Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bwawa la Nyerere lakamilika, sasa lazalisha umeme megawati 2,115

Muktasari:

  • Hatimaye mashine zote tisa za kuzalisha umeme katika Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP), zimekamilika.

Rufiji. Ndoto iliyoanzishwa kwa matumaini makubwa imefikia tamati leo, baada ya mitambo yote tisa ya kufua umeme katika mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP) kuanza kufua umeme kwa uwezo wake wote wa megawati 2,115.

Hii ni baada ya mtambo wa tisa na wa mwisho kuwashwa rasmi leo na kuanza kuzalisha umeme, huku mradi mzima ukikamilika kama alivyosema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko alipotembelea mradi huo leo Jumamosi, Aprili 5, 2025.

Bwawa hili lina jumla ya mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 235, na hivyo kufikia jumla ya megawati 2,115.

Huu ni mradi wa kihistoria ambao umegharimu Sh6.5 trilioni na hadi sasa, asilimia 99.5 ya fedha zote zimeshalipwa na Serikali.

Ujenzi wa mradi huo wa kufua umeme wa maji kutoka Mto Rufiji, mpakani mwa mikoa ya Pwani na Morogoro ulizinduliwa rasmi Julai 26, 2019 na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli.

Dk Biteko amesema kuwa mashine ya kwanza ya kuzalisha umeme iliwashwa Februari mwaka jana, na sasa baada ya kumalizika kwa mitambo yote, uzalishaji umekamilika.

Muonekano wa mtambo namba tisa na wa mwisho wa kuzalisha umeme katika mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere

“Huu ni ushahidi wa jitihada kubwa na dhamira ya Serikali kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kutosha kwa wananchi wote," amesema Dk Biteko.

Amesema mradi huo, unaozalisha umeme wa kutosha kwa mahitaji ya Taifa, unatoa matumaini ya kukuza uchumi, viwanda na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa mujibu wa Dk Biteko, Serikali ya awamu ya sita iliupokea mradi huo ukiwa umefikia asilimia 30, lakini sasa umekamilika na unafanyika utaratibu wa kumwalika Rais Samia Suluhu Hassan kuuzindua.

Amesema tayari upande wa Misri wamethibitisha mkuu wao wa nchi atawasili nchini kushuhudia uzinduzi na kinachosubiriwa ni kupangwa ratiba ya tukio hilo.

"Ni furaha mitambo yote imekamilika inazalisha umeme na ile ndoto ya kupata umeme kutoka katika bwawa hili imekamilika na umeme unapatikana," amesema.

Kutokana na uwezo wa nchi kuzalisha kiwango kikubwa cha umeme, amesema kwa sasa Serikali inakamilisha mazungumzo na Zambia kwa ajili ya kuiuzia umeme na laini ya kuusafirisha inajengwa.

Mitambo yote tisa ya kufua umeme katika mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP) imekamilika na sasa kuanza kufua umeme kwa uwezo wake wote wa megawati 2,115.

Bwawa hili lina jumla ya mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 235, na hivyo kufikia jumla ya megawati 2,115.

Amesema kwa upande wa Zambia nao wanajenga njia katika eneo lao kwa ajili ya kupokea umeme huo, hivyo Tanzania itanufaika na biashara hiyo ya nishati.

Baada ya hatua hiyo ya mradi wa JHPP, Dk Biteko amesema kwa sasa Serikali inaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme ili kuwafikia Watanzania.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni amesema kukamilika kwa mradi huo ni kama muujiza kutokana na ukubwa wake.

Kwa kutambua kuwa mradi huo unategemea maji, amesema wizara yake inashirikiana na sekta nyingine kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoweza kuathiri vyanzo vya maji.

"Tutaendelea kufanya kazi na wizara zote kuhakikisha tunalinda vyanzo vya maji ili mradi usiathiriwe baadaye," amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema hatua iliyofikiwa inathibitisha nchi imefanikiwa kufikia uhuru wa kiuchumi.

Amesema hakuna namna ya kupata uhuru wa kiuchumi iwapo haujajitegemea katika nishati ya umeme na kukamilika kwa mradi huo ni hatua nzuri ya kiuchumi.

"Hii ndio iliyokuwa ndoto ya hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kuhakikisha nchi inajitegemea kwa nishati ya umeme," amesema.