Tanzania, Zambia kuondoa vikwazo ufanyaji biashara

Muktasari:
- Kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia limefungua milango ya kuongeza biashara baina ya mataifa hayo huku Serikali za nchi zote mbili zikikubaliana kuondoa vikwazo na urasimu ili kukuza biashara na uwekezaji.
Lusaka. Tanzania na Zambia zimekubaliana kuendelea kuondoa vikwazo na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji kufanyika baina ya mataifa hayo yenye uhusiano wa kihistoria.
Makubaliano hayo ni pamoja na kuondoa urasimu, kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara, kuitumia vyema miundombinu inayounganisha nchi hizo na kuruhusu mwingiliano wa watu.
Hayo yamejadiliwa leo mjini Lusaka wakati wa kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia na kwa pamoja wakakubaliana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo.
Makubaliano hayo yamegongelewa msumari na viongozi wa wakuu wa nchi hizo Samia Suluhu Hassan na Hakainde Hichilema walipotuhubia kwenye kongamano hilo.
Akizungumzia hilo Rais Hichilema amesema hakuna sababu ya mataifa hayo kuweka urasimu na vikwazo katika biashara na uwekezaji kwa kuwa maendeleo yanahitaji kwa kiasi kikubwa ushiriki wa sekta binafsi.
“Nimetoka kwenye sekta binafsi nafahamu hizi nchi zina vikwazo vingi kwenye ufanyaji biashara ndiyo maana nasema kwa nafasi niliyonayo sasa tuna kila sababu ya kuviondoa hivyo vikwazo, hilo hatuwezi kufanya peke yetu hivyo tumekubaliana na Rais Samia kushirikiana kuviondoa hasa katika eneo la mpakani kwa kuwa sisi ni ndugu hatupaswi kutengenishwa na mikapa,” amesema.
Amesema Serikali katika nchi zote mbili zinapaswa kuondoa vikwazo vinavyoweza kukwamisha biashara, huku akitaka sekta binafsi kuwa sehemu ya jitihada za kukuza uchumi na siyo kuishia kulaumu.
“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, sasa kama kuna changamoto na hamshiriki katika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi na kuishia kuilaumu Serikali haiwezi kuwa na tija.
“Tunataka ushirikiano wetu kwenye uchumi na biashara uzidi kuimarika maradufu kama ilivuo katika uhusiano wetu, hili ndilo linasababisha tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji,” amesema Hichilema.
Rais huyo amesema ni muhimu kwa Tanzania na Zambia kuwekeza katika maboresho ya reli ya ushirikiano ya Tazara kwa kuwa ina umuhimu mkubwa katika kukuza biashara baina ya nchi hizo ikitegemewa zaidi kwenye usafirishaji wa bidhaa.
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake inafanya kila linalowezekana kusukuma uchumi na hilo linafanyika kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.
Rais Samia alitumia fursa hiyo kuinadi Tanzania na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Zambia kuwekeza nchini humo kwa kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili hiyo.
“Serikali ninayoingoza tuna maono ya kutengeneza uchumi imara na shirikishi kwa Watanzania na wote watakaotaka kuja kuwekeza Tanzania. Ushirikiano huu tunaozidi kuuimarisha kati yetu na Zambia tunaamini utakuwa kichochea katika kusukuma maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa yote mawili,” amesema Rais Samia.
Akizungumzia hatua zinazoendelea kufanyika katika kuweka mazingira bora Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema tangu Agosti mwaka jana baada ya Rais Hichilema kutembelea Tanzania, mawaziri wa kisekta wameshakutana mara kadhaa na wameondoa baadhi ya vikwazo visivyo vya kikodi.
“Kati ya vikwazo 24 tulivyovianisha Serikali zote mbili tayari tumeshaviondoa nane na vilivyosalia tumekubaliana hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu tuwe tumevimaliza vyote na vinavyoendelea kuibuka tutavishughulikia hatua kwa hatua.
Mimi na waziri mwenzangu wa Biashara upande wa Zambia, tuna vikao kwa njia ya mtandao kila wiki na mara moja kwa mwezi tunakutana katika eneo lenye changamoto iwe ni mpakani au kwenye miji mikubwa ambapo biashara zinafanyika iwe kuanzia au kuishia,” amesema Dk Ashatu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay amepongeza hatua ya Rais Samia kuongozana na wafanyabiashara kwenye nchi ambazo wana uhusiano nao wa kibiashara.
“Hatua hii inatufanya sekta binasi tusijione wanyonge, ni mara kadhaa Rais amekuwa akiongozana na sisi katika nchi za kimkakati ambazo tunafanya nao biashara au tunataka kutengeneza mazungungumzo ya kufungua biashara zetu. Mara zote amekuwa akitusikiliza na kuhakikisha kero za kibiashara zipate ufumbuzi.
“Miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto ya Serikali kutoiamini sekta binafsi lakini sasa tunaona mambo yamebadilika. Tunaaminiwa na tunapewa nafasi ya kushirikiana na Serikali kama hivi tunaposhirikishwa kwenye ziara tunapata nafasi ya kuzungumza na wafanyabiashara wa upande mwingine na hata wafanya maamuzi wakiwemo mawaziri,” amesema Lukumay.