Sh63.2 bilioni kuchochea uchumi jumuishi Tanzania

Muktasari:
- Hatua hii ni utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kukuza uchumi kwa kuwawezesha wajasiriamali kuendelea kushiriki kwenye mnyororo wa uchumi jumuishi na kuleta matokeo chanja kwa Tanzania.
Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) imesaini mikataba ya ufadhili yenye thamani ya Sh63.2 bilioni na taasisi tatu za kifedha nchini, ikiwa ni hatua muhimu inayolenga kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi, kupunguza pengo la makazi na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs).
Mikataba hiyo ilisainiwa leo Jumatatu, Juni 23, 2025, wakati wa mkutano wa wadau wa EADB uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Taasisi zilizopokea mikopo hiyo ni Benki ya Maendeleo ya TIB (Sh30 bilioni), Kampuni ya Rehani Tanzania (TMRC) (Sh20 bilioni) na Benki ya Azania Plc (Sh13.2 bilioni).
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Dk Charles Mwamwaja, amesema mikataba hiyo inaendana na vipaumbele vya Serikali vilivyowekwa katika Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26).
“Mikataba hii itachochea ukuaji jumuishi, kuwawezesha wajasiriamali wetu na kuchangia moja kwa moja utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa,” amesema Dk Mwamwaja, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya EADB.
Benki ya TIB itatumia mkopo wake wa Sh30 bilioni kufadhili miradi 20 hadi 25 katika sekta mbalimbali muhimu kama vile viwanda, madini, miundombinu, mali isiyohamishika na utalii—ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2025.
Kwa upande wake, TMRC itatumia Sh20 bilioni hiyo kupanua upatikanaji wa mikopo ya rehani ya muda mrefu kupitia taasisi za msingi za kutoa mikopo ya nyumba, ikiwa ni jitihada za kupunguza uhaba wa makazi nchini.
Benki ya Azania itatumia Sh13.2 bilioni kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika sekta za viwanda, nishati jadidifu, elimu, kilimo na afya. Mikopo hiyo itatolewa kwa fedha za kigeni (dola za Marekani) ili kusaidia upanuzi wa biashara na uboreshaji wa ajira.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EADB, Benard Mono amesisitiza umuhimu wa uvumbuzi katika kutoa majawabu kwa changamoto za kifedha.
“Mandhari ya uchumi wa Tanzania unahitaji suluhu za kifedha zenye ubunifu na uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli kwa jamii na watu mmoja mmoja,” amesema.
Tukio hilo pia lilitumika kuzindua Mpango Mkakati wa EADB wa mwaka 2024–2028 wenye kaulimbiu ‘Let’s Do It’. Mpango huo umejikita katika nguzo tano: kuimarisha matokeo ya maendeleo, kutumia mifumo ya kidijitali, kuendeleza rasilimali watu, kuongeza mwonekano wa taasisi, na kuboresha usimamizi wa hatari.
Mono ameeleza kuwa katika mwaka 2024 pekee, EADB iliweza kuwafikia zaidi ya wajasiriamali wadogo na wa kati 60,000 na kusaidia kuunda ajira zaidi ya 110,000, ambapo ajira 21,000 zilienda kwa wanawake.
Ameongeza kuwa benki hiyo inaendelea kushikilia hadhi ya juu zaidi ya ukadiriaji wa kifedha katika kanda ya Afrika Mashariki, ikiwa na alama ya A kutoka S&P Global Ratings na A3 kutoka Moody’s.
Wadau waliopokea ufadhili kutoka EADB pia walitoa ushuhuda. Mkurugenzi wa Shule za Baobab, Bi Shani Swai, alisema mkopo wa EADB umewezesha ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
“Ushirikiano wetu na EADB umeleta maboresho makubwa ya ubora na upatikanaji wa elimu. Athari zake zinaonekana katika elimu na hata afya,” amesema.
Meneja Fedha wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Adolphe Kasegenya, amesema ufadhili kutoka EADB uliwezesha ujenzi wa nyumba 300 za bei nafuu mjini Dodoma pamoja na utekelezaji wa mradi wa Morocco Square jijini Dar es Salaam.
“Sekta ya makazi huibua minyororo mingi ya thamani, kutoka ujenzi hadi viwandani. Ni injini muhimu ya ukuaji wa uchumi,” amesisitiza.
Mono alieleza kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya EADB katika ukusanyaji wa fedha ni pamoja na mkopo wa dola milioni 40 kutoka OPEC Fund, pamoja na dola milioni 25 kupitia ushirikiano wa kifedha. Pia alibainisha kuwa benki hiyo inaandaa mpango wa kutoa hati fungani zenye kiwango bora cha uwekezaji zitakazopatikana kwa wawekezaji katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Dk Mwamwaja amewataka wadau kutoka sekta ya umma na binafsi kufika katika ofisi za benki hiyo ikiwa wana miradi yenye tija:
“Ikiwa una mradi wenye tija, tembelea ofisi yetu ya nchi. Milango yetu iko wazi,” amesema.
Ameongeza kuwa mikutano kama hiyo pia itafanyika nchini Kenya, Uganda na Rwanda ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na benki hiyo.
“Benki hii ni ya kwetu sote. Tuitumie ipasavyo ili kuinua uchumi wetu,” amesema.