Wachimbaji wa jasi walia gharama kubwa za uendeshaji

Baadhi ya wadau wakiwa kwenye mkutano wa madini ya viwandani mkoani Kilimanjaro
Muktasari:
- Waomba bei ipandishwe kuwafuta machozi wachimbaji hao wa madini ya jasi, ambao wanadai bei kwa sasa ni changamoto na wanahitaji iongezeke ili kuendana na gharama halisi za uendeshaji.
Same. Wachimbaji na wasambazaji wa madini ya jasi katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuridhia kupandishwa kwa bei ya madini hayo kutoka Sh65,000 hadi Sh87,600 kwa tani moja, wakidai kuwa bei ya sasa hairidhishi na haitoshelezi gharama halisi za uzalishaji.
Maombi hayo yametolewa katika mkutano wa wadau wa madini ya viwandani uliofanyika mkoani humo, uliowakutanisha wachimbaji, wasambazaji, wawakilishi wa viwanda pamoja na maofisa wa Serikali.
Wadau hao wamedai kuwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi zimeongezeka kwa kiasi kikubwa, huku bei ya madini hayo ikibaki chini kwa muda mrefu, jambo linalowavunja moyo na kuathiri uendelevu wa shughuli zao.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Mbwambo, amesema kuwa licha ya Jasi kuwa na soko katika viwanda vingi vya saruji na bidhaa nyingine, wachimbaji bado hawafaidiki ipasavyo kutokana na bei ndogo sokoni.
“Kwa sasa bei iliyopo ni Shilingi 65,000 kwa tani moja, ikiwa ni pamoja na gharama za usafiri, jambo ambalo halina uhalisia wa kiuchumi. Tumefanya tathmini kama chama na kupendekeza bei ipandishwe hadi Shilingi 87,600 kwa tani ili kuendana na hali halisi ya gharama za uzalishaji,” amesema Mbwambo.

Baadhi ya wadau wakiwa kwenye mkutano wa wadau wa madini ya viwandani mkoani Kilimanjaro
Mbwambo ameongeza kuwa kupanda kwa bei kutawawezesha wachimbaji kugharamia pia shughuli za kurekebisha mazingira kama vile kufukia mashimo yanayosalia baada ya uchimbaji, kazi ambayo kwa sasa hufanyika kwa kusuasua kutokana na ukosefu wa fedha.
Mchimbaji mwingine, Saum Mshana, amesema changamoto zinazowakabili hazihusiani tu na bei ndogo ya madini, bali pia na miundombinu duni, hasa barabara mbovu zinazoelekea migodini.
“Tunalipa ushuru wa Shilingi 30,000 kwa kila gari, lakini barabara zetu ni mbaya sana. Mvua ziliharibu kabisa barabara, lakini hakuna jitihada za kurekebisha,” amesema.
Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Madaha amesema lengo la mkutano huo ni kuweka mazingira bora ya kazi kwa wachimbaji na kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakuwa endelevu.
Amesema suala la bei elekezi linapaswa kushirikisha pande zote; wachimbaji, wafanyabiashara na viwanda. Alitoa muda hadi Juni 15, 2025 kwa viwanda kuwasilisha hoja zao kuhusu pendekezo hilo la kupandisha bei.
“Wadau wamekubaliana kuwa gharama za uendeshaji ni kubwa, hivyo bei lazima iongezwe ili nao waweze kunufaika na shughuli wanazofanya,” amesema Madaha.
Ameongeza kuwa mchango wa wachimbaji pia unahitajika katika kurekebisha maeneo yaliyoharibiwa kimazingira, na kwamba mipango inawekwa ili kila mnunuzi achangie mfuko wa urekebishaji mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amewataka wachimbaji kuhakikisha wanaziba mashimo yote baada ya uchimbaji ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na hatari ya mmomonyoko wa ardhi.
Pia, amesisitiza umuhimu wa wachimbaji kufuata sheria na kujitambulisha kwa viongozi wa maeneo husika kabla ya kuanza kazi.
Katika mkutano huo, wadau wamesisitiza pia umuhimu wa ushirikiano kati ya wachimbaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na halmashauri ili kuhakikisha tozo na ushuru unawekwa kwa kuzingatia hali halisi ya sekta, kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya biashara.