Foleni na jinsi zinavyobadili mfumo wa maisha Dar

Magari yakiwa yamekwama katika barabara ya Morogoro enoe la Kimara jijini Dar es Salaam juzi, wakazi wanatoke Mbezi na Kimara walilazimika kuchelewa kwa zaidi ya saa moja katika eno hilo wakati wakienda kazini. Picha na Salim Shao
Muktasari:
Jiji hilo lina ukubwa wa kilomita za mraba 1800 na kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, lina watu wapatao milioni 4.3.
Dar es Salaam ni jiji linalotajwa kuwa na pilikapilika nyingi nchini. Ni jiji la kibiashara linaloiunganisha Tanzania na nchi kadhaa barani Afrika na dunia kwa jumla.
Jiji hilo lina ukubwa wa kilomita za mraba 1800 na kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, lina watu wapatao milioni 4.3.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu, pia linayo magari na pikipiki ambavyo havina uwiano katika kuongezeka kwake.
Mwaka 1988 Sensa ya Watu na Makazi ilionyesha kuwa Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na watu 1.3 milioni, mwaka 2002 wakifikia 2.4 milioni.
Licha ya ongezeko hilo kuwa la watu, bado miundombinu yake kwa kiasi kikubwa ni ile ile.
Kwa upande wa magari, jiji hilo limekuwa na idadi kubwa zaidi ya magari inayotajwa kuwa chanzo cha foleni barabarani.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2013, magari madogo 226,806 yaliingizwa nchini na kati ya hayo asilimia 70 yanatumika Dar es Salaam. Taarifa hiyo ilieleza kuwa Watanzania wengi hununua magari madogo yanayokadiriwa kuwa zaidi ya 4,500 kwa mwaka na mengi kati ya hayo hutumika ndani ya jiji hilo.
Pamoja na ukweli huo, tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya miundombinu ya Dar es Salaam, hasa barabara ni ya zamani.
Foleni zilivyobadilisha taratibu za maisha
Kutokuwa na uwiano wa kati ya ongezeko la idadi ya watu, magari na miundombinu kwa kiasi kikubwa kumekuwa kukichangia msongamano na foleni katika barabara mbalimbali za jiji hilo, hata kusababisha watu kubadilisha utaratibu wa maisha yao ya kila siku.
Hakika, utaratibu wa maisha umebadilika na sasa wengi wamepunguza kama siyo kuacha kung’ang’ania shuka kitandani na sasa hali ya foleni inawalazimisha kuamka mapema ili wasichelewe maeneo yao ya kutafuta riziki.
Ndivyo hali ilivyo maeneo mengi jijini humo na sasa vijiwe vya unywaji kahawa na tangawizi vimeshamiri kwa kupata wanywaji wengi na mashabiki wa ‘kupiga stori’ nyakati za alfajiri.
Kushamiri kwa vijiwe hivyo kunatokana na watu kubadili mfumo wao wa maisha kwa kuwahi kutoka nyumbani kukwepa kukumbana na foleni barabarani.
Mitaa inayozunguka soko la Tandika ni mfano wa mabadiliko ya mfumo wa maisha walio katika vikundi wakijadiliana mambo mbalimbali kabla ya kufungua biashara zao.
Kutokana na kuwapo kwa hali ya hewa ya baridi kwa wakati huu, wengi huonekana wakizunguka meza za wauza kahawa na tangawizi wakiwa kwenye mabenchi na kujadili mambo mbalimbali ya kimaisha, ikiwamo soka na siasa
Biashara ya kahawa na tangawizi
Katika mtaa maarufu kwa biashara ya mitumba Tandika Sokoni, watu wengi huzagaa wakiwa katika makundi makundi. Kila kundi lina muuza kahawa au tangawizi akiendelea kuwahudumia wateja wake.
Juma Matimbwa (25) ni mfanyabiashara wa mifuko katika eneo la Tandika, ni miongoni mwa watu hao, anasema kwamba sababu kubwa ya yeye kuwa hapo muda huo ni kuikimbia foleni ya barabarani kutoka Mbagala.
“Muda huu ni saa 11: 30 alfajiri, nipo hapa nami naishi Mbande. Muundo wa kazi yangu unanitaka niwe hapa kabla ya saa mbili ili kuwahudumia wateja wanaofika kufuata mahitaji yao katika eneo hili,” anasema na kuongeza:
“Kimsingi. Mbagala Rangitatu ni eneo korofi, kuna foleni kila siku, hivyo ili kukabiliana na adha hiyo nimejiwekea utaratibu wa kutoka nyumbani kwangu saa kumi na nusu alfajiri na mara nyingi hufika hapa kati ya saa 11:15 au 11:30 alfajiri.”
Tatizo la foleni Dar es Salaam limekuwa likichangiwa na mambo mbalimbali. Mbali ya ukarabati wa barabara kadhaa zinazoingia katikati ya mji, kumekuwapo na ongezeko kubwa la idadi ya watu lisiloendana na uboreshaji wa miondombinu.
Simu za mkononi kujiliwaza
Kutokana na hali ilivyo kwa sasa katika barabara mbalimbali za jiji, si jambo la ajabu kutumia muda wa saa tatu kwenye foleni kwenye safari ya kutoka posta kwenda Tabata.
Farida Jemedari (24), mwanafunzi wa chuo kimoja cha ualimu jijini, anasema kuwa kila siku hutumia usafiri wa daladala kwenda na kurudi chuoni.
“Nikiwa kwenye basi, mara nyingi hutumia muda wangu kupiga stori na wenzangu kupitia mitandao ya facebook, Twitter na instagram. Nikichoshwa na hayo yote naweka ‘headphone’ zangu masikioni, nasikiliza muziki,” anafafanua.
Hili hufanywa na vijana wengi wawapo kwenye magari yaliyo katika foleni, wakati mwingine hata husahau adha inayowakabili kwani hujikuta wakiwa wamezama kwenye kuchati. Msichana huyu huingia chuoni saa mbili asubuhi na kutoka saa tisa. Anasema licha ya utaratibu huo, hali ya usafiri imechangia kubadilisha muda wake wa kuamka.
“Kwa kuwa mazoezi ni sehemu ya maisha yangu, awali nilikuwa naamka saa kumi na moja na nusu, halafu natumia nusu saa kufanya mazoezi kabla ya kujiandaa kwenda shule, lakini ratiba hiyo kwa sasa haina nguvu tena.
Hivyo, ili niwahi shule, nalazimika kuamka saa 11:30, kisha nafanya mazoezi muda wa dakika 30 hadi 45, kabla ya kuanza maandalizi ya kwenda shule. Saa 11:30 uhakikisha nakuwa barabarani kwenda shule, kinyume cha hapo, nitachelewa shule,”anasema.
Kwa wale wanaofanya kazi katikati ya jiji hilo pia huwa na mitindo yao. Wengi wanaowahi kwa kudamka kukwepa foleni, hujikuta hawana kazi za kufanya pia kuishia vijiwe vya kahawa au michezo ya kompyuta na wengine humkumbuka Mungu kwa kwenda kanisani.
Misa za asubuhi
Christina Chacha (48) mkazi wa Kimara anayefanya kazi katika benki moja maarufu katikati ya Dar es Salaam anasema kwamba ratiba yake ya siku huanzia kanisani. “Ninatoka nyumbani kwangu mapema sana. Mara nyingi huwa naingia mjini kabla ya saa 12:00 asubuhi, hulazimika kwenda moja kwa moja kanisani. Hapo husali misa ya asubuhi, kabla ya kuanza mihangaiko yangu,” anafafanua. Anasema, kitendo cha kuingia kanisani humsaidia kutumia muda wake wa ziada vizuri kabla ya kuingia kazini.
Futari kwa mama ntilie
Kwa kawaida foleni hizi huwa ni kwa wakati wa asubuhi na jioni. Hivi sasa ni kipindi cha mfungo wa Ramadhani na nyakati za jioni katika maeneo mengi yenye foleni, wanaume wengi hushindwa kuwahi makwao kufuturu badala yake hujipanga kwenye mikeka ya mama ntilie kwa ajili ya mlo huo maalumu kwa waliofunga.
“Binafsi naona foleni imekuwa ni neema kwangu. Hivi sasa nafanya biashara wakati wa jioni muda wa kufuturu. Wateja wengi hususani wanaume huona bora wale futari na kupumzika hadi itakapopungua, kuliko kukaa kwenye mabasi wakati wa foleni,” anasema Sabina Abdallah (36) anayefanya biashara nyuma ya kituo cha mabasi cha Tazara, Barabara ya Mandela.
Madarasa ya asubuhi
Kwa baadhi ya wanafunzi, foleni imechangia kuwabadilishia utaratibu wa masomo yao. Wako walioamua kuanzisha madarasa ya asubuhi ili kufidia muda wao wa jioni.
“Mara nyingi huwa tunalazimika kuondoka chuoni mapema sana ili kuwahi foleni. Kwa maana hiyo tumekubaliana tufike chuoni mapema na kuanza kipindi saa 12:00 asubuhi,” anaeleza Musa Khalfani wa Mbezi anayesoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania(OUT), Kinondoni.