Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hapi aishauri TK Movements kuanza uzalishaji

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Ally Hapi akizungumza na Mtandao wa Vijana wa Taifa Letu Kesho Yetu (TK Movement), waliokutana jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwa Mtandao wa Vijana wa Taifa Letu, Kesho Yetu (TK Movement), vijana waliojiunga na umoja huo wameshauriwa kuchangishana ili kupata mtaji wa kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ally Hapi, amewashauri Mtandao wa Vijana wa Taifa Letu Kesho Yetu (TK Movements) kuungana na kuchangishana ili kuanzisha miradi itakayowawezesha kupata kipato na kukuza uchumi wao.

Mtandao huo ulizinduliwa Mei 25, 2024 na Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu, ambaye aliwasihi vijana kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili waweze kuchagua viongozi bora katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Hapi ameyasema hayo leo, Mei 3, 2025, wakati akifungua semina ya kitaifa kwa viongozi wa mikoa na wilaya wa mtandao huo, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Amesema kuwa, kwa kuwa mtandao huo una wanachama zaidi ya milioni mbili nchini, wakichangishana fedha wanaweza kupata mitaji ya kuanzisha mashamba na biashara kubwa zitakazowawezesha kuongeza vipato vyao.

“Kila mmoja akitoa Sh10,000 mnapata shilingi ngapi ambazo mnaweza kuzipeleka kama mtaji wa kuanzisha shughuli zikawazalishia,”amehoji Hapi ambaye alijinasibu kuwa alipowekwa pembeni baada ya kutoka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, alianzisha kilimo ambacho kilimwezesha kupata kipato.

Aidha, Hapi amewataka vijana hao kuchukulia changamoto wanazokutana nazo kama fursa katika safari yao ya kuelekea mafanikio, na wasikubali kurudishwa nyuma na mtu yeyote.

“Mafanikio matamu ni yale ambayo mtu ameyapata baada ya kukabiliana na changamoto wakati akiyatafuta, msirudi nyuma. Mimi nimezichukua changamoto zenu. Kama mnawajua (wanaowaletea changamoto) tutafuta mawasiliano nao,”amesema.

Pia, amewataka wanachama hao kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na kuwahamasisha wenzao kufanya hivyo, ili itakapofika wakati wa kupiga kura wajitokeze kwa wingi na kutimiza haki yao ya Kikatiba.

Awali, Mratibu wa mtandao huo, Ramadhan Magambo, alimuomba Hapi kusaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo tatizo la mahusiano hafifu kati ya viongozi na mtandao huo.

“Wanachama wamekuwa wakiuliza maswali, mimi ninakosa majibu, malengo ya mtandao wetu ni kuisuport Serikali na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan lakini baadhi ya wateule wa  Rais ndio wanaokwamisha,”amesema Magambo.

Amesema mkutano huo umehudhuriwa na waratibu wa mtandao huo kutoka mikoa yote nchini, zaidi ya 600 kwa jumla.