Changamoto zinazoikabili kahawa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Boniphace Simbachawene akizungumza katika mkutano mkuu wa wadau wa Kahawa Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Miongoni mwa changamoto hizo ni ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, kushuka kwa ubora wa kahawa, udanganyifu katika mizani, ukosefu wa takwimu sahihi na uuzaji wa kahawa hewa kwenye minada.
Dodoma. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Boniphace Simbachawene ametaja changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo cha kahawa nchini, ikiwamo upotevu wa fedha za wakulima unaosababishwa na viongozi wa baadhi ya vyama vya ushirika kutokuwa waaminifu na kuingia mikataba ya ununuzi wa kahawa bila kufuata utaratibu.
Akizungumza leo Julai 5, 2025, katika mkutano wa 15 wa wadau wa kahawa, Simbachawene amesema changamoto nyingine ni kutozingatia taratibu za masoko, ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, kushuka kwa ubora wa kahawa, udanganyifu katika mizani, ukosefu wa takwimu sahihi na uuzaji wa kahawa hewa kwenye minada.
Amesema Serikali imeboresha mifumo ya masoko ya kahawa kupitia ushirika, lakini bado wakulima wanakabiliwa na vikwazo vinavyohitaji kutatuliwa ili kufikia malengo ya Serikali na wadau wa mnyororo wa thamani wa kahawa.
“Pamoja na jitihada zilizopo, bado kuna viongozi wa vyama vya ushirika ambao si waaminifu, wanaingia mikataba isiyo rasmi na kuharibu mfumo mzima wa masoko. Vilevile, kuchelewa kwa malipo kwa wakulima na biashara isiyo rasmi inasababisha kushuka kwa ubora wa kahawa kwa kuwa, kahawa inayokusanywa bila utaratibu haizingatii viwango vya ubora,” amesema.
Amesema udanganyifu kwenye uzito wa kahawa na ukosefu wa takwimu sahihi, umechangia migogoro isiyo ya lazima na kudumaza maendeleo ya tasnia.

Wadau wa Kahawa wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka jijini Dodoma.
Aidha, amesema katika baadhi ya maeneo kama Kagera, viongozi wa vyama waliwasilisha taarifa za kahawa ambazo hazipo kwenye maghala yao, jambo lililosababisha upotevu wa fedha na migogoro.
Ameagiza wakulima na wadau kuhakikisha wanakusanya na kutumia takwimu sahihi na kutumia mkutano huo kama fursa ya kujadili changamoto na kutafuta suluhu za kudumu.
Aidha, Simbachawene amesema Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh294 bilioni mwaka 2021/22 hadi zaidi ya Sh1.3 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26, ili kuboresha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakati, ikiwamo mbegu bora, mbolea, huduma za ugani na maji.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, amesema tasnia hiyo ilikuwa na mkakati wa kuzalisha tani 300,000 za kahawa kwa mwaka, lakini kwa sasa inazalisha tani 85,000 pekee.
“Ingawa hatujafikia lengo, bado tunaendelea kusonga mbele. Tumeamua kufanya mapitio ili kubaini maeneo ya kuboresha, ikiwamo kugawa bure miche ya kahawa kwa wakulima, sasa tunatoa miche milioni 20,” amesema.
Ameongeza kuwa, hatua nyingine ni kupanua mashamba, kufanyia marekebisho miti ya kahawa iliyozeeka ili ichipue upya na kuhakikisha ushirikishwaji katika mnyororo wa thamani, sambamba na kushirikiana na halmashauri kutoa elimu kwa maofisa ugani.
Mmoja wa wakulima, Respicious John amesema mkutano huo umejikita kujadili namna ya kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 300,000 na kwamba ni muhimu vijana kuwekeza katika kilimo cha kahawa.
“Vijana wengi hawajitokezi kuwekeza, lakini huku ndiko kwenye uchumi. Kahawa ni fursa, ni uchumi wetu. Kwa mfano, mwaka uliopita Mkoa wa Kagera uliingiza Sh250 bilioni kutokana na mauzo ya kahawa,” amesema.