Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Deni la Taifa lafikia Sh107.7 trilioni, nchi bado inakopesheka

Muktasari:

  • Deni la Taifa lilifikia Sh107.7 trilioni kutoka Sh91.7 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 14.9.  Kati ya hizo, deni la ndani ni Sh34.25 trilioni na lile la nje likiwa dola za Marekani 26.67 bilioni.

Dar es Salaam. Wakati pato halisi la Taifa likifikia Sh156.6 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh148.5 trilioni mwaka uliotangulia, hadi kufikia Machi 2025, deni la Taifa limefikia Sh107.7 trilioni kutoka Sh91.7 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 14.9.

Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango Na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameyasema hayo leo Juni 12, 2025 wakati akiwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/26.

Profesa Mkumbo amesema kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa Sh34.76 trilioni.

“Ongezeko la deni lilitokana na Serikali kuendelea kupokea mikopo mipya kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji,” amesema.

Amesema deni la Serikali la nje limefikia dola za Marekani 26.67 bilioni, ikilinganishwa na dola za Marekani 23.72 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 12.4.

“Ongezeko hilo lilitokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo ya zamani na mipya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Pia mashirika ya fedha ya kimataifa yaliendelea kuongoza kwa kuchangia asilimia 67.8 ya deni lote la nje, ikilinganishwa na asilimia 63.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2024,” amesema.

Pia benki za biashara zilichangia asilimia 26.9 na washirika wa maendeleo walichangia asilimia 5.3 ya deni lote la nje.

Kwa upande wa deni la ndani, hadi Machi 2025, lilikuwa Sh34.25 trilioni ikilinganishwa na Sh30.7 trilioni za kipindi kama hicho mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 11.4.

“Katika kipindi hicho, mikopo ya hatifungani iliendelea kuwa sehemu kubwa ya deni la ndani ikiwa ni asilimia 66.5. Aidha, dhamana za Serikali za muda mfupi zilikuwa asilimia 5.5 na hati fungani maalumu asilimia 13.0,” imeelezwa.

Taarifa inaeleza, hadi kipindi husika benki za biashara ziliendelea kuongoza kwa kuhodhi asilimia 37.1 ya deni la ndani, ikilinganishwa na asilimia 42.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Mifuko ya hifadhi ya jamii ilihodhi asilimia 33.9 ikifuatiwa na watu binafsi asilimia 14.6 na kampuni za bima asilimia 6.9.

“Kumekuwepo na hamasa na ongezeko la ushiriki wa watu binafsi katika dhamana za Serikali kutoka asilimia 8.0 Machi 2023 hadi asilimia 14.6 Machi 2025, kufuatia kuendelea kutolewa kwa elimu kwa umma,” amesema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa tathmini ya uhimilivu wa Deni iliyofanyika Oktoba, 2024 ilionyesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu.

“Kwa mujibu wa tathmini hiyo, viashiria vya deni vilionyesha kuwa mwaka 2024/25, thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 24.1, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40, thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180,” imeelezwa.

Pia ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato yatokanayo na mauzo ya nje ni asilimia 13.9, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 15 inayotakiwa, huku ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani ukiwa asilimia 17.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 18.

“Kwa upande wa viashiria vya deni lote (deni la nje na ndani), thamani ya sasa ya deni kwa pato la Taifa ni asilimia 40.3 ikilinganisha na ukomo wa asilimia 55,” amesema akisisitiza deni hilo ni himilivu.


Uwezo wa kukopesheka

Machi 2025, Kampuni ya Moody’s Investors Services ilifanya mapitio ya pili ya uchumi wa Tanzania ili kubaini uwezo wa nchi kukopesheka.

Katika mapitio hayo, Tanzania iliendelea kubaki katika daraja la B1 ikiwa ni mtazamo thabiti (Stable Outlook) kama ilivyokuwa Machi 2024. Daraja hili la B1 linaashiria kuendelea kuimarika kwa uchumi wa nchi na uwezo wa nchi kuhimili misukosuko ya kiuchumi kutoka nje.

Kampuni nyingine ya Fitch Ratings nayo ilifanya mapitio kama hayo Desemba 2024 na kuipa Tanzania alama ya B+ ikiwa na mtazamo thabiti (Stable Outlook) kama ilivyokuwa Juni 2024.

“Matokeo hayo ni muhimu katika kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya Serikali na sekta binafsi,” amesema.