Kamati ya Bunge yawa mbogo mabasi ya mwendokasi kutotumika
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati hiyo, Florent Kyombo, walipotembelea karakana ya Mbagala Rangi Tatu, eneo ambako baadhi ya mabasi yaendayo haraka huhifadhiwa.
Muktasari:
- Kamati hiyo ipo kwa siku mbili jijini Dar es Salaam ambapo leo imetembelea mradi wa mabasi yaendayo haraka unaotekelezwa katika jiji la Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imegeuka mbogo baada ya kupata taarifa kuwa kuna mabasi ya mwendo wa haraka ‘mwendokasi’ yameletwa nchini lakini hadi sasa hayatumiki licha ya kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Wameyasema hayo leo Jumamosi Mei 9, 2026 walipofanya ziara ya kutembelea mradi wa mabasi hayo ambapo pamoja na mambo mengine walipokea taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa watoa huduma Kampuni ya Mofat kwa njia ya Mbagala na Kampuni ya Uendeshaji Mabasi ya Haraka (Udart) inayotoa huduma katika barabara ya Kimara.
Kauli hiyo inakuja ikiwa zimepita siku mbili tangu Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila, alipofanya ziara katika mradi huo na kuelezwa kuhusu changamoto hizo za mabasi kupaki kwa upande wa Mofat na kutoa maagizo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wakimsikiliza Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Mofat, Abdallah Mohammed, walipotembelea karakana ya mabasi ya mwendokasi eneo la Mbagala Rangi Tatu, Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka.
Katika maagizo hayo, Kafulila ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), amemtaka mwekezaji (Mofat) kuandaa ripoti ya tathmini ya nusu mwaka, itakayowasilishwa serikalini kupitia vikao vya juu, hususan Kamati ya Uendeshaji ya Ubia.
Ameeleza lengo ni kufanya marekebisho yatakayoufanya mradi uwe endelevu, wa mfano na usioleta changamoto kwa wawekezaji waliopo na wanaotarajia kuingia.
Aidha, baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, amesema PPPC itashirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali, ikiwemo vyombo vinavyosimamia mikataba, ili kushughulikia changamoto zilizopo.
Taarifa za Mofat na Udart kwa Kamati ya Bunge
Wakitoa taarifa kwa kamati hiyo, viongozi wa Mofat wamesema kati ya mabasi 200 waliyoleta, ambayo hadi sasa yapo barabarani ni 55 na katika hayo, 50 ndiyo yanafanya kazi kwa asilimia 100 huku matano yakiwekwa kwa ajili ya dharura ili yawe mbadala.
“Mpaka sasa mabasi tunayoweza kusema yanafanya kazi ni 55, huku mengine 145 tukiwa tumeyapaki yard tangu tulivyoyaleta kwa awamu tofauti kipindi cha mwaka jana,” amesema Philip Chalanga ambaye ni msemaji wa kampuni ya Mofat.
Hata hivyo amesema matarajio wakati wanaleta mabasi hayo ambayo yamewagharimu zaidi ya Sh200 bilioni, ilikuwa ni kusafirisha abiria 600,000 kwa siku lakini hadi sasa hata abiria 80,000 hawafiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Udart, Pius Ng’ingo, amesema hadi sasa magari yaliyoko barabarani ni 55. Kati ya hayo yapo 49 ambayo ni kati ya yale 99 mapya yaliyoingizwa mwaka jana na kubainisha watakuwa wanayaachia kadri ya uhitaji.
Ni kutokana na taarifa hiyo, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge akiwemo Hawa Lufunga, amehoji mabasi hayo yako yard yanafanya nini wakati uhitaji kwa barabara ya Mbagala walielezwa jumla yanatakiwa 700 huku mpaka sasa yaliyoletwa na mwekezaji Mofat ni mabasi 200 kati ya 255 anayotakiwa kuleta.
“Yanakuwaje yard wakati njia hiyo hakuna asiyejua kuwa ina uhitaji mkubwa wa usafiri huku kwa ile ya barabara ya Kimara-Mbezi taarifa zinaonyesha ina uhitaji wa zaidi ya mabasi 200?
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo katika hizi taasisi, watuambie maana haiwezekani miundombinu imeshakamilika ya kupita mabasi hayo, mama wa watu (Rais Samia Suluhu Hassan) anajitahidi kujenga, nini shida?” amehoji Hawa ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wakiwa ndani ya basi la mwendokasi wakati wa ziara ya kukagua mradi wa mabasi hayo jijini Dar es Salaam.
Amesema kama vipi, barabara ambazo zimeshakamilika Mofat wapewe ruti hizo kutoa huduma.
Hata hivyo Mbunge huyo amesema kama Serikali itaendelea kuwaondoa wakurugenzi wa taasisi zinazosimamia mradi huo huku chini ikawaacha wengine, jambo hilo halitasaidia.
Naye Mariam Ibrahim amesema kwa namna ya uendeshaji wa mradi huo ilivyo sasa, wawekezaji wengine wakisikia kuna mabasi yameletwa halafu yamepaki tu, kesho wakiitwa kuja kuwekeza hawatajitokeza.
“Ukiacha kuja kwa wawekezaji wapya, pia tunawavunja moyo wawekezaji walioleta mabasi yao, kwani hawa watu wana mikopo wameingia katika kununua vyombo hivyo,” amesema Mariam ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka Pwani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo, amesema wamezichukua changamoto hizo na wanachofanya ni kwenda kuziwasilisha kwa Serikali kuona nini kinaweza kufanywa kwa haraka ili mabasi yote hayo yaweze kuingia barabarani.
Kwa mujibu wa Kyombo, katika ziara hiyo walipokuwa wakipita kwenye barabara za mabasi hayo wamegundua bado uhitaji wa usafiri katika jiji la Dar es Salaam ni mkubwa.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange, amesema dhamira ya Serikali ni kuona wanapunguza changamoto ya usafiri Dar es Salaam na ndiyo maana inaendelea kujenga na kukamilisha miundombinu.
Amesema licha ya uwepo wa changamoto lakini wanashukuru wawekezaji wameleta mabasi yenye viwango vya kimataifa na lengo ni kuona yote yanaingia barabarani.
“Nataka niwahakikishie Watanzania Serikali inadhamiria kuondokana na ugonjwa sugu wa usafiri na tukitoka hapa tutaenda kukaa na wadau kuona namna gani wananchi wanafaidika na usafiri huo wa mwendokasi,” amesema.
Ilichosema Dart
Awali akitoa taarifa ya jumla ya mradi mzima, Mtendaji Mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Said Tunda, amesema mradi huo mzima una jumla ya kilometa 154 ukiwa na awamu sita ambapo mpaka sasa mbili ndiyo zimeanza kufanya kazi ambazo ni za Kimara na Mbagala.
Kwa barabara ya Kimara amesema ina urefu wa kilometa 20.9 huku ile ya Mbagala ikiwa na urefu wa kilometa 20.3.
Hata hivyo amesema miradi ya awamu hizo zinazofanya kazi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuharibiwa kwa miundombinu yake hususan mashine za ukatishaji tiketi, zilizoharibiwa katika matukio ya Oktoba 29.
“Tunashukuru tayari Serikali imeshatupatia Sh20.4 bilioni za kuikarabati miundombinu hiyo ambapo kwa sasa mkandarasi tayari yupo kazini,” amesema Tunda.
Aidha amesema katika moja ya mikakati yao ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma ya usafiri huo ambapo kwa sasa wanatarajia abiria kutumia alama za mikono na sura katika kukata tiketi badala ya kadi.
Akieleza moja ya sababu ya kuja na mfumo huo, amesema ni kutokana na kutumia gharama kubwa kutengeneza kadi hizo ambapo hutumia Sh5,000 kwa kadi moja halafu wanakuja kuiuza Sh1,000 jambo ambalo ni hasara kwao.
Jingine amesema kumekuwa na matumizi madogo ya kadi hizo kwa abiria na kueleza kuwa kati ya kadi 432,000 walizotengeneza, kadi zinazosoma kwenye mfumo wao hazizidi hata 100,000, ndiyo maana wakaona waje na mfumo huo ambao pia utasaidia abiria kuacha kuazimana kadi hizo.
Suala jingine wanalokuja nalo ukiacha kadi, amesema ni kuondoa adha ya abiria kutoa kichwa nje ya kituo kuangalia basi linalokuja na kutaka kujua linaenda wapi.
“Tukishafanya maboresho haya, ukikaa kwenye kituo utakuwa unaona basi linalokuja linaenda wapi na linafika muda gani na pia milango itakuwa inafunga na kujifungua yenyewe,” amesema Tunda.
Pia mtendaji huyo aligusia adha ya mabasi ya Mofat yaliyopakiwa hadi sasa ambapo amesema hali hiyo inachangiwa na abiria kutumia usafiri mwingine ikiwemo daladala.
Amesema mpaka sasa kwa barabara hiyo ya Mbagala zipo daladala 7,500 zikiwa zinabeba abiria 450,000 kila siku huku kwenye mwendokasi abiria wanaobebwa hawafiki hata 100,000 na kuitaka kamati kulibeba hilo kuona namna gani litatafutiwa suluhu.