Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chalamila apendekeza vyombo vya dola kutoa huduma mradi wa mwendokasi

Barabara ya Mwendokasi ya Mbezi-Kimara mpaka Kariakoo. Picha na Mtandao 

Muktasari:

  • Amesema iwapo vyombo hivyo vitapewa nafasi ya kuendesha baadhi ya mabasi ya mwendokasi, wananchi wa kawaida watakuwa wakitumia huduma hizo kila siku na hivyo kuongeza mshikamano na kuimarisha mahusiano baina ya jamii na askari.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amependekeza vyombo vya dola vikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kushirikishwa katika utoaji wa huduma za mabasi yaendayo haraka (BRT), akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya uongozi ngazi ya juu na uongozi daraja la pili kwa maofisa wa Jeshi la Magereza, Chalamila amesema ushiriki wa vyombo hivyo katika huduma za usafiri wa umma unaweza kusaidia wananchi kuyaona majeshi hayo kwa ukaribu zaidi badala ya kuyaogopa.

Amesema iwapo vyombo hivyo vitapewa nafasi ya kuendesha baadhi ya mabasi ya mwendokasi, wananchi wa kawaida watakuwa wakitumia huduma hizo kila siku na hivyo kuongeza mshikamano na kuimarisha mahusiano baina ya jamii na askari.

“Nimependekeza kwa Rais kwamba hata vyombo vya dola kama Magereza, Polisi na JWTZ vipewe nafasi ya kuendesha mabasi ya mwendokasi. Hii itasaidia wananchi kuwa karibu zaidi na vyombo vyao vya usalama,” amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inaweza pia kuwa chanzo cha mapato kwa vyombo hivyo kupitia huduma za usafiri, fedha ambazo zinaweza kusaidia katika baadhi ya mahitaji yao ya kila siku.

Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Mkoa pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaoendelea kufanyika jijini Dar es Salaam.

Akitolea mfano, amesema barabara hiyo ya mwendokasi njia ya Gongo la Mboto imejengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh231 bilioni na inatarajiwa kuanza kutoa huduma za mabasi yaendayo haraka hivi karibuni.

Amesema maboresho hayo ya miundombinu yataendelea kusaidia kupunguza changamoto za usafiri na msongamano wa magari katika jiji hilo.

Chalamila pia amezungumzia hali ya vyombo vya usalama akieleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa majeshi mbalimbali, ikiwemo kuondoa changamoto ya magari chakavu ndani ya Jeshi la Magereza.

Amesema kwa sasa jeshi hilo lina mabasi mapya na ya kisasa ambayo yameongeza hadhi ya jeshi hilo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma.

Akizungumzia hali ya usalama mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema hadi kufikia siku hiyo Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na jumla ya wahalifu 2,284 waliopo katika magereza manne.

Amewapongeza viongozi wa Jeshi la Magereza kwa juhudi wanazofanya kurekebisha tabia za wafungwa na kuwasaidia kurejea katika jamii wakiwa raia wema baada ya kutumikia vifungo vyao.