Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge: Kilimo ikolojia suluhisho kwa mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:

  • Profesa Ndakidemi amesema kilimo ikolojia kikipewa msukumu wa pamoja kati ya Serikali, wakulima na wadau kitasaidia kurutubisha udongo na kurejesha rutuba kwa mazao ya wakulima.

Dodoma. Wadau wa sekta ya kilimo nchini, wakiwemo wabunge, wakulima na taasisi zisizo za kiserikali, wametoa wito kwa Serikali kuongeza uwekezaji katika kilimo ikolojia, wakisisitiza kuwa mfumo huu ni suluhisho la kudumu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula kwa taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Mei 3, 2025 wakati wa mkutano kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na wakulima washauri kutoka mikoa ya Dodoma na Singida, uliofanyika kwa usimamizi wa shirika la ActionAid Tanzania kupitia Mpango Mkakati wa Kilimo Ikolojia.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Aloyce Ndakidemi, amesema hali ya hewa isiyotabirika pamoja na udongo kuchoka ni changamoto zinazohitaji majawabu endelevu, na kilimo ikolojia ni njia mojawapo ya kuhakikisha wakulima wanapata mavuno ya uhakika bila kuathiri mazingira.

 “Kwa sasa hatuna budi kuwekeza kwenye kilimo ikolojia. Huu ni mfumo wa kilimo unaoendana na mazingira ya wakulima wetu na unahakikisha udongo unapata rutuba ya asili, huku tukilinda vyanzo vya maji na afya ya jamii zetu,” amesema Profesa Ndakidemi.

Amesisitiza kuwa wakulima wana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na hivyo wanastahili kusikilizwa, kusaidiwa na kuwezeshwa ili waweze kuzalisha kwa tija.

"Kwa hali ilivyo sasa, hakuna njia mbadala. Tunahitaji kusukuma kwa pamoja, Serikali, wakulima na wadau  ili kuleta mapinduzi kupitia kilimo ikolojia," amesema Profesa Ndakidemi.

Profesa huyo, ambaye ni mbobezi katika taaluma ya kilimo na ufundishaji wa wataalamu wa sekta hiyo, amesitiza kuwa wakulima wana nafasi kubwa ya kuujenga uchumi wa nchi, lakini wanahitaji kusikilizwa na kusaidiwa katika changamoto wanazokumbana nazo.

"Moja ya mambo ninayoona ni namna ambavyo mara nyingi watunga sera hawawasikilizi wakulima. Tunawapuuza au kuwahisi hawajui, lakini ukweli ni kwamba wana maarifa mengi ya thamani yanayoweza kutuongoza," ameongeza.

Akigusia suala la matumizi ya mbegu, Profesa Ndakidemi amesema kuwa ingawa mbegu za asili ni muhimu kwa kulinda mazingira, wakulima pia wanapaswa kuchanganya na mbegu za kisasa ili kuongeza kipato na tija.

Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala, ameisitiza umuhimu wa kutumia mbegu sahihi katika mfumo wa kilimo ikolojia, akitolea mfano wa wakulima waliopata hasara msimu wa mwaka 2023/24 baada ya kutumia mbegu za alizeti zisizo na ubora.

Awali, akiwasilisha maoni ya wakulima, Janeth Nyamayahasi ameomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, mbegu, viuatilifu na pia kusaidia gharama za urasimishaji wa kilimo ikolojia.

Nyamayahasiamesisitiza haja ya kuingiza mitaala ya kilimo ikolojia katika mfumo wa elimu kutoka shule ya msingi hadi vyuo vikuu.

"Kama ambavyo kahawa, parachichi, pamba, viungo na kokoa vimepewa msukumo kwenye elimu, basi hata kilimo ikolojia kinafaa kuingizwa rasmi kwenye mitaala," amesema Nyamayahasi.

Aidha, ametaka utekelezaji wa Mkataba wa Afrika Mashariki kuhusu Viwango vya Bidhaa za Kilimo Hai (EAC Organic Product Standard) upewe kipaumbele, ili kuhakikisha bidhaa za kilimo ikolojia zinakuwa na soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Katika hitimisho la wasilisho lake, Nyamayahasi ameiomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku ya kilimo ikolojia zitakazosaidia wakulima kupata mikopo nafuu ya muda mrefu kwa ajili ya mbegu, pembejeo na kuhakikisha usalama wa chakula kwa kizazi cha sasa na kijacho.