Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Senene kutegwa na mashine

Muktasari:

  • Serikali imeelezea mafanikio yaliyopatikana Mkoa wa Kagera ikiwemo kufanya utafiti katika uzalishaji wa senene.

Dodoma. Wazalishaji wa senene mkoani Kagera wanatarajiwa kuanza kutumia mashine maalumu za wadudu hao mara baada ya kukamilika kwa utafiti, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika uzalishaji.

Hayo yamesemwa jana Julai Mosi, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa wakati akielezea mafanikio ya minne ya  Serikali ya awamu ya sita.

Mwasa amesema kuwa wameweka nguvu kubwa katika uzalishaji wa senene kwa kufanya utafiti uliobaini kuwa wako watu ambao wamewekeza zaidi ya Sh400 milioni katika shughuli hizo.

“Wameweka hadi Sh400 milioni kwa ajili ya utegaji wa senene. Tumefanya tafiti za kutengeneza mashine za kisasa za kutegea senene sio kutumia bati kubwa ,”amesema.

Amesema wamefanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu senene watakaotegwa na mashine kutokana na nadharia kuwa wanaotengenezwa kiasili ndio watamu.

Mwasa amesema pamoja na hayo Bukoba Mjini wanajenga kituo ambacho kitatumiwa na wanawake wanaofanya shughuli hizo, lengo ni kuboresha biashara hiyo kwa kuhakikisha inakuwa na viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mwasha amesema makusanyo ya ndani ya halmashauri yameongezeka mara mbili kutoka Sh23 bilioni hadi Sh47 bilioni.

Amesema Halmashauri ya Misenyi na ya Muleba zipo katika 10 bora kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato nchini.

Pia, amesema makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa huo umeingia katika tano bora.

“Kwa hiyo tulikuwa tunahitaji kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi na tumeyafanya kwa hiyo hatupo tena kwenye kundi la mikoa maskini, tuko mahali pengine tuko tayari kwa ukaguzi,”amesema.

Amesema wao sio maskini ni matajiri, lakini kilichofanya hali hiyo ni wakazi hao walikuwa hawajafikiwa na masoko yanayowezesha kuuza bidhaa zao kwa bei halisi.

“Tumeweka soko kubwa pale Muleba ili ile ndizi ya Kamachumu tuiuze kwa bei kubwa kwa hiyo tukiuza Sh30,000 na mtu akaja kuuza Sh50,000 tuwe tumegawana,”amesema.

Kwa mujibu wa  takwimu za pato la kila mtu na kila mkoa kwa mwaka 2023, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa 10 iliyo maskini nchini.

Kuhusu ujenzi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kagera, Mwasa amesema unaendelea na umefikia asilimia 70.

“Mwaka huu katika historia ya nchi tunakwenda kufungua kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bukoba, haya ni maendeleo makubwa. Ujenzi uko katika hatua za mwisho kufikia Desemba kitakuwa kimekamilika,” amesema.

Amesema kukamilika kwa chuo hicho  kutamaliza kiu ya wana-Kagera ambao walilazimika kwenda mikoa mingine kutafuta elimu ya chuo kikuu.

Ujenzi huo ulioanza mwaka juzi, utagharimu zaidi ya Sh18 bilioni hadi kukamilika.

Katika hatua nyingine Mwasa amesema wameanza kuwarejesha vijana kwenye kilimo kwa kuanzisha vitalu ambapo kwenye Wilaya ya Muleba wamewawezesha  300 kupatiwa mashamba.

Amesema mwaka huu wameandaa ekari 4,000 za mashamba kwenye Wilaya za Karagwe, Misenyi, Muleba na upandaji utaanza Septemba mwaka huu.

“Hata bodaboda wamehamasika kwenda kulima na tunawatengea eneo la ekari 1,000 kwa ajili yao. Tulifanya nao mijadala na mazungumzo na tuliwaambia ukweli kuwa bodaboda raha yake ukifanya ukiwa kijana lakini mgongo ukichoka unatamani kufanya kazi nje ya kazi hiyo,”amesema.

Amesema vijana wanapatiwa uhakika wa kudumu wa maisha yake na kuwa ekari moja anayopatiwa kila kijana inamwezesha kupata Sh8 milioni kwa kuuza kahawa na Sh4 milioni kwa mazao mengine.

Mwasa amesema mkoa huo umepokea Sh1.131 trilioni kati ya Novemba, 2020 hadi Aprili, 2025 kwa ajili ya maendeleo ya sekta mbalimbali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus amesema baada ya mapumziko wamerejea na programu ya tumewasikia tumewafikia ikilenga kuelezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika mikoa ya Tanzania Bara.