Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuanguka jengo na aibu kwa viongozi

Muktasari:

Ijumaa iliyopita wakati baadhi ya wakristo duniani kote wakisubiri kwa hamu kubwa kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, taarifa mbaya ilitangazwa kupitia njia mbalimbali kuwa zaidi ya watu 50 walifukiwa na kifusi baada ya jengo moja Jijini Dar es Salaam lenye ghorofa 16 kuporomoka.

Dar es Salaam. Ijumaa iliyopita wakati baadhi ya wakristo duniani kote wakisubiri kwa hamu kubwa kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, taarifa mbaya ilitangazwa kupitia njia mbalimbali kuwa zaidi ya watu 50 walifukiwa na kifusi baada ya jengo moja Jijini Dar es Salaam lenye ghorofa 16 kuporomoka.

Wapo waliodai kuwa baadhi ya wale ambao walikuwa chini ya kifusi,wakati fulani walikuwa wakiwapigia simu jamaa zao wakiomba waende kuwaokoa, kwa bahati mbaya suala la uokoaji lilikuwa gumu, hasa kutokana na vifaa duni vilivyoonekana eneo la tukio.

“Alinipigia simu nije nimuokoe, nilipofika hapa na kuanza kumpigia hapokei tena,”anasema jamaa mmoja akiwa eneo la tukio kabla ya kuondoka ghafla kwa hasira.

“Hapa hakuna dalili ya mtu kuwa hai, huwezi kuwa hai kwa kufikiwa na jengo la ukubwa kama huu wa ghorofa 16, hewa utatoa wapi, lazima utapondeka,” alisema jamaa huyo akimueleza mtu mwingine kwa njia ya simu, huku akionekana kuchanganyikiwa kwa tukio hilo.

Taarifa za awali

Ijumaa iliyopita saa 2.30 asubuhi Watanzania waliingia katika vilio baada ya jengo lililokuwa limefikia ghorofa ya 16, lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi kuporomoka.

Inaelezwa kuwa jengo hilo lilikuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Limited liliporomoka wakati mafundi na vibarua wakiendelea na ujenzi huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Haijajulikana idadi kamili ya waliokuwamo ndani yake, ila kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, zaidi ya watu 22 hadi jana walithibitiwa kufa.

Wengi wanalalamika

Wananchi wengi wanaona suala la ujenzi nchini ni kama halisimamiwi vyema, huenda ni kwa maslahi ya baadhi ya viongozi na jamaa zao.

Maisha yanachukuliwa kama kitu chepesi kwa wenye fedha, kwani wanachojali ni kubana matumizi na matokeo ya mabano ya matumizi hayawahusu tena.

Ziliwahi kutolewa ahadi

Hili si jengo la kwanza kuporomoka. Hali kama hiyo ilishawahi kutokea, kwa mfano mwaka 2006, baada ya kuporomoka jengo la hoteli ya Chang’ombe Village Inn, Keko jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo, tume iliundwa kuangalia ubora wa majengo jijini.

Tume imefanya kazi yake, nini kinaendelea? Ni swali ambalo kila mwenye akili timamu anapaswa kujiuliza.

Tume ilibaini

Tume hiyo iliyoundwa baada ya kuporomoka jengo la Hoteli ya Chang’ombe Village Inn, ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam kwa wakati ule yalijengwa kinyume cha taratibu za ujenzi, huku baadhi ya wananchi wakihofia rushwa kufifisha harakati zaidi kuchukuliwa dhidi ya waliobainika kujenga bila kufuata taratibu.

Kwa ujumla, ilibainika kuna tatizo kubwa katika sekta ya ujenzi.

“Kinachoonekana ni kama Serikali imekuwa na ujanja wa kuunda tume sio kwa ajili ya kushughulikia mambo, bali kuzubaisha watu wasifuatilie wakijua tume inaundwa, halafu hakuna kinachofanyika,” anasema Halima Shomari, mkazi wa Mbezi Beach akiwa eneo la tukio.

Anaongea Halima “Wengi wanaona kwamba maelekezo ya Tume yaliachwa kwenye makabrasha au labda wakubwa walifungia vitumbua, hili ni tatizo ambalo Tanzania lazima libadilike kama kweli tunataka kuwa na maendeleo ya kasi”.

Hali ya jengo

Wengi wanaona kwamba ujenzi huenda haukuwa umezingatia taratibu, ukiangalia kilichobaki pale katika kifusi kwa macho pekee unaweza kusema kulikuwa na ulipuaji.

“Ukiangalia hata usukaji wa nondo, hasa kuwa na vumbi jingi badala ya mabonge, inatia mashaka kama kweli ujenzi ulizingatia viwango,” anahoji Halima.

‘Wazee wa Unda tume’

Baadhi ya wananchi waliokuwapo eneo la tukio walisikika wakisema ‘tatizo linaonekana wazi kwamba ni usimamizi mbaya, lakini kesho tutasikia tume inaundwa kuchunguza, huko kutakuwa ni kupoteza fedha za wananchi...nchi hii imejaa watu ambao tunaweza kuwaita ‘unda tume’, kwa bahati mbaya zaidi hawafanyii kazi kinachoonekana kwenye tume.

Wachambuzi wanabainisha kwamba wakati nchi inaonekana kukua kiuchumi na ujenzi wa majengo kuongezeka, ni lazima Serikali iwe makini zaidi katika kusimamia majengo.

Baadhi ya watu waliohojiwa baada ya ghorofa lile kuanguka, walieleza kutoridhishwa na aina ya ujenzi unaofanywa na mjenzi na hili linaweza kwenda mbali zaidi.

Kwa vyovyote itakavyokuwa, lakini kinachoonekana ni uzembe wa Serikali katika kufuatilia suala zima la ujenzi, na hata zinapoundwa tume kama ambazo tayari zingine zimeundwa ni kama hazifanyiwi kazi ipasavyo.Wananchi wengi wanaona kwamba kuanguka kwa jengo hili ni aibu kwa viongozi hasa wale ambao wamepewa matokeo kuhusu hali ya majengo 100 Jijini, kisha hakuna la maana walilofanya.

Wakubwa waongea utafikiri hawana taarifa kwamba kuna tume ilibaini zaidi ya majengo 100 Dar ni feki

Baada ya kupewa taarifa juu ya tukio hilo, Rais Kikwete alimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha wahusika wa ujenzi wa jengo hilo wanakamatwa akiwamo Mkadiriaji Majengo (Quantity surveyor), mchora ramani za majengo (Architecturer), Mhandisi Mshauri (Consultant) na Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam.

Ingawa Rais Kikwete hakuhoji kuhusu uchunguzi wa maghorofa 100 yaliyobainika kuwa hayafai Jijini Dar es Salaam, baada ya kutembelea eneo la tukio, Rais Kikwete aliagiza wahusika wote wa ujenzi huo wachukuliwe hatua kali. Habari zinadai Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya Kinondoni, Ibrahim Kisoka ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya ujenzi, na Mhandisi Mshauri kwa pamoja wamejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi.

Pinda hana la kusema

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni kati ya watu waliotembelea eneo la tukio, hata waandishi walipomuhoji unasemaje  bwana mkubwa, akasema “Sina la kusema”.

Huenda anachoweza kuwaridhisha Watanzania ni kuzungumzia kwanini majengo 100 yaliyoonekana hayafai mwaka 2006 hadi leo kimya.Kuna nini kilichofichika nyuma ya uchunguzi huu ambao uliorodhesha majengo yasiyofaa?

Uokoaji wa kibabaishaji

Baadhi ya wananchi walilalamikia shughuli ya uokoaji. Muda mwingi ulitumika kuhangaika kuondoa kifusi kwa mikono huku tukiwa hatuna vifaa vya kuangalia uhai wala mashine zinazoweza kurahisisha kazi ya kusomba kifusi hatua kwa hatua, kitendo ambacho ni cha kushangaza mno.

“Ombi langu ni kwa Serikali kuchungua hatua na kuacha rushwa, kwani kuna ishara za wazi kwamba rushwa ndio inasababisha watu wasichukuliwe hatua hata pale tume inapoonyesha kwamba wana kasoro,” anasema mama Juanita Mhawi, mkazi wa Gongo la Mboto Jijini Dar es Salaam.