamizi wa sera za fedha na bajeti ili kudhibiti mfumuko wa bei; kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala; kuimarisha uhifadhi wa akiba ya mafuta; pamoja na kuendelea kutafuta masoko mbadala ya bidhaa zinazouzwa nje.

Alisema Serikali inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa muhimu ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje hususani mbolea na baadhi ya malighafi za viwandani.

Profesa Kitila, alisisitiza jitihada zinaendelea kufanyika katika kuimarisha sekta za usafirishaji, biashara na uwekezaji ili kuongeza ustahimilivu wa uchumi wa Taifa dhidi ya mishtuko ya kiuchumi ya kimataifa.

“Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa dunia na athari za migogoro ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa hatua za kisera zinazochukuliwa zinaendelea kulinda uthabiti wa uchumi wa Taifa, ustawi wa wananchi na mazingira ya biashara na uwekezaji nchini,” alisema.


Deni la Serikali

Kuhusu deni la deni la Serikali, Profesa Mkumbo alisema  limeongezeka hadi kufikia Sh114.34 trilioni Machi mwaka huu, kutoka Sh104.93 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 8.97.

Kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa Sh38.44 trilioni na deni la nje lilikuwa Sh75.89 trilioni.

“Ongezeko la deni linatokana na Serikali kuendelea kupokea mikopo mipya na ya zamani kutoka vyanzo vya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema Profesa Mkumbo.

Licha ya deni hilo kuongezeka, bado ni himilivu huku tathmini iliyofanyika Novemba 2025 ikibainisha kuwa deni la Serikali ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na mrefu.


Nguzo za mpango

Katika wasilisho lake hilo, Profesa Kitila alitaja maeneo 10 ambayo ni msingi wa utekelezaji wa mpango wa Taifa, ambayo ni kuendelea kuwepo kwa demokrasia, amani, usalama na utulivu, kudumisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria na kuendeleza miundombinu wezeshi ikiwemo nishati, bandari, barabara na reli.

Maeneo mengine, alisema ni matumizi ya teknolojia za kidijitali katika uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na kutumia fursa zinazotokana na ushirikiano wa kikanda.


Dira kupimwa kwa KPIs

Aidha, Profesa Kitila alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026 ni nyenzo ya kwanza katika kuanza utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/27 – 2030/31 na Dira 2050.

Alisema Serikali imekamilisha nyenzo zote muhimu za utekelezaji wa Dira 2050.

“Mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 na mikakati yake yatapimwa kwa kuzingatia viashiria vya matokeo (Key Performance Indicators – KPIs) kwa kila sekta na sio wingi wa shughuli au michakato ya utekelezaji.

“Katika kufikia azma hii, Sekretarieti ya Tume itajielekeza na kujikita katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo (Delivery Bureau)” alisema profesa Kitila wakati akiwasilisha taarifa hiyo.

Alizitaja nyenzo hizo ni Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2026/27 – 2050/51); Mpango wa Nne wa Maendeleo wa miaka Mitano (2026/27 – 2030/31); Mwongozo wa Kitaifa wa Uandaaji Mipango; na Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo.

Nyenzo nyingine ni Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira 2050 wa Miaka mitano 2026/27 – 2030/31.

“Kufuatia kukamilika kwa nyenzo hizo za utekelezaji wa Dira 2050, kazi iliyo mbele yetu sasa ni moja tu: kutekeleza,” alisema.


Idadi ya watu juu

Idadi ya watu nchini imeongezeka kwa takriban asilimia 2.8 ndani ya mwaka mmoja, kutoka watu milioni 66.27 mwaka 2024 hadi milioni 68.15 mwaka 2025.

Hiyo ni sawa na ongezeko la karibu watu milioni 1.9 ndani ya mwaka mmoja. Kwa siku wanaongezeka takriban watu 5,100, sawa na takriban watu 215 kwa saa.

Kwa mujibu wa Profesa Kitila, kasi ya ongezeko la watu inaendelea kutoa fursa chanya kwa maendeleo ya nchi, ikiwemo upatikanaji wa nguvu kazi ya kutosha na uwezekano wa kuchochea mageuzi ya kidijitali katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Fursa hizo, alisema zinaimarishwa zaidi na uwiano wa kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35, ambao ni nguzo muhimu ya ustawi wa uchumi wa kisasa.