Mambo matano kutikisa mkutano wa ushirika

Mkuu wa Mkoa wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akifungua Benki ya Ushirika Tanzania (CBT), wanaushirika watajifungia kujadili mambo matano.
Dodoma. Mambo matano yatazua mjadala katika kongamano la kitaifa la wanaushirika Tanzania, ikiwemo jinsi ya kuondoa umaskini.
Mengine yatakayojadiliwa ni fursa za uwekezaji katika sekta ya ushirika, kuchochea ukuaji wa uchumi, historia na changamoto za ushirika nchini.
Mbali na hilo, Rais Samia Suluhu Hassan atazindua Benki ya Ushirika Tanzania (CBT) Aprili 28, 2025, jijini Dodoma.
Benki hiyo inaanza kazi ikiwa na mtaji wa Sh55 bilioni, wakati wanaushirika wakimiliki hisa kwa asilimia 51 na wadau wengine, sekta binafsi asilimia 49.
CBT itaanza kufanya kazi katika matawi ya Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara na Tabora.
Akizungumza leo, Aprili 25, 2025, Mkuu wa Mkoa, Rosemary Senyamule amesema wanaushirika hao watakutanishwa katika kongamano litakalofanyika Aprili 27, 2025.
Amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa atazindua kongamano hilo likiwa na mada kuu ya tafakuri na mijadala juu ya historia, changamoto na fursa za uwekezaji katika sekta ya ushirika, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuondoa umaskini.
Amesema miongoni mwa washiriki ni viongozi wa kitaifa, wadau wa ushirika kutoka ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida.
Kuhusu uzinduzi, Senyamule amesema Rais Samia atatembelea makao makuu ya benki hiyo yaliyopo jijini Dodoma na maonyesho ya ushirika yatakayofanyika katika viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Amesema hiyo inaifanya kuwa benki inayofika karibu zaidi na wananchi, hasa wale waliokuwa hawajafikiwa na huduma za kifedha kwa muda mrefu.
Mmoja wa wakulima wa mbaazi mkoani Lindi, Sophia Yusuf ametaka benki hiyo kutoa riba ndogo katika mikopo itakayotoa kwa wakulima ili wengi wanufaike nayo.
"Kupata mitaji ya kuendeshea kilimo ni shida sana kutokana na mabenki na taasisi za kifedha kuhitaji dhamana ambazo sisi hatuna," amesema.