Mabasi 150 ya Mofat yatimiza nusu mwaka bila kuingia barabarani, Kafulila aingilia kati
Muktasari:
- Mofat ilianza kutoa huduma zake tangu Oktoba 2025 na mpaka sasa imeshaleta jumla ya mabasi 200 kila moja likiwa na uwezo wa kubeba abiria 165.
Dar es Salaam. Zaidi ya mabasi 150 ya mwendo wa haraka (mwendokasi) yaliyoletwa kwa ajili ya kutoa huduma katika barabara ya Mbagala, yamekaa kwa zaidi ya nusu mwaka bila kuanza kazi.
Hayo yameelezwa leo Jumatano, Mei 6, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, alipofanya ziara ya kukagua mradi huo eneo la Mbagala.
Kampuni ya Mofat, ambayo ni ya kizalendo, ilianza kutoa huduma Oktoba 2025 na hadi sasa imeingiza mabasi 200, kila moja likiwa na uwezo wa kubeba abiria 165.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, akiwa anapata maelezo kutoka kwa Mkurugezni Mtendaji wa kampuni ya Mofat, Mohammed Kassim Abdallah, alipofanya ziara ya kutembelea mradi wa Mabasi Yaendayo haraka’ mwendokasi’ barabara ya Mbagala
Kafulila amesema ziara yake imelenga kukagua utekelezaji wa mradi pamoja na kusikiliza changamoto za mwekezaji, akisisitiza kuwa ni mradi muhimu kwa Jiji la Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni kuwepo kwa mabasi zaidi ya 150 yaliyokamilika nyaraka zote, ikiwemo bima, lakini yameegeshwa katika kituo kikuu cha Mbagala Rangi Tatu kwa kukosa nafasi ya kuanza kazi katika baadhi ya maeneo.
“Kwa sasa ni takribani mabasi 50 pekee ndiyo yanafanya kazi, huku zaidi ya 150 yakiwa yameegeshwa kwa zaidi ya nusu mwaka, jambo linalosababisha hasara kwa mwekezaji,” alisema Kafulila.
Ameongeza kuwa hali hiyo imeathiri uwekezaji huo ambao pia unahusisha mikopo kutoka benki, hivyo kuna umuhimu wa kutafuta suluhu ya haraka.
Kwa mujibu wa Kafulila ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), wamekubaliana na mwekezaji kuandaa ripoti ya tathmini ya nusu mwaka, itakayowasilishwa serikalini kupitia vikao vya juu, hususan Kamati ya Uendeshaji ya Ubia.
Msemaji wa Mofat, Philip Changala
“Lengo ni kufanya marekebisho yatakayoufanya mradi uwe endelevu, wa mfano na usioleta changamoto kwa wawekezaji waliopo na wanaotarajia kuingia,” alisema.
Amesema baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, PPPC itashirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali, ikiwemo vyombo vinavyosimamia mikataba, ili kushughulikia changamoto zilizopo.
Hata hivyo, Kafulila amesema uwepo wa mabasi hayo mengi pia ni ishara nzuri kuwa jiji lina uwezo wa kuwa na huduma ya kutosha ya usafiri wa umma.
Kwa upande wake, Msemaji wa Mofat, Philip Changala amesema ujio wa Kafulila umewasaidia kuelewa zaidi namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
Amesema licha ya changamoto, mahitaji ya huduma yanaendelea kuongezeka na tayari wameanza kutoa huduma maalumu kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, wafanyabiashara wa samaki na abiria wanaohitaji usafiri wa haraka.
Changala amewataka wananchi kuendelea kutumia huduma hizo, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu miundombinu ya mwendokasi kwa kuepuka kutumia njia zake kinyume cha sheria.
Baadhi ya wananchi, akiwemo Raphael James, walipendekeza mabasi hayo ya ziada yaelekezwe katika barabara zilizokamilika, kama Gongo la Mboto, ili kupunguza adha ya usafiri.
Hivi karibuni, Meneja wa ujenzi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Frank Mbilinyi, alisema ujenzi wa barabara ya Gongo la Mboto umefikia asilimia 99, huku kilichobaki kikiwa ni uwekaji wa mifumo ya umeme na taa za kuongoza magari.