Vijana wataja vita Ukraine kukosa soko pilipili kichaa

Muktasari:

  • Vijana 400 kati ya 1,200 kutoka wilayani Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza waliwezeshwa kulima pilipili kichaa kupitia mradi wa 'Vijana Maisha na Kazi' unaotekelezwa chini ya Chama cha Wakulima wa Matunda na Mbogamboga Tanzania (Taha).

Mwanza. Wakulima wa mazao ya bustani na mbogamboga wameiomba Serikali na wadau kutafuta soko mbadala la zao la pilipili kichaa ili kuacha kutegemea soko la nje ambalo limetetereka kutokana na uwepo wa vita ya Ukraine na Urusi.

Wito huo umetolewa leo Machi 15, 2023 na vijana 400 kutoka wilayani Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza ambao ni waathirika wa vita hiyo baada ya mavuno yao kukosa soko la uhakika kufuatia uwepo wa vita hiyo.

Vijana hao ambao ni wanufaika na mradi wa miaka mitatu 'Vijana Maisha na Kazi' unaotekelezwa na Chama cha Wakulima wa Matunda na Mbogamboga Tanzania (Taha) wamesema soko la zao hilo liko nchini Ukraine na Uturuki huku wakidokeza kuwa tangu mwaka 2022, limeyumba kutokana na vita inayoendelea katika nchi ya Ukraine.

Mkulima wa Pilipili Kichaa, Frank James amesema kabla ya vita hiyo kilo moja ya pilipili hiyo iliuzwa Sh8,000 lakini tangu mwaka jana bei ya kilo imeshuka hadi Sh 4,500 kwa pilipili daraja la C, na Sh6,500 (daraja B).

"Tukiwa na soko mbadala hata tukilima tutakuwa na uhakika wa mahala pa kuuza mazao yetu tofauti na kutegemea zaidi nje kwa sababu mnunuzi aliyepo kwa sasa ananunua na kupeleka Uganda ili yachakatwe na kusafirisha kwenda Ukraine na Uturuki," amesema James ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mkulima mwingine, Rashid Sukwa amesema baadhi ya vikundi vya wakulima katika kata hiyo katika kata ya Bugogwa wilayani Ilemela baada ya kuzalisha zao hilo vilikosa mnunuzi jambo lililoilazimu Taha kuingilia kati kwa kumlazimisha mnunuzi (kampuni ya Vitese) kulipa fidia ya gharama za uzalishaji kwa wakulima ambao walikuwa wameshaingia makubaliano ya kumuuzia.

"Mimi ni Afisa Kilimo kata ya Bugogwa, kuna kikundi cha Jikwamue kilivuna magunia manne lakini mnunuzi hakuchukua kama ilivyotarajiwa na bidhaa hiyo ipo tu ndani baada ya mnunuzi wa kupeleka soko la nje kukosekana kutokana na vita inayoendelea. Bahati nzuri Taha wameingilia kati wamembana mnunuzi amerudisha gharama za uzalishaji," amesema

Hata hivyo, Afisa Maendeleo ya Biashara kutoka TAHA, Asia Barnabas amesema wakati wanatambulisha zao hilo nchini kupitia mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh300 milioni, lilikuwa na tija ambayo imepungua kutokana na vita ya Ukraine na Urusi huku kukiwa hakuna soko la uhakika nchini.

Katika kuhakikisha wakulima hawakati tamaa kuzalisha zao hilo, Asia amesema wakulima wamelipwa fidia ya gharama waliyotumia kuzalisha zao hilo huku mbadala wa soko la zao hilo ukitafutwa.

"Tumeona kuna haja ya kuwa na mnunuzi na soko mbadala ili ikitokea shida wakulima wasihangaike. Ieleweke kwamba watumiaji wengi wa pilipili kichaa ni watu wa mataifa ya Ulaya ikiwemo Ukraine na Uturuki," amesema Asia.

Naye, Meneja wa Plan International mkoa wa Mwanza, Majani Rwambali ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hiyo kimeanzishwa kitengo katika Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) kwa vijana kupata ujuzi wa namna ya kuongeza thamani katika zao hilo bure na kukopeshwa mitaji.