Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

OPEC, EADB kusaidia maendeleo Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Hatua hiyo inakusudia kusaidia biashara za Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs) pamoja na miradi ya miundombinu muhimu katika nchi wanachama wa EADB

Dar es Salaam. Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa wa OPEC na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) wameingia makubaliano wa mkopo wa Dola 40 milioni za Marekani (Sh106.2 bilioni) ili kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu ya kiuchumi Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yaliyofanyika juzi makao makuu ya Mfuko wa OPEC mjini Vienna, Austria yanatajwa kuwa ni makubaliano ya nne na makubwa zaidi kati ya taasisi hizi mbili.

Hatua hiyo inakusudia kusaidia biashara za Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs) pamoja na miradi ya miundombinu muhimu katika nchi wanachama wa EADB, ikionesha dhamira ya pande zote mbili ya kukuza ukuaji endelevu na jumuishi katika eneo hilo.

Akizungumza kwenye hafla ya kusaini makubaliano ya mkopo huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu EADB, Benard Mono amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa muda mrefu akisema utasaidia wananchi kuinuka kiuchumi.

“Makubaliano haya ya nne na mfuko wa OPEC si tu hatua ya kifedha, bali pia ni ushahidi wa imani yetu na maono ya pamoja kuhusu Afrika Mashariki. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, msaada wa Mfuko wa OPEC umeimarisha uwezo wetu wa kufadhili sekta muhimu, kuanzia elimu na utalii hadi usafirishaji na usindikaji wa mazao,”amesema.

 Pia, amesema makubaliano hayo yataimarisha uwezo wa kuwafikia wajasirimali zaidi na kuwekeza kwa nguvu katika miundombinu.

Rais wa Mfuko wa OPEC, Dk Abdulhamid Alkhalifa amesema ushirikiano wetu na EADB unadhihirisha dhamira yetu ya kufanya kazi na taasisi za kifedha za kikanda ili kufikia matokeo endelevu ya maendeleo.

“Kwa kusaidia wajasiriamali na miundombinu katika ukanda wa Afrika Mashariki, tunawekeza moja kwa moja katika uhimilivu wa kiuchumi wa eneo hilo na ustawi wa muda mrefu. Tunajivunia kuimarisha ushirikiano huu na kuhamasisha rasilimali zaidi zitakazoleta mabadiliko muhimu,” amesema Alkhalifa.

 Ushirikiano wa EADB na OPEC ulianza mwaka 2002 na makubaliano ya ufadhili wa Dola 10 milioni yalielekezwa katika sekta za maendeleo za kipaumbele ikiwa ni pamoja na elimu, utalii na usafirishaji.

Ushirikiano huo ulipanuka mwaka 2014 kwa mpango wa Dola 15 milioni uliolenga kuimarisha wajasiriamali, hasa katika sekta za makazi na malazi.

Mnamo mwaka 2020, Dola 20 milioni zaidi zilipatikana ili kuimarisha usindikaji wa mazao na miradi muhimu ya miundombinu.