Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Tuache mzaha, hiki si kizazi cha kupewa ahadi hewa majukwaani

Muktasari:

Tumebakiza siku 110 kama uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 26,2025, lakini tunashuhudia baadhi viongozi wa vyama vya upinzani na watia nia, wakitoa ahadi zisizotekelezeka hadi unajiuliza wanawachukuliaje Watanzania wa kizazi cha sasa.

Tumebakiza siku 110 kama uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 26,2025, lakini tunashuhudia baadhi viongozi wa vyama vya upinzani na watia nia, wakitoa ahadi zisizotekelezeka hadi unajiuliza wanawachukuliaje Watanzania wa kizazi cha sasa.

Niwatahadharishe tu, baadhi ya ahadi zinazotolewa na makada wenu, iwe majukwaani au kupitia vyombo vya habari zinawashushia hadhi na heshima mbele ya wapigakura, na kuwachukulia kama ni ahadi za matusi kwa Watanzania.

Mtambue kiwango cha uelewa (literacy rate) cha Watanzania hawa mnaowapa ahadi ambazo hata mtoto mdogo anajua ni uongo ni zaidi ya asilimia 83 kulinganisha na asilimia 23 wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961.

Muelewe hadi kufikia 2025, Tanzania tuna vyuo vikuu takriban 50, achilia vyuo vya kati ambavyo vinamwaga wahitimu mitaani na pia hakuna mtoto anayeishia darasa la saba, hivyo mnapotoa ahadi zenu muelewe Watanzania si wajinga.

Nataka niwatahadharishe kuwa Watanzania wa leo wana uwezo na maarifa ya kuchambua mambo au kwa maneno mengine wanajua mchele ni upi na chuya ni zipi katika ahadi hizo mnazotoa mkifikiri ni kama mnaahidi pipi kwa mtoto.

Toeni ahadi zenye uhalisia kupitia ilani za uchaguzi kama ambavyo Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa ilani yake ya maandishi (written) kwa ajili ya 2025-2030 na ninatarajia kuona vyama vyote 19 vinavyoshiriki uchaguzi vikitoa ilani zao.

Katika uchaguzi mkuu 2020, nilibahatika kuona ilani za uchaguzi zilizoandikwa za CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi CUF, NCCR-Mageuzi na Chama cha Sauti ya Umma (SAU).

Vyama vingine vilitamka tu ilani zao pasipo maandishi yoyote kupitia majukwaa katika mikutano ya hadhara ya kampeni japo sio vyote.

Hawa ambao ilani zao ni vinywa vyao majukwaani, ndio wale wanatamka ahadi bila tafakari yoyote na kwa mambo yasiyowezekana kulingana na uwezo wa kiuchumi wa Taifa letu, halafu bado wanataka tuwaone wapo makini na nchi yetu.

Athari ya kuwa na ilani ya ‘mdomo’ ni kwamba hata hao wenyewe wanaozitoa hawawezi kuzikumbuka zote pindi wanapopewa ridhaa ya kuongoza Dola, wala wapigakura hawawezi kuwa na nyaraka ya kufanya rejea kile walichoahidiwa.

Ilani ya uchaguzi ni hati iliyochapishwa na chama cha siasa kabla ya uchaguzi, inayoeleza sera na ahadi ambazo watazitekeleza wakichaguliwa na inatumika kama tangazo la umma inayolenga kuwashawishi wapigakura kukiunga mkono.

Kwa maneno mengine, ilani ya uchaguzi ni waraka unaoeleza maono, sera na ahadi za chama cha siasa kwa siku zijazo na ni chombo muhimu kwa wapigakura kuelewa ni nini chama kinasimamia na kile wanachokusudia kufikia kikichaguliwa.

Kama nilivyosema, ilani ni chombo muhimu sana huandikwa ili ziwe za kushawishi, zikiangazia sera muhimu na kurudia ujumbe muhimu ili kuwavutia wapigakura lakini pia zinatumika kama msingi wa kuiwajibisha Serikali iliyochaguliwa kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao baada ya uchaguzi.

Tumeona CCM katika ilani yao ya maandishi kwa ajili ya uchaguzi ya 2025-2030 imebeba malengo makuu manane ambayo ni pamoja na kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa kuziongezea thamani rasilimali zinazozalishwa hapa Tanzania.

Malengo mengine ni kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umaskini, kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii na kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

Imelenga kukuza na kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii, kudumisha demokrasia na utawala bora, kudumisha amani na utulivu na kudumisha utamaduni wa Taifa na kukuza sanaa na michezo.

Sasa ukitizama kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za mwaka 2025 ambazo zimetengenezwa chini ya kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya Mwaka 2024, zimetiwa saini na vyama vya siasa 18, sisi kama umma tunahitaji ilani zao za uchaguzi.

Tunahitaji ilani zao ili tuweze kufanya ulinganisho wa sera na ahadi ili tufanye maamuzi sahihi siku ya kupiga kura itakapofika na tutazisubiri hadi tarehe ambayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), itapuliza kipyenga cha uchaguzi.

John Lewis aliwahi kusema “The vote is precious. It is the most powerful non –violent tool we have in a democratic society and we must use it”, kwamba kura ni thamani isiyohitaji vurugu katika jamii ya kidemokrasia, ni lazima tuitumie.

Lakini Sharon Salzberg naye aliwahi kusisitiza kuwa “voting is the expression of our commitment to ourselves, one another, this country and the world”, kwamba kupiga kura kunadhihirisha wajibu wetu, wa mtu mmojammoja na dunia.

Sasa ili tuitumie hii kura vizuri, ni vyema vyama vya upinzani navyo vikaja na Ilani zao za uchaguzi za 2025-2030 kama baadhi vilivyofanya uchaguzi mkuu 2020 kwa sababu bila hivyo, hadi sasa CCM kinabaki kuwa chama pekee makini zaidi.

Tunataka vyama vyote vya upinzani vilivyosaini maadili ya uchaguzi mkuu, vituonyeshe uhai wake na visiishie kwenye makaratasi, tunatamani kuona ilani zao za uchaguzi 2025-2030 na tuwaone wagombea wao ili kuondoa hisia zilizopo.

Yapo madhara mengi ya kutokuwa na ilani, moja ni wapiga kura watashindwa kujua visheni na sera za chama lakini wapiga kura watashindwa kuwajibisha chama pasipokuwepo ilani ambayo ni mkataba kati ya wapiga kura na watawala.

Lakini chama kisicho na ilani ya uchaguzi kinachukuliwa na wapiga kura kama chama ambacho hakikujiandaa na uchaguzi, lakini kutokuwa na ilani huathiri heshima ya chama na mwisho kitashindwa kuwashawishi wapigakura.

Niviombe sana vyama vya upinzani na viongozi wao, viwazuie watia nia nao katika nafasi mbalimbali kuanzia urais, ubunge na udiwani, kuacha kutoa ahadi za mzahamzaha kwa Watanzania kwa sababu wanajishushia hadhi, heshima na kukubalika.

Mathalan, kitokee chama ambacho kinatuahidi kitajenga bahari Dodoma itakayounganika na bahari ya Hindi, au kwamba kitanunulia walimu wote wa umma karibu 200,000 magari Toyota Spacio na kila gari si chini ya Sh15 milioni.

Kwa sababu kundi hili dogo tu nchi itatumia matrilioni ya shilingi sasa najiuliza kwa nini mgombea utoe ahadi hizi kama za Abunuasi ukijua haziwezekani?

Narudia kuwatahadharisha baadhi ya wagombea, acheni kutoa ahadi za kufikirika kwa Watanzania na kufanya mzaha kana kwamba ni mazwazwa, labda kama mmeingia kwenye uchaguzi kuuza sura na kutengeneza wasifu.

Lakini kwa chama kilicho makini, hakitamki tu ahadi, bali kinaeleza pia pesa hizo za kufanya hayo mambo makubwa hivyo watazitoa wapi kwa uchumi gani tulionao na kwa nini wabague makundi ya kuwapa maisha manono.

Kama unataka kutoa ahadi ya masilahi bora ya watumishi na wafanyakazi basi chukua idadi ya wafanyakazi na watumishi wote, tuambie unataka masilahi yao yawe hivi, yatagharimu nchi kiasi gani na fedha hizo zitatoka wapi.

Kwa hiyo tuache kuwadhihaki Watanzania kwa kutoa ahadi za kisanii, hiki kizazi ni tofauti kabisa na kile cha zidumu fikra za wenyekiti, hiki cha sasa kina uwezo wa kuchambua, kupima na kufanya hitimisho la kauli yako.

0656600900