Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajasiriamali wawasilisha kero zao kwa RC Mwassa

Baadhi ya wajasiliamali Manispaa ya Bukoba wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa (hayuko pichani) alipkutana nao kusikiliza na kufahamu changamoto zao. Picha na Alodia Dominick

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Mkoa wa Kagera (Shiuma, Husna Mohamed, mkoa huo unakadiriwa kuwa na wajasiriamali zaidi ya 100, 000 wanaofanya shughuli za kununua na kuuza bidhaa na huduma mbalimbali kila siku; kundi analosema ni muhimu katika maendeleo na ustawi wa kiuchumi.

Bukoba. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa ameanza vikao vya kimkakati vyenye lengo la kusikiliza, kupokea hoja na maoni ya wadau kuhusu namna ya kuboresha utendaji na hatimaye kufikia maendeleo endelevu ya mkoa huo.

Baada ya kukutana, kuwasikiliza na kutoa maelekezo ya kiutendaji kwa viongozi na wakuu wa taasisi za Serikali mkoani Kagera, Mkuu huyo wa mkoa sasa amezigeukia sekta binafsi ambayo ni moja ya injini ya maendeleo kwa kukutana na wajasiriamali Manispaa ya Bukoba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Mkoa wa Kagera (Shiuma, Husna Mohamed, mkoa huo unakadiriwa kuwa na wajasiriamali zaidi ya 100, 000 wanaofanya shughuli za kununua na kuuza bidhaa na huduma mbalimbali kila siku; kundi analosema ni muhimu katika maendeleo na ustawi wa kiuchumi.

Akiwasilisha hoja na baadhi ya kero za wajasiriamali wadogo na wa kati mkoani Kagera, Joanither Issack, Mama Lishe eneo la Soko Kuu Manispaa ya Bukoba ametaja kukosa mitaji na elimu ya fedha kuwa miongoni mwa changamoto sugu zinazokwamisha maendeleo na ustawi wa wajasiriamali mkoani Kagera.

‘’Hatuna mitaji binafsi na wengi wetu hawakidhi masharti ya mikopo kutoka taasisi za fedha kutokana na kutokuwa na utaratibu wa kuweka kumbukumbu za fedha; hili ni eneo muhimu tunaloiomba Serikali itusaidie, kwanza kwa kupata elimu ya fedha na pili kuwezesha mikopo nafuu,’’ amesema Joanither

Amesema uhakika wa mitaji utaongeza uwezo wa wajasiriamali wa kuuza bidhaa na kutoa huduma na hatimaye kuongeza mzunguko wa fedha na faida pia.

‘’Uhakika wa kipato miongoni mwa wajasiriamali utaongeza hata makusanyo ya Serikali kupitia kodi na ushuru mbalimbali kwa sababu tutakuwa na uwezo wa kulipa,’’ amesema mjasiriamali huyo

Ugumu wa kupata alama na nembo za ubora kutoka taasisi zinazosimamia ubora wa bidhaa na huduma ni eneo lingine lililotajwa na mjasiriamali Paschal Binamungu kuwa kikwazo cha maendeleo yao kiuchumi.

‘’Tunazalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni za maji na za vipande, mafuta ya kula na bidhaa nyingine kadhaa lakini hatuwezi kuziuza katika soko la nje kwa kukosa nemba ya ubora kutoka taasisi husika; tunaoimba Serikali kutusaidia katika eneo hili,’’ amesema Binamungu

Majid Mussa, mmoja wa waendesha pikipiki za abiria maarufu kama Bodaboda ametaja mikataba umiza ya viwango vikubwa vya fedha vya kuwasilisha kwa wamiliki kuwa kero inayostahili kushughulikiwa na Serikali.

‘’Waajiri wetu ambao ni wamiliki wa pikipiki wanataka sehemu kubwa ya mapato kila siku bila kujali mazingira ya biashara, hali inayotufanya wakati mwingine kutumia akiba zetu au kukopa fedha za kuwalipa,’’ amesema Majid

Akizungumza na wajasiriamali hao, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maoni, mapendekezo na hoja zao kuwezesha shughuli zao kukua na kustawi ili wapige hatua kutoka kundi la ujasiriamali hadi kufikia kuwa wafanyabiashara wa kati na wakubwa.

‘’Serikali itahakikisha mnafanya biashara katika mazingira bora na bila vikwazo vyovyote,’’ amesema Mwassa

Amewashauri wajasiriamali hao kuanza utaratibu wa kuweka kumbukumbu zao za fedha kujiongezea sifa za kupata mikopo ya mitaji kutoka taasisi za fedha.

Ametaja kundi la wauza senene kuwa miongoni mwa makundi muhimu yatakayowekewa mikakati maalum ikiwemo kupata njia rahisi ya kukusanya senene wengi bila usumbufu wala kutumia moshi, hali itakayopanua soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi.