Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maeneo saba ya fursa, SGR Tazara sasa yaiva

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni wake Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema alipokuwa akimkabidhi zawadi ya picha kabla ya kuanza mazungumzo Ikulu - Dar es Salaam. Picha na Ikulu

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema na kujadili mambo saba, ikiwemo vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara wadogo na madereva katika mpaka wa Tunduma na Nakonde.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema na kujadili mambo saba, ikiwemo vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara wadogo na madereva katika mpaka wa Tunduma na Nakonde.

Mazungumzo hayo yalifanyika  Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya Rais Hichilema kuwasili nchini kwa ziara ya siku moja kwa mwaliko wa Rais Samia ambapo baada ya mazungumzo yao, walishuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu ya ulinzi, sanaa na utamaduni.

Akizungumzia mambo aliyojadiliana na Rais Hichilema, Rais Samia alisema wameangalia uhusiano wa kisiasa kati ya Tanzania na Zambia na kukubaliana kuendeleza uhusiano huo kama walivyoachiwa na waasisi, Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda.

Pia, alisema wamezungumzia suala la usalama kwa kuzingatia mambo ambayo yanatokea katika ukanda wao kama vile ugaidi.

“Tumezungumza suala la usalama katika nchi zetu, tumeangalia kwenye ukanda huu mambo yanayotokea, ugaidi na mengine, tukasema tuwe na ushirikiano kwenye mambo ya usalama ya nchi zetu,” alisema Rais Samia.

Mkuu huyo wanchi alibainisha kwamba walijadiliana kuhusu miundombinu ya reli ya Tazara pamoja na bomba la mafuta la Tazama na kukubaliana kuboresha miundombinu hiyo ili iwe ya kisasa na ifanye kazi kubwa.

“Leo Tazara haihudumii vema nchi zetu mbili. Tazama pipeline (bomba), lengo lake lililoanzishiwa na inavyofanya leo ni tofauti. Kwa hiyo tumekubaliana tutupe macho huko. Tuiboreshe Tazara, kama tunaifanyia marekebisho reli iliyopo lakini tukakubaliana kwamba kwa dunia ya leo, reli ni SGR.

“Kwa hiyo tumekubaliana kuwa na mradi wa pamoja, tutafute fedha pamoja kupitia PPP (ubia), ushirikiano na sekta binafsi, pengine na wenzetu na marafiki waliotujengea hiyo reli, tuone jinsi tunavyoweza kuiboresha kwenye kiwango cha SGR,” alieleza Rais Samia.

Viongozi hao walijadiliana pia kuhusu vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wafanyabiashara wadogo katika eneo la mpaka wa Tunduma na Nakonde na kuwaagiza mawaziri wanaohusika kukaa na kutafuta namna ya kuwezesha biashara zaidi baina ya nchi hizo.

Alisema kuna vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi vinakwamisha ukuaji wa biashara baina ya Tanzania na Zambia. Hivyo, wamekubaliana kwamba sekta za uwekezaji na biashara na taasisi zinazohusika na ukusanyaji wa mapato zikae pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo.

“Tumewazungumzia wafanyabiashara ndogondogo ambao wanapovuka mpaka wanakabiliwa na masharti makubwa, hasa kwenye vibali vya kuingia nchi nyingine lakini pia tozo wanayotakiwa kulipa ni kubwa.

“Kwa hiyo tumesema mawaziri wetu wakae waangalie jinsi ya kusaidia biashara ziendelee kwenye pande zetu mbili bila matatizo,” alibainisha Rais Samia.

Rais Samia alieleza kwamba walijadiliana pia kuhusu mgogoro wa madereva wa malori ambao umekuwa ukitokea mara kadhaa mpakani Serikali zifanye kazi kwa pamoja kwa kushirikiana na jumuiya za madereva hao.

Kwa upande wake, Rais Hichilema alisema: “Tunatakiwa kuimarisha uhusiano ulioanzishwa na waasisi wetu, ujirani tulionao hatuna sababu ya kutengana. Mipaka ya kijiografia isiwe chanzo cha kutengana.

“Uhusiano wetu ni wa asili, ukienda Tunduma na Nakonda kuna mwingiliano mkubwa kati ya Watanzania na Wazambia. Kama tusipowatengenezea mazingira ya ushirikiano basi watadhuriana,” aliongeza.

Rais Hichilema alisema katika mengi yaliyopo Tanzania nchi yake ingependa kujifunza kwenye sekta ya uchimbaji madini na namna ambavyo Serikali imeweza kuwaratibu wachimbaji wadogo wadogo.

“Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwapanga wachimbaji wadogo kutoka kwenye uchimbaji haramu hadi kufanya shughuli zao kwa halali, kwa kuwapatia leseni. Timu yangu itakaa chini na wenzetu wa wizara ya madini waweze kujifunza kilichofanyika ili na sisi tukafanyie kazi.Tujifunze jinsi ya kuyafanyia kazi haya tuliyokubaliana kwa pamoja, hakuna sababu ya Zambia na Tanzania kutengana,” alisema.