Tanzania, Zambia kuimarisha ushirikiano wa masoko ya mitaji

Muktasari:
- Tanzania na Zambia zinatarajiwa kushirikiana katika mageuzi ya kimfumo, kuimarisha ulinzi wa wawekezaji na kuhakikisha masoko ya mitaji yanakuwa thabiti, ya uwazi na yanayoshirikisha wadau wote.
Dar es Salaam. Nchi za Tanzania na Zambia zimeafikiana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza ujumuishaji wa kiuchumi katika kanda na kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza uwekezaji, kuboresha mifumo ya udhibiti, pamoja na kuimarisha utaratibu wa usuluhishi wa migogoro kupitia mabaraza ya masoko ya mitaji ya Tanzania na Zambia.
Mpango huu unaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mara kadhaa amesisitiza umuhimu wa masoko ya mitaji kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), jana ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Dk Ntemi Kilekamajenga, upo nchini Zambia kwa ziara ya mafunzo ya siku tano kuanzia Juni 16 hadi 20, 2025.
Ziara hiyo inahusisha pia mazungumzo ya ngazi ya juu na taasisi mbalimbali ikiwamo Tume ya Usalama wa Mitaji na Hisa ya Zambia (SEC), Soko la Hisa la Lusaka (LuSE), Chama cha Masoko ya Mitaji Zambia (CMAZ), pamoja na baadhi ya wajumbe wa Mahakama.
Akizungumzia ziara hiyo, Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji, Martin Kilikoli amesema inalenga kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuchambua maeneo yanayohitaji maboresho ya kisheria na kiudhibiti.
“Maeneo muhimu yanayolengwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro, kuimarisha uwazi wa masoko na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta, mambo ambayo ni msingi wa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje,” amesema.
Pia, amesema hatua hiyo inaendana na mkakati wa Serikali wa kuimarisha taasisi za kisheria na kuifanya mifumo ya kifedha kuwa jumuishi na rafiki kwa wawekezaji.
“Masoko ya mitaji madhubuti ni nyenzo muhimu za kuendeleza uchumi jumuishi na endelevu,” amesema Kilikoli.
Ameongeza kuwa, ushiriki wa viongozi waandamizi katika ziara hiyo, unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kukuza ushirikiano wa kikanda na kuimarisha uwezo wa taasisi katika sekta ya masoko ya mitaji.
Kupitia ushirikiano huo, Tanzania na Zambia zinatazamiwa kushirikiana katika mageuzi ya kimfumo, kuboresha ulinzi wa wawekezaji na kuhakikisha masoko yanakuwa imara, wazi na shirikishi.
“Dira yetu ya pamoja ni kuwa na masoko ya mitaji yaliyo wazi, yanayojumuisha kila kundi na yaliyo chini ya usimamizi madhubuti, ili kujenga imani kwa wawekezaji na kuchochea maendeleo ya muda mrefu,” amesisitiza.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Tanzania kujenga uchumi unaojumuisha watu wote na unaotegemea mifumo imara ya kifedha kama msingi wa maendeleo ya kitaifa na kikanda.