DC Songwe asimamisha shughuli za uchimbaji madini

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini Kata ya Saza wakati alipofika kujaribu kutatua mgogoro wa wananchi na wachimbaji. Picha Stephano Simbeye.
Songwe. Mkuu wa Wilaya ya Songwe mkoani hapa, Solomon Itunda amesimamisha shughuli za uchimbaji madini katika Kata ya Saza kwa muda wa siku saba, ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia mgogoro kati ya wananchi na wachimbaji wadogo.
Uamuzi huo ameutoa leo Jumatatu Agosti 21, mwaka huu baada ya kusikiliza malalamiko ya pande zote mbili katika mgogoro huo ambao unadaiwa kuwa ni wa muda mrefu ambapo amesema Serikali imebaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa ambayo yamekuwa chanzo cha mgogoro.
"Ili kufanya maamuzi katika mazingira kama haya ni vyema na ni busara ukafanya uchambuzi wa kina ambao utakuongoza kufanya maamuzi na pande zote zikaridhika na hasa kuzingatia Sheria ya Madini sura 123 namba 95 kifungu cha kwanza kama kinavyotaka," amesema Itunda.
Aidha Itunda amesema baada ya kusikiliza pande zote amebaini mambo kadhaa ikiwemo kaya 15 kuhusika, ambapo kati yake zipo ambazo wakazi wake wameingia makubaliano na wawekezaji (wachimbaji) na nyingine hakuna makubaliano yoyote, uwepo wa wachimbaji ambao hawana leseni na ambao wamevamia maeneo wanayochimba.
Mkuu huyo wa wilaya ameagiza Idara ya Madini ishirikiane na Idara ya Ardhi na nyingine zinazohusiana na maendeleo ya jamii ili kupitia kila kaya yenye malalamiko na kufanya tathimini ya hali ilivyo na kuandika ripoti maalumu kuzingatia usalama wa makazi ya watu na watoto wadogo wanaoishi maeneo hayo.
"Baada ya tathimini hiyo kufanyika kabla ya Agosti 30, mwaka huu tutakuja hapa tufanye maamuzi ya mwisho ili shughuli za uchumi ziendelee," amesema Itunda.
Ameongeza kuwa Serikali inathamini sekta ya madini kwa mchango wake kiuchumi kwani mwaka jana iliingiza pato la Sh27 bilioni na hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu zilikuwa zimekisanywa zaidi ya Sh32 bilioni.
Mjumbe wa nyumba 10 katika eneo la Kibaoni Getruda Patrick amesema mgogoro uliopo eneo hilo unahusisha watu wa aina tofauti, wapo ambao katika makazi yao wanafanya uchimbaji, lakini pia wapo ambao wameingia ubia na wachimbaji kwa lengo la kugawana mapato.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Sala Mwansasu amesema kilio chao ni kutokuwa na uhakika wa usalama wao kuhusiana na milipuko inayofanywa na wachimbaji ambayo inasababisha nyumba zao kupata nyufa, vumbi kutimka na usalama wa watoto kuhusu mashimo yanayoachwa wazi ni mdogo.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wilayani Songwe Steven Mushi amesema tayari wameanza mazungumzo ya kuwahamisha wananchi katika eneo la machimbo na baadhi yao wanakubali kuhama na wengine wanataka kuingia ubia na wachimbaji.
"Kuhusu uamuzi wa kusimamisha shughuli za uchimbaji utasababisha hasara kwetu, kama mimi nina vibarua 30 ambao katika kipindi cha siku Saba wataendelea kula bila kuzalisha, lakini hatuna namna tunalazimika kuukubali," amesema Steven.