Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CECOT, gereza lililovunja magenge hatari duniani

Mkuu wa gereza anasogea mbele kidogo, anamtazama kwa makini mwanamume aliyejaa michoro ya tattoo kuanzia chini ya taya hadi kiunoni, kisha kwa utulivu anasema: “Hili ni gereza lenye kiwango cha juu cha usalama, hawatatoka tena maishani mwao.”

Pembeni yake, wanaume kadhaa waliovaa kaptura na fulana nyeupe wanamtazama wakiwa kimya kutoka vyumba vya vyuma vizito vya seli. Vichwani mwao wana upara. Macho yao yanaonyesha ni watu waliopoteza matumaini.

Hapa ndipo unapokaribishwa ndani ya CECOT (Centro de Confinamiento del Terrorismo) gereza lililozua mjadala mkubwa kuliko magereza yote duniani, likichunguzwa kwa karibu na jumuiya ya kimataifa, huku wengine wakiliona kama hatua iliyobadili historia ya mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa.

Wafungwa wa Gereza la CECOT. Picha na Mtandao

Gereza hilo limejengwa pembezoni mwa misitu, takribani kilomita 75 kusini mashariki mwa Mji wa San Salvador, katika eneo la Tecoluca ambalo kwa miaka mingi halikujulikana duniani.

Hali hiyo ilibadilika baada ya Rais wa El Salvador, Nayib Bukele, kuligeuza kuwa kitovu cha kampeni kali dhidi ya magenge ya uhalifu katika karne hii ya 21.

Bila kujali kuwa kuna mtu anaona yanayotokea ndani ya kuta zake, kama vile utekelezaji wa haki au ukatili uliopitiliza, jambo moja halina ubishi; CECOT imeibadilisha El Salvador na kwa kiasi kikubwa imebadili namna dunia inavyojadili usalama, haki za binadamu na mamlaka ya dola.


Taifa lilikata tamaa

Kwa miongo kadhaa, taifa hilo dogo la Amerika ya Kati lilijulikana kama moja ya maeneo hatari zaidi duniani kwa mauaji.

Miaka michache iliyopita, El Salvador ilitajwa kama ‘mji mkuu wa mauaji duniani’ ikiwa na kiwango kikubwa zaidi cha mauaji kuliko nchi yoyote duniani.

Katika hali halisi, sehemu kubwa ya nchi ilikuwa chini ya ushawishi wa magenge ya uhalifu. Makundi hayo yalitawala maeneo mbalimbali kwa kutumia mauaji, vitisho, ukandamizaji na mfumo wa utozaji fedha kwa nguvu.

Magenge mawili yaliyokuwa kiini cha machafuko hayo yalikuwa Mara Salvatrucha (maarufu MS-13) na 18th Street linalojulikana pia kama ‘Barrio 18’. Mizizi ya makundi hayo ilianzia mitaa ya Kusini mwa California nchini Marekani. Baadhi ya wanachama wake walifukuzwa na kurejeshwa El Salvador miaka ya 1990 baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Ulinzi ukiimarishwa nje ya Gereza la CECOT. Picha na Mtandao

Waliporejea, walikuta kizazi cha vijana waliokosa matumaini, waliotengwa kijamii na wasio na imani na serikali. Kilichoanza kama uhalifu mitaani kiligeuka kuwa mtandao mkubwa wa kikatili ulioteka jamii nzima.

Mitaa na vitongoji vilianza kutawaliwa na magenge ya uhalifu. Wakazi walilazimika kulipa fedha za ulinzi, waliokataa waliuawa. Madereva wa mabasi walitozwa kodi kila wiki, waliokaidi walipigwa risasi wakiwa kazini. Watoto waliingizwa kwenye magenge hayo kwa nguvu au kutishwa wasitoe taarifa kwa vyombo vya dola.

Mamlaka zinasema katika kilele cha nguvu zao, magenge hayo yalikuwa yanadhibiti takribani asilimia 85 ya eneo la nchi.

Wafungwa wa Gereza la CECOT wakiwa chini ya ulinzi mkali. Picha na Mtandao

Ni hali sawa na taifa kuwa na ‘serikali ndani ya serikali’ mfumo wa utawala unaoendeshwa si na viongozi waliochaguliwa, bali na vijana wenye michoro ya ‘tattoo’ mikononi, mapanga na silaha nzito. Hapa ndipo alipokuja Bukele.


Kishindo cha Bukele

Nayib Bukele aliingia madarakani mwaka 2019 kama mwanasiasa kutoka nje ya mfumo wa kawaida wa vyama vya siasa. Alijijengea taswira ya kiongozi asiyeogopa kuvunja taratibu za zamani, kiasi cha kujitambulisha kuwa ‘dikteta mwenye mvuto zaidi duniani.’

Wakosoaji wake walimwona kama tishio kwa demokrasia. Wafuasi wake waliofikia mamilioni ndani na nje ya El Salvador, walimwona kuwa mtu ambaye taifa lilimuhitaji kwa dharura.

Katika miaka ya mwanzo madarakani, kiwango cha mauaji kilianza kushuka. Serikali yake ilieleza mafanikio hayo kwamba yalitokana na Mpango wa Kudhibiti Maeneo, ingawa wachambuzi waliendelea kubishana kuhusu sababu halisi za kupungua kwa uhalifu huo.

Wafungwa wa Gereza la CECOT wakifanya mazoezi chini ya ulinzi mkali. Picha na Mtandao

Kisha ikafika ‘wikendi’ iliyobadili kila kitu. Kati ya Machi 25 na 27, 2022 watu 87 waliuawa ndani ya siku tatu kutokana na mashambulizi ya magenge ya uhalifu. Taifa lilishtuka. Ilionekana wazi kwamba magenge hayo yalikuwa yametoa tangazo la vita dhidi ya serikali.

Majibu ya Bukele yalikuwa ya haraka na makubwa. Alitangaza hali ya hatari ya kitaifa. Hatua hiyo iliyoongezwa mara kwa mara hadi leo, ilitoa mamlaka mapana kwa vikosi vya usalama kuwakamata watu wanaoshukiwa kuwa wanachama au washirika wa magenge hayo.

Chini ya utaratibu huo, baadhi ya haki za msingi zilizolindwa na Katiba zilisimamishwa kwa muda ikiwamo uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kushirikiana, haki ya kupata uwakilishi wa kisheria na taratibu za kawaida za mahakama.

Operesheni za kukamata watu zikaanza. Makumi ya maelfu walikamatwa na serikali ilihitaji mahali pa kuwapeleka.


Kufunguliwa kwa CECOT

Januari 31, 2023, Bukele alizindua rasmi ‘Kituo cha Kufungia Magaidi-  CECOT’ katika eneo lisilo na makazi karibu na Tecoluca. Gereza hilo linatajwa kuwa kubwa zaidi Amerika ya Kusini kwa uwezo wa kuhifadhi wafungwa.

Wafungwa wakiwa katika seli ya pamoja katika Gereza la CECOT. Picha na Mtandao

CECOT lina mabanda manane makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi hadi wafungwa 40,000. Limejengwa kwenye eneo la hekta 166 za tambarare zilizozungukwa na misitu. Kila banda lina seli 32 zilizozungushiwa vyuma vizito vya chuma.

Kuanzia siku ya kwanza, gereza hilo halikujengwa kwa lengo la kurekebisha tabia za wafungwa. Lengo kuu lilikuwa kuwafungia na kuwazuia kabisa kurejea uraiani.

Wafungwa wa CECOT hawaruhusiwi kupokea wageni wala kwenda nje kuona mwanga wa jua. Hakuna programu za elimu wala mafunzo ya kuwaandaa kwa maisha ya baadaye. Ukumbi wa chakula, sehemu za michezo na ukumbi wa mazoezi uliopo ndani ya gereza umetengwa kwa ajili ya askari na walinzi.

Wafungwa wa Gereza la CECOT wakiwa chini ya ulinzi mkali. Picha na Mtandao

Takribani maofisa 1,000 wa magereza, wanajeshi 600 na askari 250 wa kikosi cha kutuliza ghasia hulinda eneo hilo kila siku. Cha kushangaza, wanachama wa MS-13 na Barrio 18 ambao kwa miaka mingi walikuwa maadui wakubwa wanawekwa ndani ya mfumo mmoja wa gereza.


Takwimu za kushtua

Matokeo ya kampeni ya Bukele dhidi ya magenge ya uhalifu yameendelea kuibua mjadala duniani. Kwa baadhi ya watu ni mafanikio ya kihistoria. Kwa wengine ni ushindi uliopatikana kwa gharama ya kuvunja misingi ya haki na demokrasia.

Serikali ya El Salvador inasema kiwango cha mauaji kilipungua kwa zaidi ya asilimia 98 kati ya mwaka 2015 na 2024. Mwaka 2018 kabla ya Bukele kuingia madarakani kiwango cha mauaji kilikuwa watu 53.1 kwa kila watu 100,000. Kufikia mwaka 2024 kiwango hicho kilishuka hadi watu 1.9 kwa kila watu 100,000.

Ofisa wa gereza wa CECOT akimfunga pingu mikono mfungwa kabla ya kuamriwa kutoka katika seli ya pamoja. Picha na Mtandao

Kwa idadi halisi, mauaji yalipungua kutoka watu 2,398 mwaka 2019 hadi watu 114 mwaka 2024.

Mwaka 2025 ukaweka rekodi mpya, El Salvador iliripoti mauaji 82 pekee kwa mwaka mzima, kiwango cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya nchi hiyo.

Raia wa kawaida walioishi kwa hofu kwa miaka mingi walianza kuhisi maisha yanarudi kawaida. Maeneo yaliyokuwa yakitawaliwa na watu wenye silaha yalianza kurejea mikononi mwa wananchi, utalii ukaongezeka. Vilevile, thamani ya nyumba ikapanda na watoto wakaanza kucheza katika mitaa iliyokuwa ikiogopwa hapo awali.

Umaarufu wa Bukele ukaendelea kupaa, huku tafiti zikionyesha kiwango cha uungwaji mkono kinachozidi asilimia 80.


Gharama ya amani

Lakini nyuma ya takwimu hizo za kuvutia, kuna upande mwingine wenye giza kubwa. Zaidi ya Wasalvador 80,000 wamekamatwa tangu kutangazwa kwa hali ya hatari mwaka 2022. Mwaka 2024, Bukele alikiri kuwa watu wasiopungua 8,000 waliokamatwa hawakuwa na hatia, hivyo waliachwa huru.

Baadhi ya wafungwa wa Gereza la CECOT wakiwa katika seli ya pamoja.

Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakikosoa mfumo huo kwa madai kuwa serikali imeweka matokeo mbele kuliko haki.

Ripoti kadhaa zinaeleza kuhusu msongamano mkubwa magerezani, uhaba wa huduma za msingi za usafi, ukosefu wa haki za kisheria na mazingira yasiyozingatia utu wa binadamu.

Taarifa zinaonyesha kuwa mamia ya wafungwa wamefariki dunia wakiwa mahabusu tangu mwaka 2022. Wengi hawakuwahi kufikishwa mahakamani, huku wengine hawakuwa na mawakili. Baadhi yao walikuwa vijana wenye umri mdogo.

Hata hivyo, uongozi wa magereza nchini humo hauonyeshi kujutia chochote. Mkurugenzi wa gereza, Belarmino García, amewahi kusema kuwa waliomo ndani ya CECOT ni “watu wenye hulka hatari ambao ni vigumu kurekebishika.” Akaongeza kwa kusisitiza: “Ndiyo maana wako hapa.”


Marekani na CECOT

Umaarufu wa CECOT duniani uliongezeka zaidi mwaka 2025 baada ya Marekani kuanza kupeleka wahamiaji wanaodaiwa kuwa wanachama wa magenge ya uhalifu kwenda kutumikia kifungo hapo.

MNwonekano wa Gereza la CECOT.

Utawala wa Rais, Donald Trump ulitangaza mpango wa kuwahamishia El Salvador mamia ya watu wanaotuhumiwa kuwa wanachama wa genge la Tren de Aragua kutoka Venezuela.

Bukele alikubali kuwapokea kwa makubaliano maalumu ambayo Marekani ilitakiwa kulipia gharama za kuwahifadhi.

Lakini hatua hiyo ilizua mgogoro mkubwa wa kisheria na kidiplomasia. Baadhi ya waliopelekwa CECOT walidai hawakuwa wahalifu, huku mashirika ya haki za binadamu yakidai mfumo huo ulikuwa ukiwanyang’anya watu haki zao za msingi.

Baadhi ya Wavenezuela waliowahi kushikiliwa humo baadaye walieleza mateso, mazingira magumu na madhila waliyopitia ndani ya gereza hilo.


Waiga mfumo wa CECOT

Athari za CECOT sasa zimeanza kuonekana katika nchi nyingine zinazopambana na magenge ya uhalifu.

Mataifa kadhaa ya Amerika ya Kusini tayari yametangaza mipango ya kujenga magereza yanayofanana na mfumo wa El Salvador. Viongozi mbalimbali wamekuwa wakitembelea CECOT kutafuta mbinu za namna ya kutumia mfumo huo katika nchi zao.

Swali kubwa linalobaki ni je, dunia inaiga mafanikio ya kupunguza uhalifu au inaiga mfumo wa ukandamizaji?

CECOT imeigawa dunia katika makundi mawili. Kwa wananchi waliokuwa wanaishi kwa hofu kila siku, gereza hilo linaonekana kama muujiza uliorudisha usalama na utulivu.

Lakini kwa familia za wale waliokamatwa pasipo kuwa na kesi, uwakilishi wa kisheria na bila matumaini ya kutoka, CECOT ni ishara ya namna dola inavyoweza kutumia nguvu kupita kiasi pale jamii inapokubali haki za baadhi ya watu zipuuzwe.

Watafiti wengi wanakubali kuwa sera za Bukele zimechangia kwa kiwango kikubwa kupungua kwa mauaji nchini El Salvador. Hata hivyo, wakosoaji wanaonya kuwa mafanikio hayo yameambatana na kudhoofika kwa misingi ya kidemokrasia, kupungua kwa uhuru wa kiraia na kuongezeka kwa mamlaka ya rais juu ya mihimili mingine ya dola.

Bukele amewahi kusema kwamba CECOT ni gereza linalokosolewa zaidi duniani. Kwa namna moja au nyingine, huenda hiyo ndiyo sababu limekuwa moja ya magereza yanayojadiliwa zaidi katika historia ya dunia ya sasa.