Ufugaji wa kambale unalipa

Muktasari:
Samaki hawa unaweza kusikia wakitajwa kwa majina mengine kama vile, kambale channel, koleo, samaki kidevu na mengineyo
Kambale ni aina ya samaki ambao wana majina mengi kulingana na eneo na jamii husika.
Samaki hawa unaweza kusikia wakitajwa kwa majina mengine kama vile, kambale channel, koleo, samaki kidevu na mengineyo
Asili ya samaki hawa ni Amerika ya Kaskazini. Samaki hawa hukua kwa haraka sana na kuwa na uzito mkubwa.
Aina hii ya samaki hupendwa na watu wengi kwa kuwa nyama yake ina ladha nzuri na ni laini.
Samaki hawa huzaliana vizuri zaidi wanapokuwa mtoni au sehemu ambayo wanapata tope.
Mfugaji anapokusudia kufuga aina hii ya samaki kibiashara, ni lazima asakafie bwawa ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababishwa na samaki.
Samaki aina ya kambale wana umbo refu, mpana kuanzia shingoni, ingawa kichwa ni kidogo, na upande wa mkia ni mwembamba. Wana rangi ya kijivu na wengine nyeusi.
Unaweza kulisha kambale kwa kutumia unga wa samaki, maharagwe yaliyosagwa, mahindi, mchele pumba, ngano na bidhaa nyingine. Unaweza kujenga mfumo ambao utawawezesha samaki hawa kupata aina mbalimbali za wadudu, pamoja na majani, ili kusaidia wapate mlo kamili.
Aina hii ya samaki, wakitunzwa vizuri, wanaweza kukua kwa haraka na kuwa na uzito mzuri unaoweza kumpatia mfugaji faida nzuri. Unaweza kuanza kuvuna kambale baada ya miezi sita tangu walipopandikizwa kwenye bwawa.
Fikiria soko
Wafugaji wengi, wamekuwa wakianzisha miradi ya ufugaji wa samaki kwa kufuata mkumbo bila kutambua kwanza soko watakalozalishia samaki hao.
Jambo hili huwafanya wafugaji kuwa na kipato kidogo tofauti na nguvu waliyotumia kuzalisha.
Inapofikia wakati wa kuvuna samaki, kiasi kikubwa huuzwa papo hapo bila kufika kwenye soko halisi, jambo linalosababisha kipato kuwa duni.
Ni vyema mfugaji akawa na soko maalumu ambalo atazalishia. Unaweza kuzalisha kwa ajili ya shule, hospitali, vyuo, taasisi fulani au jamii inayokuzunguka.
Zingatia haya
Kabla hujajikita katika ufugaji, fahamu ni aina gani ya samaki inayopendwa zaidi katika eneo ulipo na kiwango chao cha ukubwa. Tambua kipindi kizuri cha kuvuna ili iwe rahisi kwako kuuza kwa soko zuri.
Wasikilize wateja
Wakati wote mfugaji anapouza samaki, ni lazima kusikiliza kwa umakini, wateja wako wanasemaje. Je, wanapendelea samaki unaouza, samaki wako ni wadogo sana au ni wakubwa sana. Je, wanapendelea uzalishe zaidi? Je, kuna wafanyabiashara wanataka uzalishe zaidi ili nao wanunue na wanataka samaki wawe kwenye ubora gani.
Fuata haya kwa ufanisi wa soko
Hakikisha samaki wako katika hali ya usafi na vyombo salama unapovua tayari kwa kupeleka sokoni.
Samaki ni bidhaa inayoharibika kwa haraka, hivyo hakikisha unawapeleka sokoni mara tu baada ya kuwavua.
Hakikisha gharama za usafiri, utunzaji na uhifadhi, zinalipwa kutokana na bei ya soko.
Kumbuka gharama za uhifadhi wa bidhaa inayoharibika haraka kama samaki ni kubwa, hivyo vua kwa awamu kulingana na mahitaji.
Unaweza kuongeza thamani ya samaki kwa kufanya mambo ya msingi yanayohitajika kwenye uandaaji wa samaki, kama vile kuparua na kutumbua.
Unaweza kuwasafisha na pia kuwakaanga kulingana na soko husika.
Kwa kuzingatia mambo hayo machache, mfugaji anaweza kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza kwenye mradi wa ufugaji wa samaki.
Pia ni muhimu kuzingatia mahitaji muhimu ya ufugaji wa samaki, ili kuepuka gharama zisizo za lazima.
Mwandishi wa makala haya anapatika kwa simu 0718 986 328. Makala haya awali yalitoka kwenye jarida la mkulima mbunifu. www.mkulimambunifu.org