Walanguzi tisa wa tumbaku mbaroni wakidaiwa kwa wizi

Mabelo ambayo yamelanguliwa na kutoroshwa kutoka kwa wakulima wa Wilaya za Urambo na Sikonge. Picha na Hawa Kimwaga
Muktasari:
- Mkoa wa Tabora unafanya operesheni za mara kwa mara kwa lengo la kudhibiti uhujumu wa zao la tumbaku na kutaka kuona mkulima ananufaika na zao hilo kuu mkoani humo.
Tabora. Watu tisa, wakiwemo raia watatu wa Kenya, wafanyabiashara kutoka wilayani Serengeti mkoani Mara na baadhi ya watumishi wa kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya Global Leaf, wamefikishwa mahakamani kwa kesi ya Uhujumu uchumi, wakituhumiwa kwa ulanguzi na utoroshaji wa mabelo 452 ya tumbaku.
Washtakiwa hao katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 11376 ya mwaka 2025 ni Emmanuel Omahe Gesamba, Joel Chacha Keraryo, Sadick Mhamudu Ally, Omari Hassan Kangele, Jacinta Mwita Mwise, Flora Vicent Masegese, Juma Hamad Haganga, Ramadhani Yasin Makula na Louis Vedastus Ngaiza.
Wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tabora, leo Jumatatu Mei 13, 2025 na kusomewa jumla ya mashtaka 15 mbele ya Hakimu Demetrio Nyakunga.
Kati ya mashtaka hayo 13 ni ya uhujumu uchumi na mashtaka mawili ya ulanguzi na uchepushaji wa tumbaku na matumizi mabaya ya madaraka,

Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha akizungumza wakati akikagua mabelo yaliyohifadhiwa ndani ya godauni la Global Leaf lililopo kata ya Cheyo manispaa ya Tabora. Picha na Hawa Kimwaga
Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Merito Ukongoji, akisaidiwa na Wakili Mwananidi Mbuhuni, amesema kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo
katika wilaya za Sikonge na Urambo, Mkoa wa Tabora.
Amesema mabelo hayo waliyokamatwa nayo washtakiwa wote Yana jumla ya Sh180 milioni kwa pamoja, Mei 6, 2025, katika Manispaa ya Tabora.
Wakili Ukongoji amesema kuwa washtakiwa hao wametenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 312(1)(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya Mwaka 2022.
Amesema kuwa pia washtakiwa hao wametends makosa hayo kinyume na kifungu cha 57(1), Kifungu cha 60(2), na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (marejeo ya mwaka 2022), pamoja na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kwa kuwa mahakama ya wilaya haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi ya aina hiyo kwa hatua ya sasa, watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kuhusu mashtaka hayo.
Wakili Ukongoji alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Nyakunga amepanga kesi hiyo itatajwa mahakamani hapo Mei 27, 2025 na ameamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu mpaka tarehe hiyo, kutokana na kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.
Katika kesi hiyo washtakiwa hao wamewakilishwa na mawakili Kanani Chombala na Saikon Nakoren.
Awali kabla ya watuhumiwa kupandishwa kizimbani, Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tabora, Mathias Ndege amewaeleza waandishi wa habari kuwa mazao hayo yalichukuliwa moja kwa moja kutoka kwa wakulima bila kupitia katika masoko rasmi yaliyoidhinishwa na Serikali.
Hivyo, amesema kuwa utaratibu huo ni ukiukwaji wa taratibu za soko la tumbaku nchini.
Amesema uchunguzi wao umebaini kuwa baadhi ya walanguzi kutoka Serengeti walishirikiana na baadhi ya vyama vya msingi na wakulima katika kununua tumbaku kwa bei ya chini, na kisha kuisafirisha kwa ajili ya kuuza kwa bei ya juu sehemu nyingine.
“Walanguzi hawa wamekuwa wakifika moja kwa moja kwa wakulima, wakipatania bei ndogo na kuinunua tumbaku hiyo, ambayo wao huenda kuuza kwa faida kubwa nje ya mfumo rasmi,” amesema Ndege.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Matiko Chacha, ameeleza kuwa serikali ya mkoa haitavumilia wala kufumbia macho vitendo vya ulanguzi na utoroshaji wa tumbaku, kwani vinaathiri juhudi za serikali kuinua uchumi wa wananchi wake, hususan wakulima wa zao hilo.
“Haiwezekani serikali inapambana kuinua maisha ya wananchi, halafu watu wachache wanajitokeza kwa maslahi yao binafsi na kuhujumu jitihada hizo. Sisi kama Serikali ya mkoa tumejipanga kuhakikisha hili halitokei tena,” amesema Chacha.

Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Tabora ikikagua mabelo ya Tumbaku yaliyotoroshwa kutoka kwa wakulima. Picha na Hawa Kimwaga
Tukio hilo limeibua tahadhari kuhusu ulinzi wa masoko ya mazao ya wakulima na umuhimu wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa sera za kilimo na masoko ili kuhakikisha wakulima wanapata haki yao stahiki na nchi inanufaika na rasilimali zake.