Wakulima marufuku kuuza mashamba ya chai

Ofisa mradi mwandamizi wa Shirika la IDH, Michael Joseph, akionyesha namna bora ya uchumaji wa majani ya chai maarufu “Majani mawili sindano moja ”kwenye moja ya shamba Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuelezwa kukithiri kwa tabia ya baadhi ya wakulima kushindwa kuyaendeleza na badala yake kuyauza kwa lengo la kubadili matumizi hususan kwa mazao mengine.
Rungwe. Serikali Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya imepiga marufuku wakulima kuacha mara moja tabia ya kuuza mashamba yenye miche ya zao hilo na badala yake yaendelezwa kwa kuyatunza na kuzingatia elimu ya wataalamu wa kilimo.
Ofisa Tarafa Wilaya ya Rungwe mkoani hapa, Amimu Mwandelile amesema leo Jumamosi Septemba 2, 2023 ikiwa ni Siku ya kuhitimisha mafunzo ya mwaka mmoja kwa wakulima wa chai 3,792 kati ya 6,162 walionufaika katika Mikoa ya Njombe na Iringa.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Shirika la IDH kupitia mradi wa Agriconnect Boresha Chai kwa ufadhiri wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Amesema kuna baadhi ya vijijii kumeibuka tabia ya wakulima kujihusisha na tabia ya kuuza mashamba pindi wanaposhindwa kuyahudumia jambo ambalo siyo salama kwa mipango mikakati ya Serikali katika kuendeleza kilimo cha chai wilayani humo.
“Nitumie hadhara hii kuwataka wakulima kuacha mara moja tabia hiyo na badala yake watumieni wataalam wa kilimo kupata elimu na kuyaendeleza ili yalete tija kwani chai kwa miaka ya sasa ni dhahabu kwa wanarungwe,” amesema.
Aidha amewataka wakulima kujitokeza kwa ajili ya kujiandikisha katika mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo za ruzuku ambazo zinaanza kutolewa na Serikali hivi karibuni kwa lengo la kungeza tija ya uzalishaji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Busokelo, Anyosisye Njobelo amesema kitendo cha uuzwaji wa mashamba kimekithiri na kwamba utafika wakati Serikali kutunga sheria za kuwabana wananchi.
“Suala hili tunaomba wananchi muache kwani ardhi ni mali ya Serikali kitendo cha kujimegea na kuuza hakikubaliki ufike wakati zingatieni sheria za nchi ili kupunguza migogoro isiyo na tija,” amesema.
Ofisa Mwandamizi wa Shirika la IDH, Michael Joseph amesema mradi huo wa mwaka mmoja umenufaisha wakulima 6,162 katika Mikoa ya Mbeya, Njombe la Iringa na malengo katika awamu ya pili mpaka ya nne ni kufikia wakulima wengi zaidi.
Amesema lengo kubwa ni kuongeza thamani ya zao la chai sambamba na kuwepo kwa mifumo mizuri ya upatikanaji wa mbolea, mashine za kuchumia ili kuwapunguzia wakulima hadha ya kutumia nguvu nyingi katika uzalishaji.
“Katika kuhakikisha wakulima wanafanikiwa na kuongeza uzalishaji wa majani ya chai tunatarajia kutoa miche 1.7 milioni kwa Mikoa ambayo imepitiwa na mradi wa shamba darasa lengo ni kuona wanaziba mapengo ya miche ambayo iliharibiwa katika msimu wa kilimo uliopita,” amesema.
Amesema pia wametoa ruzuku ya mashine za kisasa za kuchumia majani ya chai kupitia vyama vya msingi vya wakulima (Amcos) ili viweze kujiendesha na kusaidia wakulima kuondokana na changamoto za kutumia muda mwingi mashambani kuchuma au kuhudumia chai.
Mtendaji Mkuu wa Wakulima Wadogo wa Chai Rungwe na Busokelo (RBTC-JE), Lebi Gabriel amesema kwa msimu huu wa kilimo wanatarajia kupokea mifuko 20,000 ya mbolea ya ruzuku kutoka Serikalini.
“Msimu huu hakuna changamoto kama za mwaka niwasihi kujipanga kuzalisha kwa tija tayari Serikali yetu imeweka mambo sawa kuhusu suala la fedha tayari tumezungumza na baadhi ya mabenki kuona namna ya kutuwezesha katika msimu huu,” amesema.
Mkulima Bupe Mwalonde ameliomba Shirika la IDH kuendelea kufadhiri elimu kwa wakulima kutokana na awamu hii ya kwanza mwamko wa vijana na wanawake kuwa mkubwa.