Mtego wa senene kukuza kipato

Muktasari:
- Veta imeanzisha mtego wa kisasa ambao ni rahisi kutengenezwa hata nyumbani na humsaidia mtumiaji kutenganisha senene na wadudu wengine.
Dar es Salaam Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) imetengeneza mashine rafiki kwa mazingira ya kuvunia senene, wadudu wanaothaminiwa na kabila la Wahaya mkoani Kagera, lengo likiwa ni kukuza ajira hasa kwa vijana.
Imeelezwa kuwa, mbinu za jadi zinazotumiwa na jamii za eneo hilo hasa Wahaya zimepitwa na wakati kwa kuwa, husababisha ukataji miti kwa wingi na njia zisizo bora za uvunaji, hali inayopunguza uwezo wa wajasiriamali kupata kipato kutokana na kiwango kidogo cha mavuno.
Ili kukabiliana na hilo, Veta imeanzisha mtego wa kisasa ambao ni rahisi kutengenezwa hata nyumbani na humsaidia mtumiaji kutenganisha senene na wadudu wengine.
Mbinu hiyo inatajwa kuwahakikishia ubora wa juu wa bidhaa na kipato bora kwa wafanyabiashara wadogo.
“Mtego wetu umetengenezwa kwa kuzingatia ulinzi wa mazingira na usalama wa afya. Unazuia wadudu kutoroka na unaweza kufungwa kwa usalama,” amesema mwalimu wa ufundi Lucus Mayala.
Akizungumza leo Julai 2, 2025 na Mwananchi katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), amesema mtego huo hutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi nchini, hivyo kuwapa vijana fursa ya kujifunza ujuzi wa vitendo na kujiajiri badala ya kubaki bila ajira.
Katika hatua nyingine ya kuunga mkono wajasiriamali wadogo na wa kati, Veta pia imeanzisha mashine ya kuchanja na kuchana mbao iliyotengenezwa nchini.
Mbunifu Johnson Hokororo ameeleza kuwa mashine kama hizo kwa kawaida huagizwa kutoka China na huwa ghali sana kwa wajasiriamali wengi wadogo.
“Mashine hii imetengenezwa kwa kutumia vifaa vinavyopatikana hapa nchini, haitumii umeme mwingi na ni nafuu,” amesema.
“Inafaa kutumika katika maeneo mbalimbali, hasa sasa ambapo umeme umefika karibu maeneo yote nchini.”
Hokororo pia amesema kuna ongezeko la hamasa miongoni mwa wafanyabiashara, baadhi tayari wameanza kuweka oda