Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachapwa bakora kwa kuvuruga familia Bukombe

Mkazi wa Nyahulukulu ,Ushirombo Wilaya ya Bukombe Mkoa wa  Geita , Kabura Isaka akimsimulia mwandishi wa gazeti hili , Ernesti Magashi namna  alivyonusurika kipigo kwa mumewe  baada ya kumnyima fedha za mpango wa Tasaf wa kusaidia kaya maskini hivi karibuni . Picha na Mpigapicha wetu.

Muktasari:

Kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo kunafuatia malalamiko ya baadhi ya wanawake wa kijiji hicho kwamba waume zao wamekuwa wakichukua fedha walizopewa na Tasaf kwa ajili ya kuziwezesha familia hizo kujikimu kwa chakula na ada za shule.

Bukombe. Sungusungu wameaza kutekeleza maagizo ya viongozi wa Kijiji cha Ihulike, Kata ya Bukombe mkoani Geita la kuwachapa bakora wanaume waliopora fedha za mradi wa Maendeleo ya Jamii, (Tasaf) kutoka kwa wake zao na kwenda kunywea pombe wakikwamisha malengo ya kuziondoa katika umasikini.

Kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo kunafuatia malalamiko ya baadhi ya wanawake wa kijiji hicho kwamba waume zao wamekuwa wakichukua fedha walizopewa na Tasaf kwa ajili ya kuziwezesha familia hizo kujikimu kwa chakula na ada za shule.

Kiongozi wa Sungungungu wa kijiji hicho, Joseph Mapinda ameliambia gazeti hili katika mahojiano kijijini hapo kwamba siku chache baada ya mradi wa Tasaf kukabidhi fedha kwa kinamama wanaotoka kaya maskini, baadhi ya wanaume walipora fedha hizo kwa wake zao na kwenda kutumia kwa kunywea pombe.

Anasema katika utekelezaji wa mikakati yake, mwenyekiti wa kitongoji hicho anashirikisha kikosi cha sungusumgu kukomesha tabia za wanaume walevi wanaopiga wake zao na kuchukua fedha hizo kisha kwenda kufanyia starehe.

Anasema kuwa tayari sungusungu imewachapa bakora wanaume wawili wa kitongoji cha Nyahulukulu baada ya kubainika wametumia fedha hizo kwa kunywea pombe.

Mapinda anabainisha kuwa wanaume hao walithibitika kutumia fedha za familia kwa kunywea pombe, huku mmoja pia akitozwa faini baada ya kumjeruhi mtu kwa kumpasua kwenye paji la uso kwa jiwe alipokuwa amelewa.

Anasema sungusungu ni chombo kinachofanya kazi kwa mwongozo wa sheria ndogondogo zilizowekwa na uongozi kuanzia ngazi ya kitongoji kwa kushirikiana na wenyeviti wa vitongoji.

“Kwa mamlaka iliyonayo serikali ya kijiji ikisema chapa bakora kadhaa hawa, mimi lazima nitekeleze agizo kwani lengo ni kudhibiti tabia mbaya, wanawake na wao wawe na haki ya kufikia malengo kupitia mradi wa Tasaf,” anasema.

Mkazi wa kitongoji cha Nyahulukulu, Ng’walu Misobi anasema alipata kipigo kutoka kwa mume wake, baada ya kumnyima fedha za Tasaf alizotaka akanywe pombe.

Anasimulia kuwa mwezi ulipopita baada ya kupokea fedha hizo za Tasaf, alifika nyumbani saa 11:00 jioni akiwa na Sh 40,000 ambapo muda mfupi baadaye mume wake alifika na kuamuru ampe fedha hizo.

“Nilikataa, lakini alinilazimisha huku akisema kabla hajaaza kunipiga nikusanye nguo zangu, niende kwetu,”anasema Ng’walu.

Anaeleza kuwa alitoka nyumbani na saa 1.00 usiku alivyorudi mumewe akamuuliza alipokuwa.

“Kwa nini hujaenda kwenu, baada ya hapo alianza kunipiga huku akisema; Nakuua. Niliona nimpe fedha, akasema ni kidogo huku akidai wanaume wenzake wamepewa Sh50,000 na wake zao mbona mimi nimempa kidogo”,”anasimulia.

Anaongeza kuwa aliendelea kupokea kipigo na kuvutwa nje ya nyumba, ndipo alipofanikiwa kuponyoka na kukimbilia kwa mwenyekiti wa kitongoji kuomba msaada.

“Nikahifadhiwa baada ya kujieleza. Malengo yangu yalikuwa ninunue kuku ili nifuge na ninunue sare na viatu vya shule kwa binti yetu Nyunis Masalu (12) anayesoma,”anasema Ng’walu akiongeza kuwa mtoto huyo aliachia shule kutokana na kukosa sare pia ni mtoro.

Naye Nyunis anaeleza kuwa licha ya kushindwa kwenda shule kwa kukosa sare na viatu, akiwa nyumbani alishuhudia baba yake akimpiga mama yake na kwamba fedha zilizotolewa na Tasaf zilitumiwa na baba pekee badala ya familia.

Baba wa familia hiyo, Masalu Kapani anasema: “Nilipigwa viboko vitano na sungusungu, kweli kitendo nilichokifanya kwa mke wangu na familia ni kibaya.

Lakini sikujua ninachofanya kutokana na pombe niliyokunywa siku hiyo. Siwezi kuingilia tena mipango yake ya maendeleo anayoelekezwa na Tasaf.”

Kapani anaongeza: “Sungusungu walivyonipa adhabu, sitarudia kuomba fedha ya Tasaf. Famila yangu inisamehe.”

Mwanamke mwingine mkazi wa kitongoji hicho, Kabra Isaka anasema yeye na familia yake hawakunufaika na fedha hizo za Tasaf ingawa walipokea Sh36,000 kwani zote zilichukuliwa na mumewe aliyemtaja kwa jina moja la Pima.

Isaka anasema alipokea fedha hizo kisha kurejea nyumbani na kumkuta mume wake akisubiri fedha hizo akanywe pombe na alimpa Sh5,000 ili kuondoa kelele.

Anasimulia kuwa siku hiyo mumewe baada ya kulewa alipigana na watu wengine na yeye alipewa taarifa kwamba amekamatwa kwa kufanya fujo na alipomfuatilia alikuta amefungwa kamba baada ya kujeruhi wenzake.

Isaka anaeleza kuwa mwenyekiti na wazee wa kijiji hicho waliamuru sungusungu imchape viboko vitano iwe adhabu kwa kutumia fedha hizo pia amtibie aliyemjeruhi kwa jiwe usoni.

“Mume wangu alipokuwa akicharazwa viboko nilimhurumia, baada ya kumaliza adhabu walielewana na mtu aliyemjeruhi kwamba amlipe Sh 20,000 kwa ajili ya matibabu, nami nikatoa fedha ya Tasaf,” anasimulia.

“Nilibaki na Sh9,000 nikanunua mafuta ya kujipaka watoto na dawa za kunywa mtoto moja aliyekuwa na homa kutokana. Tabia ya mume wangu ilifanya nisifikie malengo niliyojiwekea,” anasema Isaka.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyahulukulu, Clisent Frank huku akikiri matukio hayo anasema: “Lakini mkakati uliopo ni kuhakikisha wanaume wanaotumia ubabe kwenye fedha za mradi wa Tasaf kusaidia kaya maskini wanadhibitiwa. Sitakubali fedha hizo zitumiwe nje na utaratibu.”

Mwenyekiti wa kitongoji cha Bukwaya, Albert Pastory anapongeza sungusungu kwa kudhibiti tabia ya wanaume walevi akisisitiza sungusungu wahakikishe wanaume walevi wanachapwa bakora.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha anasema hana taarifa ya vitongoji hivyo kudhibiti wanaume walevi, lakini anaeleza hatua hiyo ni sahihi kwani lengo la serikali kupitia Tasaf ni kusaidia kaya maskini.