Mikopo 'Kimangala' yawaibua BoT Iringa, wananchi waeleza sababu

Muktasari:
- Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo na kuweka mwanga kwa wananchi juu ya mikopo umiza, maarufu 'kimangala' ambayo imekuwa kandamizi kutokana na kulipishwa riba zisizo rasmi.
Iringa. Kufuatia wimbi kubwa la wananchi wa Iringa kukumbwa na changamoto ya mikopo kandamizi maarufu ‘kimangala’, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepiga kambi mkoani hapa kutoa elimu namna ya kuepuka.
Kupitia semina kwa wananchi iliyofanyika leo Jumatano Julai 2, 2025 Manispaa ya Iringa, BoT imewaelimisha wananchi kuelewa masharti ya mkopo, riba husika na umuhimu wa kupata mkataba rasmi kabla ya kukopa, ili kujikinga na madhara ya mikopo yenye riba kubwa na vitisho isivyo halali.
Semina hiyo imekuja baada ya uchunguzi uliofanywa na BoT mwishoni wa Aprili na kubaini mikopo umiza maarufu Kimangala katika mikoa ya Iringa na Njombe kuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo.

Ili kuliwekea msisitizo jambo hilo, Ofisa Sheria Mwandamizi wa BoT, Ramadhani Myonga amesema kuwa kwa mwaka uliopita 2024 ilizifungia taasisi takribani 60 nchini zilizobainika kutoa mikopo isiyo halali, ikiwa ni hatua ya kukomesha ukopeshaji wa mikopo yenye riba kubwa na masharti kandamizi.
"Hakuna sababu ya mwananchi kuendelea kuumizwa na mikopo ya dhuluma ilhali kuna taasisi halali zinazotoa mikopo kwa masharti nafuu na ya haki," amesema Myonga.
Myonga amesema kuwa BoT itaendelea kuwasaka na kuwachukulia hatua wale wote wanaoendesha huduma hizo bila kufuata sheria.
Mchungaji Ombeni Sawike ambaye pia ni mtoa elimu wa huduma za kifedha aliyeidhinishwa na BoT, amesema elimu hiyo ni muhimu kwa wananchi wanaokumbwa na changamoto ya mikopo ya Kimangala.
"Watu wengi hukopa fedha kwa ajili ya matumizi yasiyozalisha, jambo linalowasukuma kushindwa kurejesha na hatimaye kudhulumiwa mali zao," amesema Sawike.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa pembejeo mkoani Iringa, George Kaundama, alipongeza elimu hiyo na kushauri wakopaji wajenge utamaduni wa kusoma mikataba kabla ya kusaini ili kuelewa masharti yote.

"Watu wengi wanasaini mikataba bila kuelewa chochote, hali inayowaletea matatizo baadaye tunaomba msaada," amesema Kaundama.
Naye Alex Maliga, Mfanyabiashara wa bidhaa mbalimbali katika Kata ya Mwangata amesema kuwa mikopo mingi isiyo rasmi imewatesa wafanyabiashara wadogo kutokana na masharti ya ovyo na vitisho.
"Nisema mafunzo ya BoT imekuja wakati mwafaka kuwasaidia kuepuka mitego hiyo," amesema Maliga.
Wananchi wengi walionekana kufurahishwa na elimu hiyo huku wakitoa wito kwa BoT kuendeleza elimu hiyo hadi vijijini ambapo waathirika wa mikopo haramu ni wengi zaidi.