Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapato ya uvuvi yaongezeka Ziwa Tanganyika

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti

Muktasari:

  • Serikali imesema imevuna tani 38,999.82 za samaki katika kipindi cha miezi minne baada ya kufunguliwa Ziwa Tanganyika na kuingiza mapato ya Sh324.85 bilioni.


Dodoma. Baada ya kuzuiwa kwa muda uvuvi katika Ziwa Tanganyika, Serikali imesema mavuno ya samaki yameongezeka na kufikia tani 38,999.82 katika kipindi cha miezi minne baada ya kufunguliwa, hivyo kuingiza Sh324.85 bilioni.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema hayo bungeni leo Ijumaa Aprili 25, 2025 alipojibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani (Chadema).

“Mavuno hayo ni ongezeko ikilinganishwa na samaki tani 25,113.43 zenye thamani ya Sh166.47 bilioni zilizovuliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 55.3 ya mavuno yaliyopatikana mwaka 2023,” amesema.

Amesema mavuno hayo yametokana na matokeo chanya baada ya kuruhusu shughuli za uvuvi Septemba hadi Desemba 2024.

Katika swali la msingi, mbunge huyo amehoji ni yapi matokeo chanya baada ya kupumzisha Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu bila kufanya shughuli za uvuvi.

Pia alihoji ni kwa nini Serikali isiwalipe fidia wavuvi waliokata leseni za uvuvi kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini walizuiwa kuvua, hivyo kuwasababishia umaskini.

Mnyeti amesema thamani ya mauzo ya samaki nje kwa mwaka 2024 imeongezeka na kufikia Sh180.68 bilioni ikilinganishwa na Sh97.03 bilioni kwa mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 86.2.

Amesema Serikali ilipumzisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15, 2024 ikiwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA).

Amesema mkataba huo unalenga kuruhusu mifumo ya ikolojia kurejea, kutoa fursa kwa samaki kuzaliana, kukua na kuongezeka, hivyo kuwa na uvuvi endelevu.

Pia kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wavuvi na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa.

Akijibu swali kuhusu ulipaji wa fidia kwa wavuvi walikata leseni lakini hawakufanya kazi, Mnyeti amesema walishakuwa na mazungumzo ya muda mrefu na mbunge kuhusu suala hilo lakini mara zote amekuwa akikataa maelezo ya Serikali.